2 PETRO - SURA YA 2

1 Lakini kuliondokea manabii wa uongo katika wale watu, kama vile kwenu kutakavyokuwako waalimu wa uongo, watakaoingiza kwa werevu uzushi wa kupoteza, wakimkana hata Bwana aliyewanunua, wakijiletea uharibifu usiokawia. 
2 Na wengi watafuata ufisadi wao; na kwa hao njia ya kweli itatukanwa. 
3 Na katika kutamani watajipatia faida kwenu kwa maneno yaliyotungwa; ambao hukumu yao tangu zamani haikawii, wala uvunjifu wao hausinzii. 
4 Kwa maana ikiwa Mungu hakuwaachilia malaika waliokosa, bali aliwatupa shimoni, akawatia katika vifungo vya giza, walindwe hata ije hukumu; 
5 wala hakuuachilia ulimwengu wa kale, bali alimhifadhi Nuhu, mjumbe wa haki, na watu wengine saba, hapo alipoleta Gharika juu ya ulimwengu wa wasiomcha Mungu; 
6 tena akaihukumu miji ya Sodoma na Gomora, akiipindua na kuifanya majivu, akaifanya iwe ishara kwa watu watakaokuwa hawamchi Mungu baada ya haya; 
7 akamwokoa Lutu, yule mwenye haki aliyehuzunishwa sana na mwenendo wa ufisadi wa hao wahalifu; 
8 maana mtu huyu mwenye haki akikaa kati yao, kwa kuona na kusikia, alijitesa roho yake yenye haki, siku baada ya siku, kwa matendo yao yasiyo na sheria; 
9 basi, Bwana ajua kuwaokoa watauwa na majaribu, na kuwaweka wasio haki katika hali ya adhabu hata siku ya hukumu; 
10 na hasa wale waufuatao mwili katika tamaa ya mambo machafu. na kudharau mamlaka. 
11 Wenye ushupavu, wenye kujikinai, hawatetemeki wakiyatukana matukufu; ijapokuwa malaika ambao ni wakuu zaidi kwa uwezo na nguvu, hawaleti mashitaka mabaya juu yao mbele za Bwana. 
12 Lakini hao kama wanyama wasio na akili, ambao walizaliwa kama wanyama tu wa kukamatwa na kupotezwa, wakikufuru katika mambo wasiyoyajua, wataangamizwa katika maangamizo yao; 
13 Wakipatikana na madhara, ambayo ni ujira wa udhalimu wao, wakidhania kuwa ulevi wakati wa mchana ni anasa; wamekuwa ni mawaa na aibu wakifuata anasa zisizo kiasi katika karamu zao za upendo, wafanyapo karamu pamoja nanyi; 
14 wenye macho yajaayo uzinzi, watu wasiokoma kutenda dhambi, wenye kuhadaa roho zisizo imara, wenye mioyo iliyozoezwa kutamani, wana wa laana; 
15 wakiiacha njia iliyonyoka, wakapotea, wakiifuata njia ya Balaamu, mwana wa Beori, aliyependa ujira wa udhalimu; 
16 lakini alikaripiwa kwa uhalifu wake mwenyewe; punda, asiyeweza kusema, akinena kwa sauti ya kibinadamu, aliuzuia wazimu wa nabii yule. 
17 Hawa ni visima visivyo na maji, na mawingu yachukuliwayo na tufani, ambao weusi wa giza ni akiba waliyowekewa. 
18 Maana wakinena maneno makuu mno ya kiburi, kwa tamaa za mwili na kwa ufisadi huwahadaa watu walioanza kuwakimbia wale wanaoenenda katika udanganyifu; 
19 wakiwaahidia uhuru, nao wenyewe ni watumwa wa uharibifu, maana mtu akishindwa na mtu huwa mtumwa wa mtu yule. 
20 Kwa maana wale waliokwisha kuyakimbia machafu ya dunia kwa kumjua Bwana na Mwokozi Yesu Kristo, kama wakinaswa tena na kushindwa, hali yao ya mwisho imekuwa mbaya kuliko ile ya kwanza. 
21 Maana ingekuwa heri kwao kama wasingaliijua njia ya haki, kuliko kuijua, kisha kuiacha ile amri takatifu waliyopewa. 
22 Lakini imetukia kwao sawasawa na ile mithali ya kweli, Mbwa ameyarudia matapiko yake mwenyewe, na nguruwe aliyeoshwa amerudi kugaa-gaa matopeni.

TUMA KWA RAFIKI :

Twitter FacebookMore

 
Kuhusu Huduma Hii | Masharti Ya Utumiaji Wa Tovuti Hii | Wasiliana Nasi | Tangaza Kupitia Tovuti Hii