1 Hata
alipokuwa akipita alimwona mtu, kipofu tangu kuzaliwa.
2 Wanafunzi
wake wakamwuliza wakisema, Rabi, ni yupi aliyetenda dhambi, mtu huyu au wazazi
wake, hata azaliwe kipofu?
3 Yesu
akajibu, Huyu hakutenda dhambi, wala wazazi wake; bali kazi za Mungu
zidhihirishwe ndani yake.
4 Imetupasa
kuzifanya kazi zake yeye aliyenipeleka maadamu ni mchana, usiku waja asipoweza
mtu kufanya kazi.
5 Muda
nilipo ulimwenguni, mimi ni nuru ya ulimwengu.
6 Alipokwisha
kusema hayo, alitema mate chini, akafanya tope kwa yale mate. Akampaka kipofu
tope za macho,
7 akamwambia,
Nenda kanawe katika birika ya Siloamu, (maana yake, Aliyetumwa). Basi akaenda
na kunawa; akarudi anaona.
8 Basi
jirani zake, na wale waliomwona zamani kuwa ni mwombaji, wakasema, Je! Huyu
siye yule aliyekuwa akiketi na kuomba?
9 Wengine
wakasema, Ndiye. Wengine wakasema, La, lakini amefanana naye. Yeye mwenyewe
alisema, Mimi ndiye.
10 Basi
wakamwambia, Macho yako yalifumbuliwaje?
11 Yeye
akajibu, Mtu yule aitwaye Yesu alifanya tope, akanipaka macho akaniambia, Nenda
Siloamu ukanawe; basi nikaenda na kunawa, nikapata kuona.
12 Wakamwambia,
Yuko wapi huyo? Akasema, Mimi sijui.
13 Basi
wakampeleka kwa Mafarisayo yule aliyekuwa kipofu zamani.
14 Nayo
ilikuwa sabato, hapo Yesu alipofanya zile tope na kumfumbua macho.
15 Basi
Mafarisayo nao wakamwuliza tena jinsi gani alivyopata kuona. Akawaambia,
Alinitia tope juu ya macho, nami nikanawa, na sasa naona.
16 Basi
baadhi ya Mafarisayo wakasema, Mtu huyo hakutoka kwa Mungu, kwa sababu haishiki
sabato. Wengine wakasema, Awezaje mtu mwenye dhambi kufanya ishara kama hizo?
Kukawa matengano kati yao.
17 Basi
wakamwambia yule kipofu mara ya pili, Wewe wasemaje katika habari zake kwa vile
alivyokufumbua macho? Akasema, Ni nabii.
18 Basi
Wayahudi hawakusadiki habari zake, ya kuwa alikuwa kipofu, kisha akapata kuona;
hata walipowaita wazazi wake yule aliyepata kuona.
19 Wakawauliza
wakisema, Huyu ndiye mwana wenu, ambaye mnasema kwamba alizaliwa kipofu?
Amepataje, basi, kuona sasa?
20 Wazazi
wake wakawajibu, wakasema, Tunajua ya kuwa huyu ndiye mwana wetu, tena ya kuwa
alizaliwa kipofu;
21 lakini
jinsi aonavyo sasa hatujui; wala hatujui ni nani aliyemfumbua macho. Mwulizeni
yeye mwenyewe; yeye ni mtu mzima; atajisemea mwenyewe.
22 Wazazi
wake waliyasema hayo kwa sababu waliwaogopa Wayahudi; kwa maana Wayahudi
walikuwa wamekwisha kuafikiana kwamba mtu akimkiri kuwa ni Kristo, atatengwa na
sinagogi.
23 Ndiyo
sababu wale wazazi wake walisema, Ni mtu mzima, mwulizeni yeye.
24 Basi
mara ya pili wakamwita yule mtu aliyekuwa kipofu, wakamwambia, Mpe Mungu
utukufu. Sisi tunajua ya kuwa mtu huyo ni mwenye dhambi.
25 Basi
yule mtu akajibu, Kwamba yeye ni mwenye dhambi sijui. Najua neno moja, kuwa
mimi nalikuwa kipofu na sasa naona.
26 Basi
wakamwambia, Alikutendea nini? Alikufumbua macho jinsi gani?
27 Akawajibu,
Nimekwisha kuwaambia, wala hamkusikia; mbona mnataka kusikia tena? Ninyi nanyi
mnataka kuwa wanafunzi wake?
28 Basi
wakamshutumu, wakasema, Wewe u mwanafunzi wake yule; sisi tu wanafunzi wa Musa.
29 Sisi
tunajua ya kuwa Mungu alisema na Musa; bali yule hatujui atokako.
30 Yule
mtu akajibu, akawaambia, Hii ni ajabu! Kwamba ninyi hamjui atokako, naye
alinifumbua macho!
31 Twajua
ya kuwa Mungu hawasikii wenye dhambi; bali mtu akiwa ni mcha Mungu, na
kuyafanya mapenzi yake, humsikia huyo.
32 Tokea
hapo haijasikiwa ya kuwa mtu ameyafumbua macho ya kipofu, ambaye alizaliwa hali
hiyo.
33 Kama
huyo asingalitoka kwa Mungu, asingeweza kutenda neno lo lote.
34 Wakajibu,
wakamwambia, Ama! Wewe ulizaliwa katika dhambi tupu, nawe unatufundisha sisi? Wakamtoa
nje.
35 Yesu
akasikia kwamba wamemtoa nje; naye alipomwona alisema, Wewe wamwamini Mwana wa
Mungu?
36 Naye
akajibu akasema, Ni nani, Bwana, nipate kumwamini?
37 Yesu
akamwambia, Umemwona, naye anayesema nawe ndiye.
38 Akasema,
Naamini, Bwana. Akamsujudia.
39 Yesu
akasema, Mimi nimekuja ulimwenguni humu kwa hukumu, ili wao wasioona waone, nao
wanaoona wawe vipofu.
40 Baadhi
ya Mafarisayo waliokuwapo pamoja naye wakasikia hayo, wakamwambia, Je! Sisi
nasi tu vipofu?
41 Yesu
akawaambia, Kama mngekuwa vipofu, msingekuwa na dhambi; lakini sasa mwasema,
Twaona; basi dhambi yenu inakaa.