1 Wakamjia Mafarisayo
na Masadukayo, wakamjaribu, wakamwomba awaonyeshe ishara itokayo mbinguni.
2 Akajibu, akawaambia,
[Kukiwa jioni, mwasema, Kutakuwa na kianga; kwa maana mbingu ni nyekundu.
3 Na asubuhi, mwasema,
Leo kutakuwa na dhoruba; kwa maana mbingu ni nyekundu, tena kumetanda. Enyi
wanafiki, mwajua kuutambua uso wa mbingu; lakini, je! Ishara za zamani hizi
hamwezi kuzitambua?]
4 Kizazi kibaya na cha
zinaa chataka ishara; wala hakitapewa ishara, isipokuwa ishara ya Yona.
Akawaacha, akaenda zake.
5 Nao wanafunzi
wakaenda hata ng'ambo, wakasahau kuchukua mikate.
6 Yesu akawaambia,
Angalieni, jilindeni na chachu ya Mafarisayo na Masadukayo.
7 Wakabishana wao kwa
wao, wakisema, Ni kwa sababu hatukuchukua mikate.
8 Naye Yesu akafahamu,
akawaambia, Mbona mnabishana ninyi kwa ninyi, enyi wa imani chache, kwa sababu
hamna mikate?
9 Hamjafahamu bado,
wala hamkumbuki ile mikate mitano kwa wale elfu tano, na vikapu vingapi
mlivyoviokota?
10 Wala ile mikate saba
kwa watu elfu nne, na makanda mangapi mliyoyaokota?
11 Imekuwaje hamkufahamu
ya kuwa si kwa sababu ya mkate naliwaambia? Ila jilindeni na chachu ya
Mafarisayo na Masadukayo.
12 Ndipo walipofahamu ya
kuwa hakuwaambia kujilinda na chachu ya mkate, bali na mafundisho ya Mafarisayo
na Masadukayo.
13 Basi Yesu akaenda
pande za Kaisaria-Filipi, akawauliza wanafunzi wake akasema, Watu hunena Mwana
wa Adamu kuwa ni nani?
14 Wakasema, Wengine
hunena u Yohana Mbatizaji, wengine Eliya, wengine Yeremia au mmojawapo wa
manabii.
15 Akawaambia, Nanyi
mwaninena mimi kuwa ni nani?
16 Simoni Petro akajibu
akasema, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.
17 Yesu akajibu,
akamwambia, Heri wewe Simoni Bar-yona; kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia
hili, bali Baba yangu aliye mbinguni.
18 Nami nakuambia, Wewe
ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya
kuzimu haitalishinda.
19 Nami nitakupa wewe
funguo za ufalme wa mbinguni; na lo lote utakalolifunga duniani, litakuwa
limefungwa mbinguni; na lo lote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa
mbinguni.
20 Ndipo alipowakataza
sana wanafunzi wake wasimwambie mtu ye yote ya kwamba yeye ndiye Kristo.
21 Tangu wakati huo Yesu
alianza kuwaonya wanafunzi wake ya kwamba imempasa kwenda Yerusalemu, na kupata
mateso mengi kwa wazee na wakuu wa makuhani, na waandishi, na kuuawa, na siku
ya tatu kufufuka.
22 Petro akamchukua,
akaanza kumkemea, akisema, Hasha, Bwana, hayo hayatakupata.
23 Akageuka, akamwambia
Petro, Nenda nyuma yangu, Shetani; u kikwazo kwangu; maana huyawazi yaliyo ya
Mungu, bali ya wanadamu.
24 Wakati huo Yesu
aliwaambia wanafunzi wake, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe,
ajitwike msalaba wake, anifuate.
25 Kwa kuwa mtu atakaye
kuiokoa nafsi yake, ataipoteza; na mtu atakayepoteza nafsi yake kwa ajili
yangu, ataiona.
26 Kwani atafaidiwa nini
mtu akiupata ulimwengu wote, na kupata hasara ya nafsi yake? Au mtu atatoa nini
badala ya nafsi yake?
27 Kwa sababu Mwana wa
Adamu atakuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika zake; ndipo
atakapomlipa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake.
28 Amin, nawaambieni,
Pana watu katika hawa wasimamao hapa, ambao hawataonja mauti kabisa, hata
watakapomwona Mwana wa Adamu akija katika ufalme wake.