1 Ikawa
makutano walipomsonga wakilisikiliza neno la Mungu, yeye alikuwa amesimama
kando ya ziwa la Genesareti,
2 akaona
vyombo viwili vimekaa kando ya ziwa, lakini wavuvi wametoka, wanaosha nyavu
zao.
3 Akaingia
katika chombo kimoja, ndicho chake Simoni, akamtaka akipeleke mbali kidogo na
pwani. Akaketi, akawafundisha makutano ali chomboni.
4 Hata
alipokwisha kunena, alimwambia Simoni, Tweka mpaka kilindini, mkashushe nyavu
zenu mvue samaki.
5 Simoni
akajibu akamwambia, Bwana mkubwa, tumefanya kazi ya kuchosha usiku kucha,
tusipate kitu; lakini kwa neno lako nitazishusha nyavu.
6 Basi,
walipofanya hivyo walipata samaki wengi mno, nyavu zao zikaanza kukatika;
7 wakawapungia
mikono washirika wao waliokuwa katika chombo cha pili, waje kuwasaidia; wakaja,
wakavijaza vyombo vyote viwili, hata vikataka kuzama.
8 Simoni
Petro alipoona hayo, alianguka magotini pa Yesu, akisema, Ondoka kwangu, kwa
kuwa mimi ni mtu mwenye dhambi, Bwana.
9 Maana
alishikwa na ushangao, yeye na wote waliokuwa pamoja naye, kwa sababu ya wingi
wa samaki walioupata;
10 na
kadhalika Yakobo na Yohana, wana wa Zebedayo, waliokuwa washirika wa Simoni.
Yesu akamwambia Simoni, Usiogope, tangu sasa utakuwa ukivua watu.
11 Hata
walipokwisha kuviegesha pwani vyombo vyao, wakaacha vyote wakamfuata.
12 Ikawa,
alipokuwa katika mmojawapo wa miji ile, tazama, palikuwa na mtu amejaa ukoma;
naye alipomwona Yesu alianguka kifudifudi, akamwomba akisema, Bwana, ukitaka,
waweza kunitakasa.
13 Naye
akaunyosha mkono wake, akamgusa akisema, Nataka; takasika. Na mara ukoma wake
ukamwondoka.
14 Akamkataza
asimwambie mtu, ila, Nenda ukajionyeshe kwa kuhani; ukatoe kwa ajili ya
kutakasika kwako kama Musa alivyoamuru, iwe ushuhuda kwao.
15 Lakini
habari zake zikazidi kuenea, wakakutanika makutano mengi wamsikilize na
kuponywa magonjwa yao.
16 Lakini
yeye alikuwa akijiepua, akaenda mahali pasipokuwa na watu, akaomba.
17 Ikawa
siku zile mojawapo alikuwa akifundisha, na Mafarisayo na waalimu wa torati
walikuwa wameketi hapo, waliotoka katika kila kijiji cha Galilaya, na Uyahudi,
na Yerusalemu; na uweza wa Bwana ulikuwapo apate kuponya.
18 Na
tazama, wakaja watu wanamchukua kitandani mtu mwenye kupooza; wakataka
kumpeleka ndani na kumweka mbele yake.
19 Hata
walipokosa nafasi ya kumpeleka ndani kwa ajili ya lile kundi la watu, walipanda
juu ya dari wakampisha katika matofali ya juu, wakamshusha yeye na kitanda
chake katikati mbele ya Yesu.
20 Naye
alipoiona imani yao, alimwambia, Ee rafiki, umesamehewa dhambi zako.
21 Basi,
wale waandishi na Mafarisayo wakaanza kuhojiana wakisema, Ni nani huyu asemaye
maneno ya kukufuru? N'nani awezaye kusamehe dhambi isipokuwa Mungu peke yake?
22 Na
Yesu alijua hoja zao, akajibu akawaambia, Mnahojiana nini mioyoni mwenu?
23 Lililo
jepesi ni lipi? Kusema, Umesamehewa dhambi zako, au kusema, Ondoka, uende?
24 Lakini,
mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi,
(alimwambia yule mwenye kupooza). Nakuambia, Ondoka, ujitwike kitanda chako,
ukaende zako nyumbani kwako.
25 Mara
hiyo akasimama mbele yao, akajitwika kile alichokilalia, akaenda zake nyumbani
kwake, huku akimtukuza Mungu.
26 Ushangao
ukawashika wote, wakamtukuza Mungu; wakajaa hofu, wakisema, Leo tumeona mambo
ya ajabu.
27 Baada
ya hayo akatoka, akaona mtoza ushuru, jina lake Lawi, ameketi forodhani,
akamwambia, Nifuate.
28 Akaacha
vyote, akaondoka, akamfuata.
29 Na
Lawi akamfanyia karamu kubwa nyumbani mwake; palikuwa na mkutano mkuu wa watoza
ushuru na watu wengineo waliokuwa wameketi chakulani pamoja nao.
30 Ikawa
Mafarisayo na waandishi wao kuwanung'unikia wanafunzi wake, wakisema, Mbona
mnakula na kunywa pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi?
31 Yesu
akajibu akawaambia, Wenye afya hawana haja na tabibu, isipokuwa walio hawawezi.
32 Sikuja
kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi, wapate kutubu.
33 Nao
wakamwambia, Wanafunzi wa Yohana hufunga mara nyingi, na kuomba dua; na
kadhalika wanafunzi wa Mafarisayo; lakini wanafunzi wako hula na kunywa!
34 Lakini
Yesu akawaambia, Je! Mwaweza kuwafanya wafunge walioalikwa arusini, akiwapo
bwana arusi pamoja nao?
35 Lakini
siku zitakuja watakapoondolewa bwana arusi, ndipo watakapofunga siku zile.
36 Akawaambia
na mithali, Hakuna akataye kiraka cha vazi jipya na kukitia katika vazi kuukuu;
na kama akitia, amelikata lile jipya, na kile kiraka cha vazi jipya hakilingani
na lile vazi kuukuu.
37 Wala
hakuna mtu atiaye divai mpya katika viriba vikuukuu; na kama akitia, ile divai
mpya itavipasua vile viriba, divai yenyewe itamwagika, na viriba vitaharibika.
38 Lakini
divai mpya sharti kutiwa katika viriba vipya.
39 Wala
hakuna anywaye divai ya kale akatamani divai mpya; kwa kuwa asema, Ile ya kale
ndiyo iliyo njema.