1 Ikawa Yesu alipomaliza maneno hayo, akatoka
Galilaya akafika mipaka ya Uyahudi, ng'ambo ya Yordani.
2 Makutano mengi wakamfuata, akawaponya huko.
3 Basi Mafarisayo wakamwendea, wakamjaribu,
wakimwambia, Je! Ni halali mtu kumwacha mkewe kwa kila sababu?
4 Akajibu, akawaambia, Hamkusoma ya kwamba yeye
aliyewaumba mwanzo, aliwaumba mtu mume na mtu mke,
5 akasema, Kwa sababu hiyo, mtu atamwacha babaye
na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja?
6 Hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja.
Basi aliowaunganisha Mungu, mwanadamu asiwatenganishe.
7 Wakamwambia, Jinsi gani basi Musa aliamuru kumpa
hati ya talaka, na kumwacha?
8 Akawaambia, Musa, kwa sababu ya ugumu wa mioyo
yenu, aliwapa ruhusa kuwaacha wake zenu; lakini tangu mwanzo haikuwa hivi.
9 Nami nawaambia ninyi, Kila mtu atakayemwacha
mkewe, isipokuwa ni kwa sababu ya uasherati, akaoa mwingine, azini; naye
amwoaye yule aliyeachwa azini.
10 Wanafunzi wake wakamwambia, Mambo ya mtu na
mkewe yakiwa hivyo, haifai kuoa.
11 Lakini yeye akawaambia, Si wote wawezao
kulipokea neno hili, ila wale waliojaliwa.
12 Maana wako matowashi waliozaliwa hali hiyo toka
matumboni mwa mama zao; tena wako matowashi waliofanywa na watu kuwa matowashi;
tena wako matowashi waliojifanya kuwa matowashi kwa ajili ya ufalme wa
mbinguni. Awezaye kulipokea neno hili, na alipokee.
13 Ndipo akaletewa watoto wadogo ili aweke mikono
yake juu yao na kuwaombea; wanafunzi wake wakawakemea.
14 Lakini Yesu akasema, Waacheni watoto wadogo waje
kwangu; wala msiwazuie; kwa maana walio mfano wa hao, ufalme wa mbinguni ni
wao.
15 Akaweka mikono yake juu yao, akatoka huko.
16 Na tazama, mtu mmoja akamwendea akamwambia,
Mwalimu, nitende jambo gani jema, ili nipate uzima wa milele?
17 Akamwambia Kwani kuniuliza habari ya wema? Aliye
mwema ni mmoja. Lakini ukitaka kuingia katika uzima, zishike amri.
18 Akamwambia, Zipi? Yesu akasema, Ni hizi, Usiue,
Usizini, Usiibe, Usishuhudie uongo,
19 Waheshimu baba yako na mama yako, na, Mpende
jirani yako kama nafsi yako.
20 Yule kijana akamwambia, Haya yote nimeyashika;
nimepungukiwa na nini tena?
21 Yesu akamwambia, Ukitaka kuwa mkamilifu, enenda
ukauze ulivyo navyo, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha njoo
unifuate.
22 Yule kijana alipolisikia neno lile, akaenda zake
kwa huzuni; kwa sababu alikuwa na mali nyingi.
23 Yesu akawaambia wanafunzi wake, Amin,
nawaambieni, ya kwamba itakuwa shida tajiri kuingia katika ufalme wa mbinguni.
24 Nawaambia tena, Ni rahisi zaidi ngamia kupenya
tundu ya sindano, kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu.
25 Wanafunzi waliposikia, walishangaa mno,
wakisema, Ni nani basi awezaye kuokoka?
26 Yesu akawakazia macho, akawaambia, Kwa wanadamu
hilo haliwezekani; bali kwa Mungu yote yawezekana.
27 Ndipo Petro akajibu, akamwambia, Tazama, sisi
tumeacha vyote tukakufuata; tutapata nini basi?
28 Yesu akawaambia, Amin, nawaambia ya kwamba ninyi
mlionifuata mimi, katika ulimwengu mpya, atakapoketi Mwana wa Adamu katika kiti
cha utukufu wake, ninyi nanyi mtaketi katika viti kumi na viwili, mkiwahukumu
kabila kumi na mbili za Israeli.
29 Na kila mtu aliyeacha nyumba, au ndugu wa kiume
au wa kike, au baba, au mama, au watoto, au mashamba, kwa ajili ya jina langu,
atapokea mara mia, na kuurithi uzima wa milele.
30 Lakini wengi walio wa kwanza watakuwa wa mwisho,
na walio wa mwisho watakuwa wa kwanza.