1 Akawaita wanafunzi wake kumi na wawili, akawapa
amri juu ya pepo wachafu, wawatoe, na kupoza magonjwa yote na udhaifu wa kila
aina.
2 Na majina ya hao mitume kumi na wawili ni haya;
Wa kwanza Simoni aliyeitwa Petro, na Andrea nduguye; Yakobo wa Zebedayo, na
Yohana nduguye;
3 Filipo, na Bartholomayo; Tomaso, na Mathayo
mtoza ushuru; Yakobo wa Alfayo, na Thadayo;
4 Simoni Mkananayo, na Yuda Iskariote, naye ndiye
mwenye kumsaliti.
5 Hao Thenashara Yesu aliwatuma, akawaagiza,
akisema, Katika njia ya Mataifa msiende, wala katika mji wo wote wa Wasamaria
msiingie.
6 Afadhali shikeni njia kuwaendea kondoo
waliopotea wa nyumba ya Israeli.
7 Na katika kuenenda kwenu, hubirini, mkisema,
Ufalme wa mbinguni umekaribia.
8 Pozeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye
ukoma, toeni pepo; mmepata bure, toeni bure.
9 Msichukue dhahabu, wala fedha, wala mapesa
mishipini mwenu;
10 wala mkoba wa safari, wala kanzu mbili, wala
viatu, wala fimbo; maana mtenda kazi astahili posho lake.
11 Na mji wo wote au kijiji cho chote
mtakachoingia, tafuteni ni nani humo aliye mtu mwaminifu; mkae kwake hata
mtakapotoka.
12 Nanyi mkiingia katika nyumba isalimuni.
13 Na nyumba ile ikistahili, amani yenu na iifikilie;
la, kwamba haistahili, amani yenu na iwarudie ninyi.
14 Na mtu asipowakaribisha wala kuyasikiliza maneno
yenu, mtokapo katika nyumba ile, au mji ule, kung'uteni mavumbi ya miguuni
mwenu.
15 Amin, nawaambia, itakuwa rahisi nchi ya Sodoma
na Gomora kustahimili adhabu ya siku ya hukumu, kuliko mji ule.
16 Angalieni, mimi nawatuma kama kondoo kati ya
mbwa-mwitu; basi iweni na busara kama nyoka, na kuwa watu wapole kama hua.
17 Jihadharini na wanadamu; kwa maana watawapeleka
mabarazani, na katika masinagogi yao watawapiga;
18 nanyi mtachukuliwa mbele ya maliwali na wafalme
kwa ajili yangu, kuwa ushuhuda kwao na kwa mataifa.
19 Lakini hapo watakapowapeleka, msifikiri-fikiri
jinsi mtakavyosema; maana mtapewa saa ile mtakayosema.
20 Kwa kuwa si ninyi msemao, bali ni Roho wa Baba
yenu asemaye ndani yenu.
21 Na ndugu atamsaliti nduguye ili auawe, na baba
atamsaliti mwana, na wana watawainukia wazazi wao, na kuwafisha.
22 Nanyi mtakuwa mkichukiwa na watu wote kwa ajili
ya jina langu; lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka.
23 Lakini watakapowafukuza katika mji huu,
kimbilieni mwingine; kwa maana ni kweli nawaambia, Hamtaimaliza miji ya
Israeli, hata ajapo Mwana wa Adamu.
24 Mwanafunzi hampiti mwalimu wake, wala mtumwa
hampiti bwana wake.
25 Yamtosha mwanafunzi kuwa kama mwalimu wake, na
mtumwa kuwa kama bwana wake. Ikiwa wamemwita mwenye nyumba Beelzebuli, je! Si
zaidi wale walio wa nyumbani mwake?
26 Basi, msiwaogope, kwa maana hakuna neno
lililositirika, ambalo halitafunuliwa; wala lililofichwa, ambalo
halitajulikana.
27 Niwaambialo ninyi katika giza, lisemeni katika
nuru; na msikialo kwa siri, lihubirini juu ya nyumba.
28 Msiwaogope wauuao mwili, wasiweze kuiua na roho;
afadhali mwogopeni yule awezaye kuangamiza mwili na roho pia katika jehanum.
29 Je! Mashomoro wawili hawauzwi kwa senti moja?
Wala hata mmoja haanguki chini asipojua Baba yenu;
30 lakini ninyi, hata nywele za vichwa vyenu
zimehesabiwa zote.
31 Msiogope basi; bora ninyi kuliko mashomoro
wengi.
32 Basi, kila mtu atakayenikiri mbele ya watu, nami
nitamkiri mbele za Baba yangu aliye mbinguni.
33 Bali mtu ye yote atakayenikana mbele ya watu,
nami nitamkana mbele za Baba yangu aliye mbinguni.
34 Msidhani ya kuwa nimekuja kuleta amani duniani;
la! Sikuja kuleta amani, bali upanga.
35 Kwa maana nalikuja kumfitini mtu na babaye, na
binti na mamaye, na mkwe na mkwe mtu;
36 na adui za mtu ni wale wa nyumbani mwake.
37 Apendaye baba au mama kuliko mimi, hanistahili;
wala apendaye mwana au binti kuliko mimi, hanistahili.
38 Wala mtu asiyechukua msalaba wake akanifuata,
hanistahili.
39 Mwenye kuiona nafsi yake ataipoteza; naye mwenye
kuipoteza nafsi yake kwa ajili yangu ataiona.
40 Awapokeaye ninyi, anipokea mimi; naye anipokeaye
mimi, ampokea yeye aliyenituma.
41 Ampokeaye nabii kwa kuwa ni nabii, atapata
thawabu ya nabii; naye ampokeaye mwenye haki kwa kuwa ni mwenye haki, atapata
thawabu ya mwenye haki.
42 Na mtu awaye yote atakayemnywesha mmojawapo wa
wadogo hawa ngaa kikombe cha maji ya baridi, kwa kuwa ni mwanafunzi, amin,
nawaambia, haitampotea kamwe thawabu yake.