1 Na
baada ya hayo Yesu alikuwa akitembea katika Galilaya; maana hakutaka kutembea
katika Uyahudi, kwa sababu Wayahudi walikuwa wakitafuta kumwua.
2 Na
sikukuu ya Wayahudi, Sikukuu ya Vibanda, ilikuwa karibu.
3 Basi
ndugu zake wakamwambia, Ondoka hapa, uende Uyahudi, wanafunzi wako nao wapate
kuzitazama kazi zako unazozifanya.
4 Kwa
maana hakuna mtu afanyaye neno kwa siri, naye mwenyewe ataka kujulikana.
Ukifanya mambo haya, basi jidhihirishe kwa ulimwengu.
5 Maana
hata nduguze hawakumwamini.
6 Basi
Yesu akawaambia, Haujafika bado wakati wangu; ila wakati wenu sikuzote upo.
7 Ulimwengu
hauwezi kuwachukia ninyi; bali hunichukia mimi, kwa sababu mimi naushuhudia ya
kuwa kazi zake ni mbovu.
8 Kweeni
ninyi kwenda kula sikukuu; mimi sikwei bado kwenda kula sikukuu hii, kwa kuwa
haujatimia wakati wangu.
9 Naye
alipokwisha kuwaambia hayo, alikaa vivi hivi huko Galilaya.
10 Hata
ndugu zake walipokwisha kukwea kuiendea sikukuu, ndipo yeye naye alipokwea, si
kwa wazi bali kana kwamba kwa siri.
11 Basi
Wayahudi wakamtafuta kwenye sikukuu, wakasema, Yuko wapi yule?
12 Kukawa
na manung'uniko mengi katika makutano juu yake. Wengine wakasema, Ni mtu mwema.
Na wengine wakasema, Sivyo; bali anawadanganya makutano.
13 Walakini
hakuna mtu aliyemtaja waziwazi, kwa sababu ya kuwaogopa Wayahudi.
14 Hata
ikawa katikati ya sikukuu Yesu alikwea kuingia hekaluni, akafundisha.
15 Wayahudi
wakastaajabu wakisema, Amepataje huyu kujua elimu, ambaye hakusoma?
16 Basi
Yesu akawajibu, akasema, Mafunzo yangu si yangu mimi, ila ni yake yeye
aliyenipeleka.
17 Mtu
akipenda kuyatenda mapenzi yake, atajua habari ya yale mafunzo, kwamba yatoka
kwa Mungu, au kwamba mimi nanena kwa nafsi yangu tu.
18 Yeye
anenaye kwa nafsi yake tu hutafuta utukufu wake mwenyewe; bali yeye anayetafuta
utukufu wake aliyempeleka, huyo ni wa kweli, wala ndani yake hamna udhalimu.
19 Je!
Musa hakuwapa torati? Wala hakuna mmoja wenu aitendaye torati. Mbona mnatafuta
kuniua?
20 Mkutano
wakajibu, Ama! Una pepo! Ni nani anayetafuta kukuua?
21 Yesu
akajibu, akawaambia, Mimi nalitenda kazi moja, nanyi nyote mnaistaajabia.
22 Musa
aliwapa tohara; lakini si kwamba yatoka kwa Musa, bali kwa mababa; nanyi siku
ya sabato humtahiri mtu.
23 Basi
ikiwa mtu hupashwa tohara siku ya sabato, ili torati ya Musa isije ikavunjika,
mbona mnanikasirikia mimi kwa sababu nalimfanya mtu kuwa mzima kabisa siku ya
sabato?
24 Basi
msihukumu hukumu ya macho tu, bali ifanyeni hukumu iliyo ya haki.
25 Basi
baadhi ya watu wa Yerusalemu wakasema, Je! Huyu siye wanayemtafuta ili wamwue?
26 Na
kumbe! Anena waziwazi, wala hawamwambii neno! Yamkini hao wakuu wanajua hakika
ya kuwa huyu ndiye Kristo?
27 Lakini
huyu twamjua atokako; bali Kristo atakapokuja hakuna ajuaye atokako.
28 Basi
Yesu akapaza sauti yake hekaluni, akifundisha na kusema, Mimi mnanijua, na huko
nitokako mnakujua; wala sikuja kwa nafsi yangu; ila yeye aliyenipeleka ni wa
kweli, msiyemjua ninyi.
29 Mimi
namjua, kwa kuwa nimetoka kwake, naye ndiye aliyenituma.
30 Basi
wakatafuta kumkamata; lakini hakuna mtu aliyeunyosha mkono wake ili kumshika,
kwa sababu saa yake ilikuwa haijaja bado.
31 Na
watu wengi katika mkutano wakamwamini; wakasema, Atakapokuja Kristo, je!
Atafanya ishara nyingi zaidi kuliko hizi alizozifanya huyu?
32 Mafarisayo
wakawasikia mkutano wakinung'unika hivi juu yake; basi wakuu wa makuhani na
Mafarisayo wakatuma watumishi ili wamkamate.
33 Basi
Yesu akasema, Bado kitambo kidogo nipo pamoja nanyi; kisha naenda zangu kwake
yeye aliyenipeleka.
34 Mtanitafuta
wala hamtaniona; nami nilipo ninyi hamwezi kuja.
35 Basi
Wayahudi wakasemezana, Huyu atakwenda wapi hata sisi tusimwone? Ati! Atakwenda
kwa Utawanyiko wa Wayunani, na kuwafundisha Wayunani?
36 Ni
neno gani hilo alilolisema, Mtanitafuta wala hamtaniona; nami nilipo ninyi
hamwezi kuja?
37 Hata
siku ya mwisho, siku ile kubwa ya sikukuu, Yesu akasimama, akapaza sauti yake
akisema, Mtu akiona kiu, na aje kwangu anywe.
38 Aniaminiye
mimi, kama vile maandiko yalivyonena, mito ya maji yaliyo hai itatoka ndani
yake.
39 Na
neno hilo alilisema katika habari ya Roho, ambaye wale wamwaminio watampokea
baadaye; kwa maana Roho alikuwa hajaja, kwa sababu Yesu alikuwa hajatukuzwa.
40 Basi
wengine katika mkutano walipoyasikia maneno hayo, walisema, Hakika huyu ndiye
nabii yule.
41 Wengine
walisema, Huyu ndiye Kristo. Wengine wakasema, Je! Kristo atoka Galilaya?
42 Andiko
halikusema ya kwamba Kristo atoka katika uzao wa Daudi, na kutoka Bethlehemu,
mji ule alioukaa Daudi?
43 Basi
kukaingia matengano katika mkutano kwa ajili yake.
44 Baadhi
yao wakataka kumkamata, lakini hakuna mtu aliyenyosha mikono yake ili kumshika.
45 Basi
wale watumishi wakawaendea wakuu wa makuhani na Mafarisayo. Nao wakawaambia,
Mbona hamkumleta?
46 Wale
watumishi wakajibu. Hajanena kamwe mtu ye yote kama huyu anavyonena.
47 Basi
Mafarisayo wakawajibu, Je! Ninyi nanyi mmedanganyika?
48 Ni
nani katika wakuu amwaminiye, au katika Mafarisayo?
49 Lakini
makutano hawa wasioifahamu torati wamelaaniwa.
50 Akawaambia
Nikodemo, (naye ni yule aliyemwendea zamani, maana ni mmoja wao),
51 Je!
Torati yetu humhukumu mtu kabla ya kumsikia kwanza, na kujua atendavyo?
52 Wakajibu,
wakamwambia, Je! Wewe nawe umetoka Galilaya!
53 Tafuta,
ukaone ya kuwa kutoka Galilaya hakutokea nabii.