1 Hata
ilipotimia siku ya Pentekoste walikuwako wote mahali pamoja.
2 Kukaja
ghafula toka mbinguni uvumi kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza
nyumba yote waliyokuwa wameketi.
3 Kukawatokea
ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao.
4 Wote
wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho
alivyowajalia kutamka.
5 Na
walikuwako Yerusalemu Wayahudi wakikaa, watu watauwa, watu wa kila taifa chini
ya mbingu.
6 Basi
sauti hii iliposikiwa makutano walikutanika, wakashikwa na fadhaa, kwa kuwa
kila mmoja aliwasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe.
7 Wakashangaa
wote, wakastaajabu wakiambiana, Tazama, hawa wote wasemao si Wagalilaya?
8 Imekuwaje
basi sisi kusikia kila mtu lugha yetu tuliyozaliwa nayo?
9 Warparthi
na Wamedi na Waelami, nao wakaao Mesopotamia, Uyahudi na Kapadokia, Ponto na
Asia,
10 Frigia
na Pamfilia, Misri na pande za Libia karibu na Kirene, na wageni watokao Rumi,
Wayahudi na waongofu,
11 Wakrete
na Waarabu; tunawasikia hawa wakisema kwa lugha zetu matendo makuu ya Mungu.
12 Wakashangaa
wote wakaingiwa na shaka, wakiambiana, Maana yake nini mambo haya?
13 Wengine
walidhihaki, wakisema, wamelewa kwa mvinyo mpya.
14 Lakini
Petro akasimama pamoja na wale kumi na mmoja, akapaza sauti yake, akawaambia,
Enyi watu wa Uyahudi, na ninyi nyote mkaao Yerusalemu, lijueni jambo hili,
mkasikilize maneno yangu.
15 Sivyo
mnavyodhani; watu hawa hawakulewa, kwa maana ni saa tatu ya mchana;
16 lakini
jambo hili ni lile lililonenwa kwa kinywa cha nabii Yoeli,
17 Itakuwa
siku za mwisho, asema Mungu, nitawamwagia watu wote Roho yangu, na wana wenu na
binti zenu watatabiri; na vijana wenu wataona maono; na wazee wenu wataota
ndoto.
18 Naam,
na siku zile nitawamwagia watumishi wangu wanaume na wanawake Roho yangu, nao watatabiri.
19 Nami
nitatoa ajabu katika mbingu juu, na ishara katika nchi chini, damu na moto, na
mvuke wa moshi.
20 Jua
litageuka kuwa giza, na mwezi kuwa damu, kabla ya kuja ile siku ya Bwana iliyo
kuu na iliyo dhahiri.
21 Na
itakuwa kila atakayeliitia jina la Bwana ataokolewa.
22 Enyi
waume wa Israeli, sikilizeni maneno haya: Yesu wa Nazareti, mtu
aliyedhihirishwa kwenu na Mungu kwa miujiza na ajabu na ishara, ambazo Mungu
alizifanya kwa mkono wake kati yenu, kama ninyi wenyewe mnavyojua;
23 mtu
huyu alipotolewa kwa shauri la Mungu lililokusudiwa, na kwa kujua kwake tangu
zamani, ninyi mkamsulibisha kwa mikono ya watu wabaya, mkamwua;
24 ambaye
Mungu alimfufua, akiufungua uchungu wa mauti, kwa sababu haikuwezekana ashikwe
nao.
25 Maana
Daudi ataja habari zake, Nalimwona Bwana mbele yangu siku zote, Kwa kuwa yuko
upande wa mkono wangu wa kuume, nisitikisike.
26 Kwa
hiyo moyo wangu ukapendezewa, ulimi wangu ukafurahi; Tena mwili wangu nao
utakaa katika matumaini.
27 Kwa
maana hutaiacha roho yangu katika kuzimu; Wala hutamtoa Mtakatifu wako aone
uharibifu.
28 Umenijuvisha
njia za uzima; Utanijaza furaha kwa uso wako.
29 Waume,
ndugu zangu, mniwie radhi, niseme kwa ujasiri mbele yenu habari za baba yetu
mkuu, Daudi, ya kuwa alifariki akazikwa, na kaburi lake liko kwetu hata leo.
30 Basi
kwa kuwa ni nabii, akijua ya kuwa Mungu amemwapia kwa kiapo, ya kwamba katika
uzao wa viuno vyake atamketisha mmoja katika kiti chake cha enzi;
31 yeye
mwenyewe akitangulia kuyaona haya, alitaja habari za kufufuka kwake Kristo, ya
kwamba roho yake haikuachwa kuzimu, wala mwili wake haukuona uharibifu.
32 Yesu
huyo Mungu alimfufua, na sisi sote tu mashahidi wake.
33 Basi
yeye, akiisha kupandishwa hata mkono wa kuume wa Mungu, na kupokea kwa Baba ile
ahadi ya Roho Mtakatifu, amekimwaga kitu hiki mnachokiona sasa na kukisikia.
34 Maana
Daudi hakupanda mbinguni; bali yeye mwenyewe anasema, Bwana alimwambia Bwana
wangu, Keti upande wa mkono wangu wa kuume.
35 Hata
nitakapowaweka adui zako chini ya miguu yako.
36 Basi
nyumba yote ya Israeli na wajue yakini ya kwamba Mungu amemfanya Yesu huyo
mliyemsulibisha kuwa Bwana na Kristo.
37 Walipoyasikia
haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje,
ndugu zetu?
38 Petro
akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate
ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.
39 Kwa
kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio
mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie.
40 Akawashuhudia
kwa maneno mengine mengi sana na kuwaonya, akisema, Jiokoeni na kizazi hiki
chenye ukaidi.
41 Nao
waliolipokea neno lake wakabatizwa; na siku ile wakaongezeka watu wapata elfu
tatu.
42 Wakawa
wakidumu katika fundisho la mitume, na katika ushirika, na katika kuumega
mkate, na katika kusali.
43 Kila
mtu akaingiwa na hofu; ajabu nyingi na ishara zikafanywa na mitume.
44 Na
wote walioamini walikuwa mahali pamoja, na kuwa na vitu vyote shirika,
45 wakiuza
mali zao, na vitu vyao walivyokuwa navyo, na kuwagawia watu wote kama kila mtu
alivyokuwa na haja.
46 Na
siku zote kwa moyo mmoja walidumu ndani ya hekalu, wakimega mkate nyumba kwa
nyumba, na kushiriki chakula chao kwa furaha na kwa moyo mweupe,
47 wakimsifu
Mungu, na kuwapendeza watu wote. Bwana akalizidisha kanisa kila siku kwa wale
waliokuwa wakiokolewa.