1 Hata
Festo alipokwisha kuingia katika uliwali, baada ya siku tatu akapanda kwenda
Yerusalemu kutoka Kaisaria.
2 Kuhani
Mkuu na wakuu wa Wayahudi wakampasha habari za Paulo, wakamsihi,
3 na
kumwomba fadhili juu yake, kwamba atoe amri aletwe Yerusalemu, wapate kumwotea
na kumwua njiani.
4 Lakini
Festo akajibu ya kwamba Paulo analindwa Kaisaria; naye mwenyewe yu tayari
kwenda huko karibu.
5 Akasema,
Wale walio na mamlaka kwenu na watelemke pamoja nami wakamshitaki, ikiwa liko
neno baya katika mtu huyu.
6 Alipokwisha
kukaa kwao siku nane au kumi si zaidi, akatelemkia Kaisaria; hata siku ya pili
akaketi katika kiti cha hukumu akaamuru Paulo aletwe.
7 Alipokuja,
wale Wayahudi walioshuka kutoka Yerusalemu wakasimama karibu yake wakaleta
mashitaka mengi mazito juu yake, wasiyoweza kuyayakinisha.
8 Paulo
akasema akijitetea, Mimi sikukosa neno juu ya sheria ya Wayahudi, wala juu ya
hekalu, wala juu ya Kaisari.
9 Lakini
Festo akitaka kujipendekeza kwa Wayahudi akamjibu Paulo, akisema, Je! Wataka
kwenda Yerusalemu, ukahukumiwe huko mbele yangu kwa ajili ya mambo hayo?
10 Paulo
akasema, Mimi ninasimama hapa mbele ya kiti cha hukumu cha Kaisari, ndipo
panipasapo kuhukumiwa; sikuwakosa Wayahudi neno, kama wewe ujuavyo sana.
11 Basi
ikiwa ni mkosa au nimetenda neno la kustahili kufa, sikatai kufa; bali, kama si
kweli neno hili wanalonishitaki, hapana awezaye kunitia mikononi mwao. Nataka
rufani kwa Kaisari.
12 Basi
Festo alipokwisha kusema na watu wa baraza, akajibu, Umetaka rufani kwa
Kaisari! Basi, utakwenda kwa Kaisari.
13 Siku
kadha wa kadha zilipokwisha kupita, Agripa mfalme na Bernike wakafika Kaisaria,
wakimwamkia Festo.
14 Na
walipokuwa wakikaa huko siku nyingi, Festo akamweleza mfalme habari za Paulo,
akisema, Yupo hapa mtu mmoja aliyeachwa na Feliki kifungoni;
15 ambaye
nilipokuwa Yerusalemu wakuu wa makuhani na wazee wa Wayahudi wakaniarifu habari
zake, wakinitaka hukumu juu yake.
16 Nikawajibu
kwamba si desturi ya Warumi kumtoa mtu awaye yote, kabla mtu yule
aliyeshitakiwa hajaonana na washitaki wake uso kwa uso, na kupewa nafasi ya
kujitetea katika mashitaka yake.
17 Basi
walipokutanika hapa sikukawia; bali siku ya pili nikaketi katika kiti cha
hukumu nikaamuru mtu huyo aletwe.
18 Na
wale waliomshitaki waliposimama hawakuleta neno lo lote baya, kama
nilivyodhani,
19 bali
walikuwa na maswali mengine mengine juu yake katika dini yao wenyewe, na katika
habari ya mtu mmoja Yesu, aliyekuwa amekwisha kufa, ambaye Paulo alikaza kusema
kwamba yu hai.
20 Nami
nikaona shaka jinsi ya kutafuta hakika ya habari hii, nikamwuliza kama anataka
kwenda Yerusalemu ahukumiwe huko katika mambo haya.
21 Lakini
Paulo alipodai kuwekwa ahukumiwe na Kaisari, nikaamuru alindwe hata
nitakapompeleka kwa Kaisari.
22 Agripa
akamwambia Festo, Mimi nami nalikuwa nikitaka kumsikia mtu huyu. Akasema, Utamsikia
kesho.
23 Hata
asubuhi Agripa akaja pamoja na Bernike kwa fahari nyingi, wakaingia mahali pa
kusikia maneno, pamoja na maakida wakuu na watu wakuu wa mji; Festo akatoa
amri, Paulo akaletwa.
24 Festo
akasema, Mfalme Agripa, na ninyi nyote mliopo hapa pamoja nasi, mnamwona mtu
huyu, ambaye jamii yote ya Wayahudi huko Yerusalemu na hapa pia wamenitaka
niwasaidie, wakipiga kelele kwamba haimpasi kuishi zaidi.
25 Lakini
mimi naliona kwamba hakutenda neno la kustahili kuuawa, na yeye mwenyewe
alipotaka kuhukumiwa na Kaisari, nalikusudia kumpeleka kwake.
26 Nami
katika habari yake sina neno la hakika la kumwandikia bwana. Kwa hiyo nimemleta
hapa mbele yenu, hasa mbele yako wewe, mfalme Agripa, ili akiisha
kuulizwa-ulizwa nipate neno la kuandika.
27 Kwa
maana naona ni neno lisilo maana kumpeleka mfungwa, bila kuonyesha mashitaka
yale aliyoshitakiwa.