1 Hata
walipokuwa wakisema na watu wale, makuhani na akida wa hekalu na Masadukayo
wakawatokea,
2 wakifadhaika
sana kwa sababu wanawafundisha watu na kuhubiri katika Yesu ufufuo wa wafu.
3 Wakawakamata,
wakawaweka gerezani hata asubuhi; kwa kuwa imekwisha kuwa jioni.
4 Lakini
wengi katika hao waliosikia lile neno waliamini; na hesabu ya watu waume ikawa
kama elfu tano.
5 Hata
asubuhi wakubwa na wazee na waandishi wakakusanyika Yerusalemu,
6 na
Anasi Kuhani Mkuu, na Kayafa pia, na Yohana na Iskanda, na wote wale waliokuwa
jamaa zake Kuhani Mkuu.
7 Walipowaweka
katikati wakawauliza, Kwa nguvu gani na kwa jina la nani ninyi mmefanya haya?
8 Ndipo
Petro, akijaa Roho Mtakatifu, akawaambia, Enyi wakubwa wa watu na wazee wa
Israeli,
9 kama
tukiulizwa leo habari ya jambo jema alilofanyiwa yule mtu dhaifu, jinsi
alivyoponywa,
10 jueni
ninyi nyote na watu wote wa Israeli ya kuwa kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti,
ambaye ninyi mlimsulibisha, na Mungu akamfufua katika wafu, kwa jina hilo mtu
huyu anasimama ali mzima mbele yenu.
11 Yeye
ndiye jiwe lile lililodharauliwa na ninyi waashi, nalo limewekwa kuwa jiwe kuu
la pembeni.
12 Wala
hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini
ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.
13 Basi
walipoona ujasiri wa Petro na Yohana, na kuwajua ya kuwa ni watu wasio na
elimu, wasio na maarifa, wakastaajabu, wakawatambua ya kwamba walikuwa pamoja
na Yesu.
14 Na
wakimwona yule aliyeponywa akisimama pamoja nao hawakuwa na neno la kujibu.
15 Wakawaamuru
kutoka katika baraza, wakafanya shauri wao kwa wao,
16 wakisema,
Tuwafanyie nini watu hawa? Maana ni dhahiri kwa watu wote wakaao Yerusalemu ya
kwamba ishara mashuhuri imefanywa nao, wala hatuwezi kuikana.
17 Lakini
neno hili lisije likaenea katika watu, na tuwatishe wasiseme tena na mtu awaye
yote kwa jina hili.
18 Wakawaita,
wakawaamuru wasiseme kabisa wala kufundisha kwa jina la Yesu.
19 Petro
na Yohana wakawajibu wakawaambia, Kwamba ni haki mbele za Mungu kuwasikiliza
ninyi kuliko Mungu, hukumuni ninyi wenyewe;
20 maana
sisi hatuwezi kuacha kuyanena mambo tuliyoyaona na kuyasikia.
21 Nao
walipokwisha kuwatisha tena wakawafungua, wasione njia ya kuwaadhibu, kwa
sababu ya watu; kwa kuwa watu wote walikuwa wakimtukuza Mungu kwa hayo
yaliyotendeka;
22 maana
umri wake yule mtu aliyefanyiwa ishara hii ya kuponya ulipita miaka arobaini.
23 Hata
walipofunguliwa, wakaenda kwa watu wao, wakawapasha habari ya mambo yote
waliyoambiwa na wakuu wa makuhani na wazee.
24 Nao
waliposikia, wakampazia Mungu sauti zao kwa moyo mmoja, wakisema, Mola, wewe
ndiwe Mungu, ndiwe uliyefanya mbingu na nchi na bahari na vitu vyote vilivyomo;
25 nawe
ulinena kwa Roho Mtakatifu kwa kinywa cha babaetu Daudi, mtumishi wako, Mbona
mataifa wamefanya ghasia, Na makabila wametafakari ubatili?
26 Wafalme
wa dunia wamejipanga, Na wakuu wamefanya shauri pamoja Juu ya Bwana na juu ya
Kristo wake.
27 Maana
ni kweli, Herode na Pontio Pilato pamoja na Mataifa na watu wa Israeli,
walikusanyika katika mji huu juu ya Mtumishi wako mtakatifu Yesu, uliyemtia
mafuta,
28 ili
wafanye yote ambayo mkono wako na mashauri yako yamekusudia tangu zamani
yatokee.
29 Basi
sasa, Bwana, yaangalie matisho yao; ukawajalie watumwa wako kunena neno lako
kwa ujasiri wote,
30 ukinyosha
mkono wako kuponya; ishara na maajabu vifanyike kwa jina la Mtumishi wako
mtakatifu Yesu.
31 Hata
walipokwisha kumwomba Mungu, mahali pale walipokusanyika pakatikiswa, wote
wakajaa Roho Mtakatifu, wakanena neno la Mungu kwa ujasiri.
32 Na
jamii ya watu walioamini walikuwa na moyo mmoja na roho moja; wala hapana mmoja
aliyesema ya kuwa kitu cho chote alicho nacho ni mali yake mwenyewe; bali walikuwa
na vitu vyote shirika.
33 Na
mitume wakatoa ushuhuda wa kufufuka kwake Yesu kwa nguvu nyingi, na neema
nyingi ikawa juu yao wote.
34 Wala
hapakuwa na mtu mmoja miongoni mwao mwenye mahitaji; kwa sababu watu wote
waliokuwa na viwanja au nyumba waliviuza, wakaileta thamani ya vitu vile
vilivyouzwa,
35 wakaiweka
miguuni pa mitume; kila mtu akagawiwa kwa kadiri ya alivyohitaji.
36 Na
Yusufu, aliyeitwa na mitume Barnaba, (maana yake, Mwana wa faraja), Mlawi,
asili yake ni mtu wa Kipro,
37 alikuwa
na shamba akaliuza, akaileta fedha, akaiweka miguuni pa mitume.