1 Hata
sabato ilipokwisha kupita, Mariamu Magdalene na Mariamu mamaye Yakobo, na
Salome walinunua manukato wapate kwenda kumpaka.
2 Hata
alfajiri mapema, siku ya kwanza ya juma, wakaenda kaburini, jua lilipoanza
kuchomoza;
3 wakasemezana
wao kwa wao, Ni nani atakayetuvingirishia lile jiwe mlangoni pa kaburi?
4 Hata
walipotazama, waliona ya kuwa lile jiwe limekwisha kuvingirishwa; nalo lilikuwa
kubwa mno.
5 Wakaingia
kaburini wakaona kijana ameketi upande wa kuume, amevaa vazi jeupe; wakastaajabu.
6 Naye
akawaambia, Msistaajabu; mnamtafuta Yesu Mnazareti, aliyesulibiwa; amefufuka;
hayupo hapa; patazameni mahali walipomweka.
7 Lakini
enendeni zenu, mkawaambie wanafunzi wake, na Petro, ya kwamba awatangulia
kwenda Galilaya; huko mtamwona, kama alivyowaambia.
8 Wakatoka
nje, wakakimbia kutoka kaburini; kwa maana wameingia tetemeko na ushangao; wala
hawakumwambia mtu neno, maana waliogopa. [
9 Naye
alipofufuka alfajiri siku ya kwanza ya juma, alimtokea kwanza Mariamu
Magdalene, ambaye kwamba alimtoa pepo saba.
10 Huyo
akashika njia akawapasha habari wale waliokuwa pamoja naye, nao wakali
wanaomboleza na kulia.
11 Walakini
hao waliposikia kama yu hai, naye amemwona, hawakusadiki.
12 Baada
ya hayo akawatokea watu wawili miongoni mwao, ana sura nyingine; nao walikuwa
wakishika njia kwenda shamba.
13 Na
hao wakaenda zao wakawapa habari wale wengine; wala hao hawakuwasadiki.
14 Baadaye
akaonekana na wale kumi na mmoja walipokuwa wakila, akawakemea kwa kutokuamini
kwao na ugumu wa mioyo yao, kwa kuwa hawakuwasadiki wale waliomwona alipofufuka
katika wafu.
15 Akawaambia,
Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe.
16 Aaminiye
na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa.
17 Na
ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema
kwa lugha mpya;
18 watashika
nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono
yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya.
19 Basi
Bwana Yesu, baada ya kusema nao, akachukuliwa juu mbinguni, akaketi mkono wa
kuume wa Mungu.
20 Nao
wale wakatoka, wakahubiri kotekote, Bwana akitenda kazi pamoja nao, na
kulithibitisha lile neno kwa ishara zilizofuatana nalo.]