1 Ikawa
alipokuwa mahali fulani akiomba, alipokwisha, mmoja katika wanafunzi wake
alimwambia, Bwana, tufundishe sisi kusali, kama vile Yohana alivyowafundisha
wanafunzi wake.
2 Akawaambia,
Msalipo, semeni, Baba [yetu uliye mbinguni], Jina lako litakaswe, Ufalme wako
uje, [Mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni.]
3 Utupe
siku kwa siku riziki yetu.
4 Utusamehe
dhambi zetu, kwa kuwa sisi nasi tunamsamehe kila tumwiaye. Na usitutie
majaribuni [lakini tuokoe na yule mwovu].
5 Akawaambia,
Ni nani kwenu aliye na rafiki, akamwendea usiku wa manane, na kumwambia, Rafiki
yangu, nikopeshe mikate mitatu,
6 kwa
sababu rafiki yangu amefika kwangu, atoka safarini, nami sina kitu cha kuweka
mbele yake;
7 na
yule wa ndani amjibu akisema, Usinitaabishe; mlango umekwisha fungwa, nasi
tumelala kitandani mimi na watoto wangu; siwezi kuondoka nikupe?
8 Nawaambia
ya kwamba, ijapokuwa haondoki ampe kwa kuwa ni rafiki yake, lakini kwa vile
asivyoacha kumwomba, ataondoka na kumpa kadiri ya haja yake.
9 Nami
nawaambia, Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi
mtafunguliwa.
10 Kwa
kuwa kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa.
11 Maana
ni yupi kwenu aliye baba, ambaye mwanawe akimwomba mkate, atampa jiwe au
samaki, badala ya samaki atampa nyoka?
12 Au
akimwomba yai, atampa nge?
13 Basi,
ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Baba aliye
mbinguni hatazidi sana kuwapa Roho Mtakatifu hao wamwombao?
14 Naye
alikuwa akitoa pepo bubu; ikawa pepo alipotoka, yule bubu akanena, makutano
wakastaajabu.
15 Wengine
wao wakasema, Atoa pepo kwa Beelzebuli, mkuu wa pepo.
16 Wengine
walimjaribu, wakimtaka ishara itokayo mbinguni.
17 Naye
akajua mawazo yao, akawaambia, Kila ufalme uliofitinika wenyewe kwa wenyewe
hufanyika ukiwa; na nyumba juu ya nyumba huanguka.
18 Basi,
ikiwa Shetani naye amefitinika juu ya nafsi yake, ufalme wake utasimamaje? Kwa
kuwa ninyi mnasema kwamba mimi natoa pepo kwa Beelzebuli.
19 Basi,
kama mimi nikitoa pepo kwa Beelzebuli, wana wenu je! Huwatoa kwa nani? Kwa
sababu hiyo, hao ndio watakaowahukumu.
20 Lakini,
ikiwa mimi natoa pepo kwa kidole cha Mungu, basi ufalme wa Mungu umekwisha
kuwajilia.
21 Mtu
mwenye nguvu aliyejifunga silaha zake, alindapo nyumba yake, vitu vyake vi
salama;
22 lakini
mtu mwenye nguvu kuliko yeye atakapomwendea na kumshinda, amnyang'anya silaha
zake zote alizokuwa akizitegemea, na kuyagawanya mateka yake.
23 Mtu
ambaye si pamoja nami yu kinyume changu; na mtu asiyekusanya pamoja nami
hutawanya.
24 Pepo
mchafu amtokapo mtu, hupitia mahali pasipo maji, akitafuta mahali pa kupumzika;
asipoona, husema,
25 Nitairudia
nyumba yangu niliyotoka.
26 Hata
afikapo, akaiona imefagiwa na kupambwa, ndipo huenda akachukua pepo wengine
saba, walio waovu kuliko yeye mwenyewe, wakaingia na kukaa humo; na mtu yule
hali yake ya mwisho huwa mbaya kuliko ya kwanza.
27 Ikawa
alipokuwa akisema maneno hayo, mwanamke mmoja katika mkutano alipaza sauti
yake, akamwambia, Heri tumbo lililokuzaa, na matiti uliyonyonya.
28 Lakini
yeye alisema, Afadhali, heri walisikiao neno la Mungu na kulishika.
29 Na
makutano walipokuwa wakimkusanyikia, alianza kusema, Kizazi hiki ni kizazi
kibaya; kinatafuta ishara, wala hakitapewa ishara, ila ishara ya Yona.
30 Maana,
kama vile Yona alivyokuwa ishara kwa Waninawi, ndivyo atakavyokuwa Mwana wa
Adamu kwa kizazi hiki.
31 Malkia
wa Kusini ataondoka siku ya hukumu pamoja na watu wa kizazi hiki, naye
atawahukumu kuwa na hatia; kwa sababu yeye alikuja kutoka ncha za dunia aisikie
hekima ya Sulemani; na hapa pana mkubwa kuliko Sulemani.
32 Watu
wa Ninawi watasimama siku ya hukumu pamoja na kizazi hiki, nao watakihukumu
kuwa na hatia; kwa sababu wao walitubu kwa mahubiri ya Yona, na hapa pana
mkubwa kuliko Yona.
33 Hakuna
mtu awashaye taa na kuiweka mahali palipositirika, au chini ya pishi; bali
huiweka juu ya kiango, ili waingiao wapate kuuona mwanga.
34 Taa
ya mwili ni jicho; basi jicho lako likiwa safi, mwili wako wote unao mwanga;
lakini likiwa bovu, mwili wako nao una giza.
35 Angalia
basi, mwanga ulio ndani yako usije ukawa giza.
36 Basi
kama mwanga umeenea katika mwili wako wote, wala hauna sehemu iliyo na giza,
mwili wako wote utakuwa na mwanga mtupu; kama vile taa ikumulikiapo kwa mwanga
wake.
37 Alipokuwa
akinena, Farisayo mmoja alimwita aje kwake ale chakula; akaingia, akaketi
chakulani.
38 Farisayo
huyo alipomwona, alistaajabu kwa sababu hakunawa kabla ya chakula.
39 Bwana
akamwambia, Ninyi Mafarisayo mwasafisha kikombe na sahani kwa nje, lakini ndani
yenu mmejaa unyang'anyi na uovu.
40 Enyi
wapumbavu; aliyevifanya vya nje, siye yeye aliyevifanya vya ndani pia?
41 Lakini,
toeni sadaka vile vya ndani, na tazama, vyote huwa safi kwenu.
42 Lakini,
ole wenu, Mafarisayo, kwa kuwa mwatoa zaka za mnanaa na mchicha na kila mboga,
na huku mwaacha mambo ya adili, na upendo wa Mungu; iliwapasa kuyafanya hayo ya
kwanza, bila kuyaacha hayo ya pili.
43 Ole
wenu, Mafarisayo, kwa kuwa mwapenda kuketi mbele katika masinagogi, na
kusalimiwa masokoni.
44 Ole
wenu, kwa kuwa mmefanana na makaburi yasiyoonekana, ambayo watu wapitao juu
yake hawana habari nayo.
45 Mtu
mmoja katika wana-sheria akajibu, akamwambia, Mwalimu, kwa kusema hayo
umetushutumu sisi nasi.
46 Akasema,
Nanyi wana-sheria, ole wenu, kwa sababu mwawatwika watu mizigo isiyochukulika,
wala ninyi wenyewe hamwigusi mizigo hiyo hata kwa kimoja cha vidole vyenu.
47 Ole
wenu, kwa kuwa mwajenga maziara ya manabii, na baba zenu ndio waliowaua.
48 Basi,
mwashuhudia na kuziridhia kazi za baba zenu; kwa kuwa wao waliwaua nanyi
mwawajengea maziara.
49 Na
kwa sababu hiyo hekima ya Mungu ilisema, Tazama, nitatuma kwao manabii na
mitume, nao watawaua baadhi yao na kuwafukuza,
50 ili
kwa kizazi hiki itakwe damu ya manabii wote, iliyomwagika tangu kupigwa msingi
wa ulimwengu;
51 tangu
damu ya Habili hata damu ya Zakaria, aliyeuawa kati ya madhabahu na hekalu.
Naam, nawaambieni ya kwamba itatakwa kwa kizazi hiki.
52 Ole
wenu, enyi wana-sheria, kwa kuwa mmeuondoa ufunguo wa maarifa; wenyewe
hamkuingia, na wale waliokuwa wakiingia mmewazuia.
53 Alipotoka
humo, waandishi na Mafarisayo walianza kumsonga vibaya, na kumchokoza kwa
maswali mengi,
54 wakimvizia,
ili wapate neno litokalo kinywani mwake.