1 Ikawa Yesu alipokwisha kuwaagiza wanafunzi wake
kumi na wawili, alitoka huko kwenda kufundisha na kuhubiri katika miji yao.
2 Naye Yohana aliposikia huko gerezani matendo
yake Kristo, alituma wanafunzi wake, kumwuliza,
3 Wewe ndiwe yule ajaye, au tumtazamie mwingine?
4 Yesu akajibu akawaambia, Nendeni mkamweleze
Yohana mnayoyasikia na kuyaona;
5 vipofu wanapata kuona, viwete wanakwenda, wenye
ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, na maskini wanahubiriwa
habari njema.
6 Naye heri awaye yote asiyechukizwa nami.
7 Na hao walipokwenda zao, Yesu alianza kuwaambia
makutano habari za Yohana, Mlitoka kwenda nyikani kutazama nini? Unyasi
ukitikiswa na upepo?
8 Lakini mlitoka kwenda kuona nini? Mtu aliyevikwa
mavazi mororo? Tazama, watu wavaao mavazi mororo wamo katika nyumba za wafalme.
9 Lakini kwa nini mlitoka? Ni kuona nabii? Naam,
nawaambia, na aliye mkuu zaidi ya nabii.
10 Huyo ndiye aliyeandikiwa haya, Tazama, mimi
namtuma mjumbe wangu Mbele ya uso wako, Atakayeitengeneza njia yako mbele yako.
11 Amin, nawaambieni, Hajaondokea mtu katika wazao
wa wanawake aliye mkuu kuliko Yohana Mbatizaji; walakini aliye mdogo katika
ufalme wa mbinguni ni mkuu kuliko yeye.
12 Tangu siku za Yohana Mbatizaji hata sasa ufalme
wa mbinguni hupatikana kwa nguvu, nao wenye nguvu wauteka.
13 Kwa maana manabii wote na torati walitabiri
mpaka wakati wa Yohana.
14 Na ikiwa mnataka kukubali, yeye ndiye Eliya
atakayekuja.
15 Mwenye masikio, na asikie.
16 Lakini nitakifananisha na nini kizazi hiki?
Kimefanana na watoto wanaokaa sokoni, wanaowaita wenzao, wakisema,
17 Tuliwapigia filimbi, wala hamkucheza;
tuliomboleza, wala hamkulia.
18 Maana Yohana alikuja, hali wala hanywi, wakasema,
Yuna pepo.
19 Mwana wa Adamu alikuja, akila na kunywa,
wakasema, Mlafi huyu, na mlevi, rafiki yao watoza ushuru na wenye dhambi! Na
hekima imejulikana kuwa ina haki kwa kazi zake.
20 Ndipo akaanza kuikemea miji ile ambamo ndani
yake ilifanyika miujiza yake iliyo mingi, kwa sababu haikutubu.
21 Ole wako, Korazini! Ole wako, Bethsaida! Kwa
kuwa kama miujiza iliyofanyika kwenu ingalifanyika katika Tiro na Sidoni,
wangalitubu zamani kwa kuvaa magunia na majivu.
22 Walakini nawaambieni, itakuwa rahisi Tiro na
Sidoni kustahimili adhabu zao siku ya hukumu kuliko ninyi.
23 Nawe Kapernaumu, je! Utakuzwa mpaka mbinguni?
Utashushwa mpaka kuzimu; kwa kuwa kama miujiza iliyofanyika kwako ingalifanyika
katika Sodoma, ungalikuwapo mji huo hata leo.
24 Walakini nawaambieni, itakuwa rahisi nchi ya
Sodoma kustahimili adhabu yake siku ya hukumu kuliko wewe.
25 Wakati ule Yesu akajibu, akasema, Nakushukuru,
Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na
akili, ukawafunulia watoto wachanga.
26 Naam, Baba, kwa kuwa ndivyo ilivyopendeza mbele
zako.
27 Akasema, Nimekabidhiwa vyote na baba yangu; wala
hakuna amjuaye Mwana, ila Baba; wala hakuna amjuaye Baba, ila Mwana, na ye yote
ambaye Mwana apenda kumfunulia.
28 Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye
kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.
29 Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa
mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu;
30 kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni
mwepesi.