1 Saa ile wanafunzi wakamwendea Yesu wakisema,
2 Ni nani basi aliye mkuu katika ufalme wa
mbinguni? Akaita mtoto mmoja, akamweka katikati yao,
3 akasema, Amin, nawaambia, Msipoongoka na kuwa
kama vitoto, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni.
4 Basi, ye yote ajinyenyekeshaye mwenyewe kama
mtoto huyu, huyo ndiye aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni.
5 Na ye yote atakayempokea mtoto mmoja mfano wa
huyu kwa jina langu, anipokea mimi;
6 bali atakayemkosesha mmojawapo wa wadogo hawa
waniaminio, yamfaa afungiwe shingoni jiwe kubwa la kusagia, na kutoswa katika
kilindi cha bahari.
7 Ole ni wa ulimwengu kwa sababu ya mambo ya
kukosesha! Maana hayana budi kuja mambo ya kukosesha; lakini ole wake mtu yule
aliletaye jambo la kukosesha!
8 Basi mkono wako au mguu wako ukikukosesha, ukate
ukautupe mbali nawe; ni afadhali kuingia katika uzima hali umepungukiwa na
mkono au mguu, kuliko kuwa na mikono miwili au miguu miwili, na kutupwa katika
moto wa milele.
9 Na jicho lako likikukosesha, ling'oe, ukalitupe
mbali nawe; ni afadhali kuingia katika uzima una chongo, kuliko kuwa na macho
mawili, na kutupwa katika jehanum ya moto.
10 Angalieni msidharau mmojawapo wadogo hawa; kwa
maana nawaambia ya kwamba malaika wao mbinguni siku zote huutazama uso wa Baba
yangu aliye mbinguni.
11 [Kwa maana Mwana wa Adamu alikuja kukiokoa
kilichopotea.]
12 Mwaonaje? Mtu akiwa na kondoo mia, mmoja
akampotea, je! Hawaachi wale tisa na tisini, akaenda milimani, na kumtafuta
yule aliyepotea?
13 Hata akipata kumwona, amin, nawaambia, amfurahia
huyo zaidi, kuliko wale tisa na tisini wasiopotea.
14 Vivyo hivyo haipendezi mbele za Baba yenu aliye
mbinguni kwamba mmoja wa wadogo hawa apotee.
15 Na ndugu yako akikukosa, enenda ukamwonye, wewe
na yeye peke yenu; akikusikia, umempata nduguyo.
16 La, kama hasikii, chukua pamoja nawe tena mtu
mmoja au wawili, ili kwa vinywa vya mashahidi wawili au watatu kila neno
lithibitike.
17 Na asipowasikiliza wao, liambie kanisa; na
asipolisikiliza kanisa pia, na awe kwako kama mtu wa mataifa na mtoza ushuru.
18 Amin, nawaambieni, yo yote mtakayoyafunga
duniani yatakuwa yamefungwa mbinguni; na yo yote mtakayoyafungua duniani
yatakuwa yamefunguliwa mbinguni.
19 Tena nawaambia, ya kwamba wawili wenu
watakapopatana duniani katika jambo lo lote watakaloliomba, watafanyiwa na Baba
yangu aliye mbinguni.
20 Kwa kuwa walipo wawili watatu wamekusanyika kwa
jina langu, nami nipo papo hapo katikati yao.
21 Kisha Petro akamwendea akamwambia, Bwana, ndugu
yangu anikose mara ngapi nami nimsamehe? Hata mara saba?
22 Yesu akamwambia, Sikuambii hata mara saba, bali
hata saba mara sabini.
23 Kwa sababu hii ufalme wa mbinguni umefanana na
mfalme mmoja aliyetaka kufanya hesabu na watumwa wake.
24 Alipoanza kuifanya, aliletewa mtu mmoja awiwaye
talanta elfu kumi.
25 Naye alipokosa cha kulipa, bwana wake akaamuru
auzwe, yeye na mkewe na watoto wake, na vitu vyote alivyo navyo, ikalipwe ile
deni.
26 Basi yule mtumwa akaanguka, akamsujudia akisema,
Bwana, nivumilie, nami nitakulipa yote pia.
27 Bwana wa mtumwa yule akamhurumia, akamfungua,
akamsamehe ile deni.
28 Mtumwa yule akatoka, akamwona mmoja wa wajoli
wake, aliyemwia dinari mia akamkamata,akamshika koo,akisema Nilipe uwiwacho.
29 Basi mjoli wake akaanguka miguuni pake,
akamsihi, akisema, Nivumilie, nami nitakulipa yote pia.
30 Lakini hakutaka, akaenda, akamtupa kifungoni,
hata atakapoilipa ile deni.
31 Basi wajoli wake walipoyaona yaliyotendeka,
walisikitika sana, wakaenda wakamweleza bwana wao yote yaliyotendeka.
32 Ndipo bwana wake akamwita, akamwambia, Ewe
mtumwa mwovu, nalikusamehe wewe deni ile yote, uliponisihi;
33 nawe, je! Haikukupasa kumrehemu mjoli wako, kama
mimi nilivyokurehemu wewe?
34 Bwana wake akaghadhibika, akampeleka kwa
watesaji, hata atakapoilipa deni ile yote.
35 Ndivyo na Baba yangu wa mbinguni atakavyowatenda
ninyi, msiposamehe kwa mioyo yenu kila mtu ndugu yake.