HESABU - SURA YA 6

1 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia, 
2 Nena na watu wa Israeli, uwaambie, Mtu mume au mtu mke atakapoweka nadhiri kubwa, nadhiri ya Mnadhiri, ili ajiweke wakfu kwa Bwana; 
3 atajitenga na divai na vileo; hatakunywa siki ya divai, wala siki ya kileo, wala asinywe maji yo yote ya zabibu, wala asile zabibu, mbichi wala zilizokauka. 
4 Siku zote za kujitenga kwake asile kitu cho chote kilichoandaliwa kwa mzabibu, tangu kokwa hata maganda. 
5 Siku zote za nadhiri yake ya kujitenga, wembe usimfikilie kichwani mwake; hata hizo siku zitakapotimia, ambazo alijiweka wakfu kwa Bwana, atakuwa mtakatifu, ataziacha nywele za kichwani mwake zikue ziwe ndefu. 
6 Siku hizo zote ambazo alijiweka awe wa Bwana asikaribie maiti. 
7 Hatajitia unajisi kwa ajili ya baba yake, wala kwa ajili ya mamaye, wala kwa nduguye mume, wala kwa umbu lake, wakifa wao; kwa sababu ya huku kujiweka kwa Mungu ni juu ya kichwa chake. 
8 Siku zote za kujitenga kwake, yeye ni mtakatifu kwa Bwana 
9 Na kama mtu ye yote akifa ghafla karibu naye, akajitia unajisi kichwa cha kutengwa kwake, ndipo atakinyoa kichwa siku hiyo ya kutakaswa kwake, atakinyoa siku ya saba. 
10 Tena siku ya nane ataleta hua wawili, au makinda mawili ya njiwa, aende nao kwa kuhani, hata mlangoni pa hema ya kukutania; 
11 naye kuhani atasongeza mmoja kuwa sadaka ya dhambi, na wa pili kuwa sadaka ya kuteketezwa, naye atafanya upatanisho kwa ajili yake, kwa sababu aliingia kosani kwa ajili ya mfu, naye atatakasa kichwa chake siku iyo hiyo. 
12 Kisha ataziweka kwa Bwana hizo siku za kujitenga kwake, naye ataleta mwana-kondoo mume wa mwaka wa kwanza, kuwa sadaka ya hatia; lakini hizo siku za kwanza hazitahesabiwa, kwa kuwa kule kujitenga kwake kulitiwa unajisi. 
13 Na sheria ya Mnadhiri ni hii, zitakapotimia hizo siku za kujitenga kwake; ataletwa mlangoni pa hema ya kukutania; 
14 naye atasongeza sadaka yake kwa Bwana, mwana-kondoo mmoja mume wa mwaka wa kwanza mkamilifu, kuwa sadaka ya kuteketezwa, na mwana-kondoo mmoja mke wa mwaka wa kwanza mkamilifu, kuwa sadaka ya dhambi, na kondoo mume mmoja mkamilifu kwa sadaka ya amani, 
15 na kikapu cha mikate isiyotiwa chachu, mikate ya unga mwembamba iliyokandwa kwa mafuta, na mikate ya kaki isiyochachwa, iliyotiwa mafuta, pamoja na sadaka zake za unga, na sadaka zake za kinywaji. 
16 Na kuhani atavisongeza mbele za Bwana, naye atasongeza sadaka yake ya dhambi, na sadaka yake ya kuteketezwa; 
17 naye atamsongeza huyo kondoo mume kuwa dhabihu ya sadaka za amani kwa Bwana, pamoja na kikapu cha mikate isiyotiwa chachu; kisha kuhani atasongeza sadaka ya unga nayo, na sadaka yake ya kinywaji. 
18 Naye Mnadhiri atakinyoa kichwa cha kujitenga kwake, mlangoni pa hema ya kukutania, kisha atatwaa hizo nywele za kichwa cha kujitenga kwake, na kuzitia katika moto ulio chini ya dhabihu ya sadaka za amani. 
19 Kisha kuhani atautwaa mkono wa huyo kondoo mume uliotokoswa, na mkate mmoja usio chachu atautwaa kikapuni, na mkate mmoja wa kaki, naye ataitia mikononi mwa yule Mnadhiri, baada ya kunyoa kichwa cha kujitenga kwake; 
20 naye kuhani atavitikisa viwe sadaka ya kutikiswa mbele za Bwana; kitu hicho ni kitakatifu kwa kuhani, pamoja na kidari cha kutikiswa, na paja la kuinuliwa; kisha baadaye Mnadhiri ana ruhusa kunywa divai. 
21 Sheria ya Mnadhiri awekaye nadhiri ni hiyo, tena ni sheria ya sadaka yake atakayomtolea Bwana kwa ajili ya kujitenga kwake, pamoja na vitu vile ambavyo aweza kuvipata zaidi; kama nadhiri yake awekayo ilivyo, ndivyo impasavyo kufanya kwa kuiandama sheria ya kujitenga kwake. 
22 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia, 
23 Nena na Haruni na wanawe, uwaambie, Hivi ndivyo mtakavyowabarikia wana wa Israeli; mtawaambia; 
24 Bwana akubarikie, na kukulinda; 
25 Bwana akuangazie nuru za uso wake, na kukufadhili; 
26 Bwana akuinulie uso wake, na kukupa amani. 
27 Ndivyo watakavyoweka jina langu juu ya wana wa Israeli; nami nitawabarikia.



TUMA KWA RAFIKI :

Twitter FacebookMore

 
Kuhusu Huduma Hii | Masharti Ya Utumiaji Wa Tovuti Hii | Wasiliana Nasi | Tangaza Kupitia Tovuti Hii