1 Tulipokwisha
kuokoka, ndipo tulipojua ya kuwa kisiwa kile chaitwa Melita.
2 Wenyeji
wakatufanyia fadhili zisizokuwa za kawaida. Kwa maana waliwasha moto,
wakatukaribisha sote, kwa sababu ya mvua iliyonyesha na kwa sababu ya baridi.
3 Paulo
alipokuwa amekusanya mzigo wa kuni, na kuuweka motoni, nyoka akatoka kwa ajili
ya ule moto akamzonga-zonga mkononi.
4 Wenyeji
walipomwona yule nyoka akilewa-lewa mkononi, wakaambiana, Hakosi mtu huyu ni
mwuaji; ambaye ijapokuwa ameokoka katika bahari haki haimwachi kuishi.
5 Lakini
yeye akamtukusia motoni asipate madhara.
6 Wao
wakadhani ya kuwa atavimba au kuanguka chini kwa kufa ghafula; na wakiisha
kumwangalia sana, na kuona kwamba halimpati dhara lo lote, wakageuka, wakasema
kwamba yeye ni mungu.
7 Karibu
na mahali pale palikuwa na mashamba ya mkuu wa kisiwa, jina lake Publio; mtu
huyu akatukaribisha kwa moyo wa urafiki, akatufanya wageni wake kwa muda wa
siku tatu.
8 Ikawa
babaake Publio alikuwa hawezi homa na kuhara damu. Paulo akaingia kwake,
akaomba, akaweka mikono yake juu yake, na kumpoza.
9 Yalipokwisha
kutendeka hayo wengine waliokuwa na magonjwa katika kisiwa wakaja wakapozwa;
10 nao
wakatuheshimu kwa heshima nyingi; basi tulipoabiri wakatupakilia vitu vile
tulivyokuwa na haja navyo.
11 Baada
ya miezi mitatu tukasafiri katika merikebu ya Iskanderia iliyokuwa imekaa pale
kisiwani wakati wa baridi; na alama yake ni Ndugu Pacha.
12 Tukafika
Sirakusa, tukakaa siku tatu.
13 Kutoka
huko tukazunguka tukafikia Regio; baada ya siku moja upepo wa kusi ukavuma, na
siku ya pili tukawasili Puteoli.
14 Huko
tukakuta ndugu, wakatusihi tukae nao siku saba; na hivi tukafika Rumi.
15 Na
kutoka huko ndugu, waliposikia habari zetu, wakaja kutulaki mpaka Soko la Apio
na Mikahawa Mitatu. Paulo alipowaona alimshukuru Mungu, akachangamka.
16 Tulipoingia
Rumi Paulo alipewa ruhusa kukaa kwake mwenyewe pamoja na askari aliyemlinda.
17 Ikawa
baada ya siku tatu akawaita wakuu wa Wayahudi wakutane, hata walipokutanika
akawaambia, Ndugu zangu, ningawa sikufanya neno kinyume cha watu wetu wala neno
lililopingamana na desturi za baba zetu, nalitiwa katika mikono ya Warumi, hali
nimefungwa, tokea Yerusalemu.
18 Na
hao walipokwisha kuniuliza-uliza walitaka kunifungua, kwa maana hapakuwa na
sababu yo yote kwangu ya kuuawa.
19 Lakini
Wayahudi walipotoa hoja juu ya shauri hili nalishurutishwa kutaka rufani kwa
Kaisari. Si kwamba nalikuwa na neno la kuwashitaki watu wa taifa langu.
20 Basi
kwa ajili ya hayo, nimewaita mje kunitazama na kusema nami; kwa maana
nimefungwa kwa mnyororo huu kwa ajili ya tumaini la Israeli.
21 Wale
wakamwambia, Sisi hatukupata nyaraka zenye habari zako kutoka Uyahudi, wala
hapana ndugu hata mmoja aliyefika hapa na kutupasha habari, au kunena neno baya
juu yako.
22 Lakini
tunataka kusikia kwako uonavyo wewe; kwa maana katika habari za madhehebu hiyo
imejulikana kwetu kwamba inanenwa vibaya kila mahali.
23 Wakiisha
kuagana naye siku, wakamjia katika nyumba aliyokaa, watu wengi sana, akawaeleza
kwa taratibu na kuushuhudia ufalme wa Mungu, akiwaonya mambo yake Yesu, kwa
maneno ya sheria ya Musa na ya manabii, tangu asubuhi hata jioni.
24 Wengine
waliamini yale yaliyonenwa, wengine hawakuyaamini.
25 Na
walipokuwa hawapatani wao kwa wao, wakaenda zao, Paulo alipokwisha kusema neno
hili moja, ya kwamba, Roho Mtakatifu alinena vema na baba zetu, kwa kinywa cha
nabii Isaya,
26 akisema,
Enenda kwa watu hawa, ukawaambie, Kusikia, mtasikia wala hamtafahamu; Na kuona,
mtaona wala hamtatambua;
27 Kwa
maana mioyo ya watu hawa imepumbaa, Na masikio yao ni mazito ya kusikia, Na
macho yao wameyafumba; Wasije wakaona kwa macho yao, Na kusikia kwa masikio
yao, Na kufahamu kwa mioyo yao, Na kubadili nia zao, nikawaponya.
28 Basi
ijulikane kwenu ya kwamba wokovu huu wa Mungu umepelekwa kwa Mataifa, nao
watasikia!
29 Alipokwisha
kusema hayo, Wayahudi wakaenda zao, wakiulizana mengi wao kwa wao.]
30 Akakaa
muda wa miaka miwili mizima katika nyumba yake aliyokuwa ameipanga, akawakaribisha
watu wote waliokuwa wakimwendea,
31 akihubiri
habari za ufalme wa Mungu, na kuyafundisha mambo ya Bwana Yesu Kristo, kwa
ujasiri mwingi, asikatazwe na mtu.