HESABU - SURA YA 25

1 Basi Israeli akakaa Shitimu, kisha watu wakaanza kuzini pamoja na wanawake wa Moabu; 
2 kwa kuwa waliwaalika hao watu waende sadakani, sadaka walizowachinjia miungu yao; watu wakala chakula, wakaisujudu hiyo miungu yao. 
3 Ikawa Israeli kujiungamanisha na Baal-peori; hasira za Bwana zikawaka juu ya Israeli. 
4 Kisha Bwana akamwambia Musa, Watwae wakuu wote wa hao watu, ukamtungikie Bwana watu hao mbele ya jua, ili kwamba hizo hasira kali za Bwana ziwaondokee Israeli. 
5 Basi Musa akawaambia waamuzi wa Israeli, Waueni kila mtu watu wake waliojiungamanisha na Baal-peori. 
6 Na tazama, mtu mmoja miongoni mwa wana wa Israeli akaja na kuwaletea nduguze mwanamke Mmidiani mbele ya macho ya Musa, na mbele ya macho ya mkutano wote wa wana wa Israeli, hapo walipokuwa walia mbele ya mlango wa hema ya kukutania. 
7 Naye Finehasi mwana wa Eleazari, mwana wa Haruni kuhani, alipoona jambo hilo, akaondoka hapo katikati ya mkutano, akashika fumo mkononi mwake; 
8 akamwandama huyo mtu wa Israeli na kuingia ndani ya hema nyuma yake, naye akawachoma wote wawili kwa fumo lake, yule mume wa Israeli na huyo mwanamke kati ya tumbo lake. Basi pigo likazuiwa kwao wana wa Israeli. 
9 Nao waliokufa kwa hilo pigo walikuwa watu elfu ishirini na nne hesabu yao. 
10 Kisha Bwana akanena na Musa, akamwambia, 
11 Finehasi, mwana wa Eleazari, mwana wa Haruni kuhani, amezigeuza hasira zangu zisiwe juu ya wana Wa Israeli, kwa kuwa alikuwa na wivu kati yao kwa wivu wangu mimi, hata nisiwaangamize wana wa Israeli katika wivu wangu. 
12 Basi kwa hiyo, sema, Tazama, nampa yeye agano langu la amani; 
13 tena kwake yeye, na kizazi chake baada yake, litakuwa agano la ukuhani wa milele; kwa sababu alikuwa na wivu kwa ajili ya Mungu wake, na kuwafanyia upatanisho wana wa Israeli. 
14 Basi jina la Mwisraeli huyo aliyeuawa pamoja na yule mwanamke Mmidiani, aliitwa Zimri, mwana wa Salu, mkuu wa nyumba ya baba zake, katika kabila la Simeoni. 
15 Na jina la huyo mwanamke Mmidiani aliyeuawa, aliitwa Kozbi, binti Suri; naye alikuwa kichwa cha watu wa nyumba ya baba zake huko Midiani 
16 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia, 
17 Wasumbue Wamidiani, na kuwapiga; 
18 kwa sababu wao wawasumbua ninyi kwa hila zao, ambazo kwa hizo wamewadanganya ninyi katika jambo la Peori, na katika jambo la huyo Kozbi, binti wa mkuu wa Midiani, umbu lao, huyo aliyeuawa siku hiyo ya pigo katika jambo la Peori.



TUMA KWA RAFIKI :

Twitter FacebookMore

 
Kuhusu Huduma Hii | Masharti Ya Utumiaji Wa Tovuti Hii | Wasiliana Nasi | Tangaza Kupitia Tovuti Hii