1 Naye alipowaona makutano, alipanda mlimani; na
alipokwisha kuketi, wanafunzi wake walimjia;
2 akafumbua kinywa chake, akawafundisha, akisema,
3 Heri walio maskini wa roho; Maana ufalme wa
mbinguni ni wao.
4 Heri wenye huzuni; Maana hao watafarijika.
5 Heri wenye upole; Maana hao watairithi nchi.
6 Heri wenye njaa na kiu ya haki; Maana hao
watashibishwa.
7 Heri wenye rehema; Maana hao watapata rehema.
8 Heri wenye moyo safi; Maana hao watamwona Mungu.
9 Heri wapatanishi; Maana hao wataitwa wana wa
Mungu.
10 Heri wenye kuudhiwa kwa ajili ya haki; Maana
ufalme wa mbinguni ni wao.
11 Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na
kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu.
12 Furahini, na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu
ni kubwa mbinguni; kwa maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu.
13 Ninyi ni chumvi ya dunia; lakini chumvi ikiwa
imeharibika itatiwa nini hata ikolee? Haifai tena kabisa, ila kutupwa nje na
kukanyagwa na watu.
14 Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji hauwezi
kusitirika ukiwa juu ya mlima.
15 Wala watu hawawashi taa na kuiweka chini ya
pishi, bali juu ya kiango; nayo yawaangaza wote waliomo nyumbani.
16 Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu,
wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni.
17 Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au
manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza.
18 Kwa maana, amin, nawaambia ,Mpaka mbingu na nchi
zitakapoondoka,yodi moja wala nukta moja ya torati haitaoondoka ,hata yote
yatimie.
19 Basi mtu ye yote atakayevunja amri moja katika hizi
zilizo ndogo, na kuwafundisha watu hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika ufalme wa
mbinguni; bali mtu atakayezitenda na kuzifundisha, huyo ataitwa mkubwa katika
ufalme wa mbinguni.
20 Maana nawaambia ya kwamba, Haki yenu isipozidi
hiyo haki ya waandishi na Mafarisayo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa
mbinguni.
21 Mmesikia watu wa kale walivyoambiwa, Usiue, na
mtu akiua, itampasa hukumu.
22 Bali mimi nawaambieni, Kila amwoneaye ndugu yake
hasira itampasa hukumu; na mtu akimfyolea ndugu yake, itampasa baraza; na mtu
akimwapiza, itampasa jehanum ya moto.
23 Basi ukileta sadaka yako madhabahuni, na huku
ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno juu yako,
24 iache sadaka yako mbele ya madhabahu, uende
zako, upatane kwanza na ndugu yako, kisha urudi uitoe sadaka yako.
25 Patana na mshitaki wako upesi, wakati uwapo
pamoja naye njiani; yule mshitaki asije akakupeleka kwa kadhi, na kadhi
akakupeleka kwa askari, ukatupwa gerezani.
26 Amin, nakuambia, Hutoki humo kamwe hata uishe
kulipa senti ya mwisho.
27 Mmesikia kwamba imenenwa, Usizini;
28 lakini mimi nawaambia, Kila mtu atazamaye
mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake.
29 Jicho lako la kuume likikukosesha, ling'oe
ulitupe mbali nawe; kwa maana yakufaa kiungo chako kimoja kipotee wala mwili
wako mzima usitupwe katika jehanum.
30 Na mkono wako wa kuume ukikukosesha, ukate
uutupe mbali nawe; kwa maana yakufaa kiungo chako kimoja kipotee wala mwili
wako mzima usitupwe katika jehanum.
31 Imenenwa pia, Mtu akimwacha mkewe, na ampe hati ya
talaka;
32 lakini mimi nawaambia, Kila mtu amwachaye mkewe,
isipokuwa kwa habari ya uasherati, amfanya kuwa mzinzi; na mtu akimwoa yule
aliyeachwa, azini.
33 Tena mmesikia watu wa kale walivyoambiwa, Usiape
uongo, ila mtimizie Bwana nyapo zako;
34 lakini mimi nawaambia, Usiape kabisa; hata kwa
mbingu, kwa maana ndicho kiti cha enzi cha Mungu;
35 wala kwa nchi, kwa maana ndiyo pa kuwekea miguu
yake; wala kwa Yerusalemu, kwa maana ndio mji wa Mfalme mkuu.
36 Wala usiape kwa kichwa chako, maana huwezi kufanya
unywele mmoja kuwa mweupe au mweusi.
37 Bali maneno yenu yawe Ndiyo, ndiyo; Siyo, siyo;
kwa kuwa yazidiyo hayo yatoka kwa yule mwovu.
38 Mmesikia kwamba imenenwa, Jicho kwa jicho, na
jino kwa jino;
39 Lakini mimi nawaambia, Msishindane na mtu mwovu;
lakini mtu akupigaye shavu la kuume, mgeuzie na la pili.
40 Na mtu atakaye kukushitaki na kuitwaa kanzu
yako, mwachie na joho pia.
41 Na mtu atakayekulazimisha mwendo wa maili moja,
nenda naye mbili.
42 Akuombaye, mpe; naye atakaye kukopa kwako, usimpe
kisogo.
43 Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako,
na, Umchukie adui yako;
44 lakini mimi nawaambia, Wapendeni adui zenu,
waombeeni wanaowaudhi,
45 ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni;
maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na
wasio haki.
46 Maana mkiwapenda wanaowapenda ninyi mwapata
thawabu gani? Hata watoza ushuru, je! Nao hawafanyi yayo hayo?
47 Tena mkiwaamkia ndugu zenu tu, mnatenda tendo
gani la ziada? Hata watu wa mataifa, je! Nao hawafanyi kama hayo?
48 Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa
mbinguni alivyo mkamilifu.