MITHALI - SURA YA 21

1 Moyo wa mfalme huwa katika mkono wa Bwana; Kama mifereji ya maji huugeuza po pote apendapo. 
2 Kila njia ya mtu ni sawa machoni pake mwenyewe; Bali Bwana huipima mioyo. 
3 Kutenda haki na hukumu Humpendeza Bwana kuliko kutoa sadaka. 
4 Macho yenye kiburi, na moyo wa kutakabari, Hata ukulima wa waovu, ni dhambi. 
5 Mawazo ya wenye bidii huuelekea utajiri tu; Bali kila mwenye pupa huuelekea uhitaji. 
6 Kupata akiba ya mali kwa ulimi wa uongo Ni moshi upeperushwao; ni kutafuta mauti. 
7 Jeuri ya wabaya itawaondolea mbali; Kwa sababu wamekataa kutenda hukumu. 
8 Njia yake aliyelemewa na dhambi imepotoka sana; Bali mtu aliye safi, kazi yake ni sawasawa. 
9 Ni afadhali kukaa katika pembe ya darini, Kuliko katika nyumba pana pamoja na mwanamke mgomvi. 
10 Nafsi ya mtu mbaya hutamani uovu; Jirani yake hapati fadhili machoni pake. 
11 Mwenye mzaha aadhibiwapo, mjinga hupata hekima; Na mwenye hekima afundishwapo, hupokea maarifa. 
12 Mwenye haki huitafakari nyumba ya mtu mbaya; Jinsi wabaya waangushwavyo wakaangamia. 
13 Azibaye masikio yake asisikie kilio cha maskini, Yeye naye atalia, lakini hatasikiwa. 
14 Kipawa cha siri hutuliza hasira; Na rushwa bindoni humliza ghadhabu kali. 
15 Ni furaha yao wenye haki kutenda hukumu; Lakini ni uharibifu kwao watendao maovu. 
16 Mtu aikosaye njia ya busara Atakaa katika mkutano wao waliokufa. 
17 Mtu apendaye anasa atakuwa maskini; Apendaye mvinyo na mafuta hatakuwa tajiri. 
18 Mtu asiye haki ni fidia ya wenye haki; Naye afanyaye hila ni badala ya watu wa adili. 
19 Ni afadhali kukaa katika nchi ya nyika; Kuliko na mwanamke mgomvi, mchokozi. 
20 Kuna hazina ya thamani na mafuta katika maskani ya mwenye hekima; Bali mwanadamu aliye mpumbavu huyameza. 
21 Aandamaye haki na fadhili, Ataona uhai na haki na heshima. 
22 Mwenye hekima huupandia mji wao wenye nguvu; Na kuziangusha nguvu za tumaini lao. 
23 Mtu azuiaye kinywa chake na ulimi wake, Atajilinda nafsi yake na taabu. 
24 Mwenye kiburi na kutakabari, jina lake ni mbishi; Hutenda mambo katika majivuno ya kiburi chake. 
25 Matakwa yake mtu mvivu humfisha, Kwa maana mikono yake hukataa kufanya kazi. 
26 Kuna atamaniye kwa choyo mchana kutwa; Bali mwenye haki hutoa wala hanyimi. 
27 Sadaka ya wasio haki ni chukizo; Si zaidi sana ailetapo mwenye nia mbaya! 
28 Shahidi wa uongo atapotea; Bali mtu asikiaye atasema maneno yadumuyo. 
29 Asiye haki huufanya uso wake kuwa mgumu; Bali mtu mnyofu huzifikiri njia zake. 
30 Hapana hekima, wala ufahamu, Wala shauri, juu ya Bwana. 
31 Farasi huwekwa tayari kwa siku ya vita; Lakini Bwana ndiye aletaye wokovu.

TUMA KWA RAFIKI :

Twitter FacebookMore

 
Kuhusu Huduma Hii | Masharti Ya Utumiaji Wa Tovuti Hii | Wasiliana Nasi | Tangaza Kupitia Tovuti Hii