ZEKARIA - SURA YA 10

1 Mwombeni Bwana mvua wakati wa masika, naam, Bwana afanyaye umeme, naye atawapa manyunyu ya mvua, kila mtu atapewa nyasi kondeni. 
2 Kwa maana vinyago vimenena maneno ya ubatili, nao waaguzi wameona uongo; nao wameleta habari za ndoto za uongo, wafariji bure; kwa sababu hiyo waenda zao kama kondoo, wateswa, kwa sababu hapana mchungaji. 
3 Hasira yangu imewaka juu ya wachungaji, nami nitawaadhibu mbuzi waume; kwa maana Bwana wa majeshi ameliangalia kundi lake, yaani, nyumba ya Yuda, naye atawafanya kuwa kama farasi wake mzuri vitani. 
4 Kwake yeye litatoka lile jiwe la pembeni, kwake yeye utatoka msumari, kwake yeye utatoka upinde wa vita, kwake yeye atatoka kila mtawala pamoja. 
5 Nao watakuwa kama mashujaa, wakanyagao adui zao katika matope ya njia vitani; nao watapiga vita, kwa sababu Bwana yu pamoja nao; na hao wapandao farasi watafadhaishwa. 
6 Nami nitaitia nguvu nyumba ya Yuda, nami nitaiokoa nyumba ya Yusufu, nami nitawarudisha, kwa maana nawaonea rehema; nao watakuwa kana kwamba sikuwatupa; kwa maana mimi ni Bwana, Mungu wao, nami nitawasikia. 
7 Na watu wa Efraimu watakuwa kama shujaa, na moyo wao utafurahi kana kwamba ni kwa divai; naam, watoto wao wataona mambo haya, na kufurahi; mioyo yao itamfurahia Bwana. 
8 Nitawapigia kelele, na kuwakusanya pamoja; kwa maana nimewakomboa; nao wataongezeka kama walivyoongezeka. 
9 Nami nitawapanda kama mbegu kati ya mataifa; nao watanikumbuka katika nchi zilizo mbali; nao watakaa pamoja na watoto wao; tena watarudi. 
10 Tena nitawarudisha toka nchi ya Misri, nitawakusanya na kuwatoa katika Ashuru; nami nitawaingiza katika nchi ya Gileadi na Lebanoni; ila nafasi ya kuwatosha haitaonekana. 
11 Naye atapita kati ya bahari ya mateso, na kuyapiga mawimbi ya bahari, na vilindi vyote vya mto wa Nile vitakauka; na kiburi cha Ashuru kitashushwa; na fimbo ya enzi ya Misri itatoweka. 
12 Nami nitawatia nguvu katika Bwana; nao watatembea huko na huko katika jina lake, asema Bwana.

TUMA KWA RAFIKI :

Twitter FacebookMore

 
Kuhusu Huduma Hii | Masharti Ya Utumiaji Wa Tovuti Hii | Wasiliana Nasi | Tangaza Kupitia Tovuti Hii