1 Basi
ndipo Pilato alipomtwaa Yesu, akampiga mijeledi.
2 Nao
askari wakasokota taji ya miiba, wakamtia kichwani, wakamvika vazi la zambarau.
3 Wakawa
wakimwendea, wakisema, Salamu! Mfalme wa Wayahudi! Wakampiga makofi.
4 Kisha
Pilato akatokea tena nje, akawaambia, Mtu huyu namleta nje kwenu, mpate
kufahamu ya kuwa mimi sioni hatia yo yote kwake.
5 Ndipo
Yesu alipotoka nje, naye amevaa ile taji ya miiba, na lile vazi la zambarau.
Pilato akawaambia, Tazama, mtu huyu!
6 Basi
wale wakuu wa makuhani na watumishi wao walipomwona, walipiga kelele wakisema,
Msulibishe! Msulibishe! Pilato akawaambia, Mtwaeni ninyi basi, mkamsulibishe;
kwa maana mimi sioni hatia kwake.
7 Wayahudi
wakamjibu, Sisi tunayo sheria, na kwa sheria hiyo amestahili kufa, kwa sababu
alijifanya kuwa Mwana wa Mungu.
8 Basi
Pilato aliposikia neno hilo, akazidi kuogopa.
9 Akaingia
tena ndani ya ile Praitorio, akamwambia Yesu, Wewe umetokapi? Lakini Yesu
hakumpa jibu lo lote.
10 Basi
Pilato akamwambia, Husemi nami? Hujui ya kuwa mimi nina mamlaka ya kukufungua,
nami nina mamlaka ya kukusulibisha?
11 Yesu
akamjibu, Wewe hungekuwa na mamlaka yo yote juu yangu, kama usingepewa kutoka
juu; kwa hiyo yeye aliyenitia mikononi mwako yuna dhambi iliyo kubwa zaidi.
12 Na
tangu hapo Pilato akatafuta kumfungua; lakini Wayahudi wakapiga makelele
wakisema, Ukimfungua huyu, wewe si rafiki yake Kaisari; kila mtu ajifanyaye
kuwa mfalme humfitini Kaisari.
13 Basi
Pilato, aliposikia maneno hayo, akamleta Yesu nje, akaketi juu ya kiti cha
hukumu, mahali paitwapo Sakafu ya Mawe, au kwa Kiebrania, Gabatha.
14 Nayo
ilikuwa Maandalio ya pasaka, yapata saa sita. Akawaambia Wayahudi, Tazama,
Mfalme wenu!
15 Basi
wale wakapiga kelele, Mwondoshe! Mwondoshe! Msulibishe! Pilato akawaambia, Je!
Nimsulibishe mfalme wenu! Wakuu wa makuhani wakamjibu, Sisi hatuna mfalme ila
Kaisari.
16 Basi
ndipo alipomtia mikononi mwao ili asulibiwe; nao wakampokea Yesu.
17 Akatoka,
hali akijichukulia msalaba wake, mpaka mahali paitwapo Fuvu la Kichwa, au kwa
Kiebrania, Golgotha.
18 Wakamsulibisha
huko, na wengine wawili pamoja naye, mmoja huku na mmoja huku, na Yesu
katikati.
19 Naye
Pilato akaandika anwani, akaiweka juu ya msalaba, imeandikwa, YESU MNAZARETI,
MFALME WA WAYAHUDI.
20 Basi
anwani hiyo waliisoma wengi katika Wayahudi; maana mahali pale aliposulibiwa
Yesu palikuwa karibu na mji; nayo iliandikwa kwa Kiebrania, na Kirumi, na
Kiyunani.
21 Basi
wakuu wa makuhani na Wayahudi wakamwambia Pilato, Usiandike, Mfalme wa
Wayahudi; bali ya kwamba yule alisema, Mimi ni mfalme wa Wayahudi.
22 Pilato
akajibu, Niliyoandika nimeyaandika.
23 Nao
askari walipomsulibisha Yesu, waliyatwaa mavazi yake, wakafanya mafungu manne,
kwa kila askari fungu lake; na kanzu nayo. Basi kanzu ile haikushonwa, ilikuwa
imefumwa yote pia tangu juu.
24 Basi
wakaambiana, Tusiipasue, lakini tuipigie kura, iwe ya nani. Ili litimie andiko
lile linenalo, Waligawanya nguo zangu, Na vazi langu wakalipigia kura. Basi
ndivyo walivyofanya wale askari.
25 Na
penye msalaba wake Yesu walikuwa wamesimama mamaye, na umbu la mamaye, Mariamu
wa Klopa, na Mariamu Magdalene.
26 Basi
Yesu alipomwona mama yake, na yule mwanafunzi aliyempenda amesimama karibu,
alimwambia mama yake, Mama, tazama, mwanao.
27 Kisha
akamwambia yule mwanafunzi, Tazama, mama yako. Na tangu saa ile mwanafunzi yule
akamchukua nyumbani kwake.
28 Baada
ya hayo Yesu, hali akijua ya kuwa yote yamekwisha kumalizika ili andiko
litimizwe, akasema, Naona kiu.
29 Kulikuwako
huko chombo kimejaa siki; basi wakatia sifongo iliyojaa siki juu ya ufito wa
hisopo, wakampelekea kinywani.
30 Basi
Yesu alipokwisha kuipokea ile siki, alisema, Imekwisha. Akainama kichwa,
akaisalimu roho yake.
31 Basi
Wayahudi, kwa sababu ni Maandalio, miili isikae juu ya misalaba siku ya sabato,
(maana sabato ile ilikuwa siku kubwa), walimwomba Pilato miguu yao ivunjwe,
wakaondolewe.
32 Basi
askari wakaenda, wakamvunja miguu wa kwanza, na wa pili, aliyesulibiwa pamoja
naye.
33 Lakini
walipomjia Yesu na kuona ya kuwa amekwisha kufa, hawakumvunja miguu;
34 lakini
askari mmojawapo alimchoma ubavu kwa mkuki; na mara ikatoka damu na maji.
35 Naye
aliyeona ameshuhudia, na ushuhuda wake ni kweli; naye anajua ya kuwa anasema
kweli ili ninyi nanyi mpate kusadiki.
36 Kwa
maana hayo yalitukia ili andiko litimie, Hapana mfupa wake utakaovunjwa.
37 Na
tena andiko lingine lanena, Watamtazama yeye waliyemchoma.
38 Hata
baada ya hayo Yusufu wa Arimathaya, naye ni mwanafunzi wa Yesu, (lakini kwa
siri, kwa hofu ya Wayahudi), alimwomba Pilato ruhusa ili auondoe mwili wake
Yesu. Na Pilato akampa ruhusa. Basi akaenda, akauondoa mwili wake.
39 Akaenda
Nikodemo naye, (yule aliyemwendea usiku hapo kwanza), akaleta machanganyiko ya
manemane na uudi, yapata ratli mia.
40 Basi
wakautwaa mwili wake Yesu, wakaufunga sanda ya kitani pamoja na yale manukato, kama
ilivyo desturi ya Wayahudi katika kuzika.
41 Na
pale pale aliposulibiwa palikuwa na bustani; na ndani ya bustani mna kaburi
jipya, ambalo hajatiwa bado mtu ye yote ndani yake.
42 Humo
basi, kwa sababu ya Maandalio ya Wayahudi, wakamweka Yesu; maana lile kaburi
lilikuwa karibu.