1 Angalieni msifanye wema wenu machoni pa watu,
kusudi mtazamwe na wao; kwa maana mkifanya kama hayo, hampati thawabu kwa Baba
yenu aliye mbinguni.
2 Basi wewe utoapo sadaka, usipige panda mbele
yako, kama wanafiki wafanyavyo katika masinagogi na njiani, ili watukuzwe na
watu.
3 Amin, nawaambieni, Wamekwisha kupata thawabu
yao. Bali wewe utoapo sadaka, hata mkono wako wa kushoto usijue ufanyalo mkono
wako wa kuume;
4 sadaka yako iwe kwa siri; na Baba yako aonaye
sirini atakujazi.
5 Tena msalipo, msiwe kama wanafiki; kwa maana wao
wapenda kusali hali wamesimama katika masinagogi na katika pembe za njia, ili
waonekane na watu. Amin, nawaambia, Wamekwisha kupata thawabu yao.
6 Bali wewe usalipo, ingia katika chumba chako cha
ndani, na ukiisha kufunga mlango wako, usali mbele za Baba yako aliye sirini;
na Baba yako aonaye sirini atakujazi.
7 Nanyi mkiwa katika kusali, msipayuke-payuke,
kama watu wa mataifa; maana wao hudhani ya kuwa watasikiwa kwa sababu ya maneno
yao kuwa mengi.
8 Basi msifanane na hao; maana Baba yenu anajua
mnayohitaji kabla ninyi hamjamwomba.
9 Basi ninyi salini hivi; Baba yetu uliye
mbinguni, Jina lako litukuzwe, Ufalme wako uje,
10 Mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko
mbinguni.
11 Utupe leo riziki yetu.
12 Utusamehe deni zetu, kama sisi nasi
tuwasamehevyo wadeni wetu.
13 Na usitutie majaribuni, lakini utuokoe na yule
mwovu. [Kwa kuwa ufalme ni wako, na nguvu, na utukufu, hata milele. Amina.]
14 Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na Baba
yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi.
15 Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala Baba
yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu.
16 Tena mfungapo, msiwe kama wanafiki wenye uso wa
kukunjamana; maana hujiumbua nyuso zao, ili waonekane na watu kuwa wanafunga.
Amin, nawaambia, wamekwisha kupata thawabu yao.
17 Bali wewe ufungapo, jipake mafuta kichwani,
unawe uso;
18 ili usionekane na watu kuwa unafunga, ila na
Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi.
19 Msijiwekee hazina duniani, nondo na kutu
viharibupo, na wevi huvunja na kuiba;
20 bali jiwekeeni hazina mbinguni, kusikoharibika
kitu kwa nondo wala kutu, wala wevi hawavunji wala hawaibi;
21 kwa kuwa hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwapo
na moyo wako.
22 Taa ya mwili ni jicho; basi jicho lako likiwa
safi, mwili wako wote utakuwa na nuru.
23 Lakini jicho lako likiwa bovu, mwili wako wote
utakuwa na giza. Basi ile nuru iliyomo ndani yako ikiwa giza; si giza hilo!
24 Hakuna mtu awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa
maana atamchukia huyu, na kumpenda huyu; ama atashikamana na huyu, na kumdharau
huyu. Hamwezi kumtumikia Mungu na mali.
25 Kwa sababu hiyo nawaambieni, Msisumbukie maisha
yenu, mle nini au mnywe nini; wala miili yenu, mvae nini. Maisha je! Si zaidi
ya chakula, na mwili zaidi ya mavazi?
26 Waangalieni ndege wa angani, ya kwamba
hawapandi, wala hawavuni, wala hawakusanyi ghalani; na Baba yenu wa mbinguni
huwalisha hao. Ninyi je! Si bora kupita hao?
27 Ni yupi kwenu ambaye akijisumbua aweza
kujiongeza kimo chake hata mkono mmoja?
28 Na mavazi, ya nini kuyasumbukia? Fikirini maua
ya mashamba, jinsi yameavyo; hayafanyi kazi, wala hayasokoti
29 nami nawaambia, ya kwamba hata Sulemani katika
fahari yake yote hakuvikwa vizuri kama mojawapo la hayo.
30 Basi, ikiwa Mungu huyavika hivi majani ya
kondeni, yaliyopo leo, na kesho hutupwa kalibuni, je! Hatazidi sana kuwavika
ninyi, enyi wa imani haba?
31 Msisumbuke, basi, mkisema, Tule nini? Au Tunywe
nini? Au Tuvae nini?
32 Kwa maana hayo yote Mataifa huyatafuta; kwa
sababu Baba yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote.
33 Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake;
na hayo yote mtazidishiwa.
34 Basi msisumbukie ya kesho; kwa kuwa kesho
itajisumbukia yenyewe. Yatosha kwa siku maovu yake.