EZEKIELI - SURA YA 43

1 Kisha akanileta mpaka langoni, yaani, lango lile lielekealo upande wa mashariki; 
2 na tazama, huo utukufu wa Mungu wa Israeli ulitokea kwa njia ya mashariki; na sauti yake ilikuwa kama mshindo wa maji mengi, nayo nchi iling'aa kwa utukufu wake. 
3 Na maono niliyoyaona yalikuwa kama maono niliyoyaona nilipokuja kuuharibu mji; nayo maono niliyoyaona yalikuwa kama maono niliyoyaona karibu na mto wa Kebari; nikaanguka kifudifudi. 
4 Na huo utukufu wa Bwana ukaingia ndani ya nyumba, kwa njia ya lango lile lielekealo upande wa mashariki. 
5 Kisha Roho ikaniinua, ikanichukua mpaka ua wa ndani; na tazama, utukufu wa Bwana uliijaza nyumba. 
6 Nikasikia sauti ya mmoja asemaye nami, itokayo katika nyumba hiyo; na mtu akasimama karibu nami. 
7 Akaniambia, Mwanadamu, hapa ni mahali pa kiti changu cha enzi, na mahali pa nyayo za miguu yangu, nitakapokaa kati ya wana wa Israeli milele; na nyumba ya Israeli hawatalinajisi jina langu takatifu tena, wao, wala wafalme wao, kwa mambo yao ya kikahaba, na kwa mizoga ya wafalme wao, katika mahali pao pa juu; 
8 kwa kuweka kizingiti chao karibu na kizingiti changu; na mwimo wao karibu na mwimo wangu; tena palikuwa na ukuta tu kati ya mimi na wao; nao wamelinajisi jina langu takatifu kwa machukizo yao waliyoyatenda; basi, kwa sababu hiyo, nimewakomesha katika hasira yangu. 
9 Basi sasa wayaondoe mambo yao ya kikahaba, na mizoga ya wafalme wao, yawe mbali nami, nami nitakaa kati yao milele. 
10 Na wewe, mwanadamu, waonyeshe wana wa Israeli nyumba hii, ili wayatahayarikie maovu yao; na waipime hesabu yake. 
11 Na ikiwa wameyatahayarikia yote waliyoyatenda, waonyeshe umbo la nyumba, na namna yake, na matokeo yake, na maingilio yake, na maumbo yake yote, na maagizo yake yote, na kawaida zake zote, na sheria zake zote, ukayaandike machoni pao; ili walishike umbo lake lote, na maagizo yake, na kuyatenda. 
12 Hii ndiyo sheria ya nyumba; juu ya kilele cha mlima, mpaka wake wote pande zote patakuwa patakatifu sana. Tazama, hii ndiyo sheria ya nyumba. 
13 Na vipimo vya madhabahu kwa dhiraa ni hivi; (dhiraa ni dhiraa na shubiri); tako lake ni dhiraa moja, na upana wake dhiraa moja; na pambizo yake karibu na ncha yake pande zote, shubiri moja; na hili litakuwa tako la madhabahu. 
14 Tena toka chini, juu ya nchi, hata daraja ya chini, dhiraa mbili, na upana wake dhiraa moja; tena toka daraja ndogo hata daraja kubwa, dhiraa nne, na upana wake dhiraa moja. 
15 Na madhabahu ya juu itakuwa dhiraa nne; na toka madhabahu pawashwapo moto na kwenda juu zitakuwa pembe nne. 
16 Na pale pawashwapo moto, urefu wake dhiraa kumi na mbili, na upana wake kumi na mbili, mraba pande zake nne. 
17 Na daraja, urefu wake dhiraa kumi na nne, na upana wake dhiraa kumi na nne, pande zake nne; na pambizo yake nusu dhiraa; na tako lake dhiraa moja, kote kote, na madaraja yake yataelekea upande wa mashariki. 
18 Kisha akaniambia, Mwanadamu, Bwana MUNGU asema hivi; Hizi ndizo sheria za madhabahu katika siku ile watakapoifanya, ili watoe sadaka za kuteketezwa juu yake, na kunyunyiza damu juu yake. 
19 Utawapa makuhani Walawi, walio wa uzao wa Sadoki, walio karibu nami, ili kunihudumu, asema Bwana MUNGU, ng'ombe mume mchanga awe sadaka ya dhambi. 
20 Nawe utatwaa baadhi ya damu yake, na kuitia juu ya pembe zake nne, na juu ya ncha nne za daraja, na juu ya pambizo yake pande zote; ndivyo utakavyoitakasa, na kuifanyia upatanisho. 
21 Tena utamtwaa ng'ombe wa sadaka ya dhambi, naye utamteketeza mahali palipoamriwa pa nyumba ile, nje ya mahali patakatifu. 
22 Na siku ya pili utamtoa beberu mkamilifu awe sadaka ya dhambi; nao wataisafisha madhabahu, kama walivyoisafisha kwa ng'ombe huyo. 
23 Utakapokwisha kuitakasa, utatoa ng'ombe mume mchanga mkamilifu, na kondoo mume wa kundini mkamilifu. 
24 Nawe utawaleta karibu mbele za Bwana, na makuhani watamwaga chumvi juu yao, nao watawatoa wawe sadaka za kuteketezwa kwa Bwana. 
25 Kwa muda wa siku saba utaweka tayari mbuzi kila siku awe sadaka ya dhambi; pia wataweka tayari ng'ombe mume mchanga, na kondoo mume wa kundini, wakamilifu. 
26 Kwa muda wa siku saba wataifanyia madhabahu upatanisho, na kuitakasa; ndivyo watakavyoiweka wakfu. 
27 Nao watakapozitimiza siku hizo, itakuwa, siku ya nane na baadaye, makuhani watatoa sadaka zenu za kuteketezwa juu ya madhabahu, na sadaka zenu za amani nami nitawakubali ninyi, asema Bwana MUNGU.

TUMA KWA RAFIKI :

Twitter FacebookMore

 
Kuhusu Huduma Hii | Masharti Ya Utumiaji Wa Tovuti Hii | Wasiliana Nasi | Tangaza Kupitia Tovuti Hii