1 Siku
zile amri ilitoka kwa Kaisari Augusto ya kwamba iandikwe orodha ya majina ya watu
wote wa ulimwengu.
2 Orodha
hii ndiyo ya kwanza iliyoandikwa hapo Kirenio alipokuwa liwali wa Shamu.
3 Watu
wote wakaenda kuandikwa, kila mtu mjini kwao.
4 Yusufu
naye aliondoka Galilaya, toka mji wa Nazareti, akapanda kwenda Uyahudi mpaka
mji wa Daudi, uitwao Bethlehemu, kwa kuwa yeye ni wa mbari na jamaa ya Daudi;
5 ili
aandikwe pamoja na Mariamu mkewe, ambaye amemposa, naye ana mimba.
6 Ikawa,
katika kukaa huko, siku zake za kuzaa zikatimia,
7 akamzaa
mwanawe, kifungua mimba, akamvika nguo za kitoto, akamlaza katika hori ya kulia
ng'ombe, kwa sababu hawakupata nafasi katika nyumba ya wageni.
8 Na
katika nchi ile ile walikuwako wachungaji wakikaa makondeni na kulinda kundi
lao kwa zamu usiku.
9 Malaika
wa Bwana akawatokea ghafula, utukufu wa Bwana ukawang'aria pande zote,
wakaingiwa na hofu kuu.
10 Malaika
akawaambia, Msiogope; kwa kuwa mimi ninawaletea habari njema ya furaha kuu
itakayokuwa kwa watu wote;
11 maana
leo katika mji wa Daudi amezaliwa, kwa ajili yenu, Mwokozi, ndiye Kristo Bwana.
12 Na
hii ndiyo ishara kwenu; mtamkuta mtoto mchanga amevikwa nguo za kitoto, amelala
katika hori ya kulia ng'ombe.
13 Mara
walikuwapo pamoja na huyo malaika, wingi wa jeshi la mbinguni, wakimsifu Mungu,
na kusema,
14 Atukuzwe
Mungu juu mbinguni, Na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia.
15 Ikawa,
malaika hao walipoondoka kwenda zao mbinguni, wale wachungaji waliambiana,
Haya, na twendeni mpaka Bethlehemu, tukalione hilo lililofanyika,
alilotujulisha Bwana.
16 Wakaenda
kwa haraka wakamkuta Mariamu na Yusufu, na yule mtoto mchanga amelala horini.
17 Walipomwona
wakatoa habari waliyoambiwa juu ya huyo mtoto.
18 Wote
waliosikia wakastaajabu kwa hayo waliyoambiwa na wachungaji.
19 Lakini
Mariamu akayaweka maneno hayo yote, akiyafikiri moyoni mwake.
20 Wale
wachungaji wakarudi, huku wanamtukuza Mungu na kumsifu kwa mambo yote
waliyosikia na kuyaona, kama walivyoambiwa.
21 Hata
zilipotumia siku nane za kumtahiri, aliitwa jina lake Yesu; kama alivyoitwa na
malaika kabla hajachukuliwa mimba.
22 Kisha,
zilipotimia siku za kutakasika kwao, kama ilivyo torati ya Musa walikwenda naye
hata Yerusalemu, wamweke kwa Bwana,
23 (kama
ilivyoandikwa katika sheria ya Bwana, Kila mtoto mwanamume aliye kifungua mimba
ya mamaye na aitwe mtakatifu kwa Bwana),
24 wakatoe
na sadaka, kama ilivyonenwa katika sheria ya Bwana, Hua wawili au makinda ya
njiwa wawili.
25 Na
tazama, pale Yerusalemu palikuwa na mtu, jina lake Simeoni, naye ni mtu mwenye
haki, mcha Mungu, akiitarajia faraja ya Israeli; na Roho Mtakatifu alikuwa juu
yake.
26 Naye
alikuwa ameonywa na Roho Mtakatifu ya kwamba hataona mauti kabla ya kumwona
Kristo wa Bwana.
27 Basi
akaja hekaluni ameongozwa na Roho; na wale wazazi walipomleta mtoto Yesu ndani,
ili wamfanyie kama ilivyokuwa desturi ya sheria,
28 yeye
mwenyewe alimpokea mikononi mwake, akamshukuru Mungu, akisema,
29 Sasa,
Bwana, wamruhusu mtumishi wako, Kwa amani, kama ulivyosema;
30 Kwa
kuwa macho yangu yameuona wokovu wako,
31 Uliouweka
tayari machoni pa watu wote;
32 Nuru
ya kuwa mwangaza wa Mataifa, Na kuwa utukufu wa watu wako Israeli.
33 Na
babaye na mamaye walikuwa wakiyastaajabia hayo yaliyonenwa juu yake.
34 Simeoni
akawabariki, akamwambia Mariamu mama yake, Tazama, huyu amewekwa kwa kuanguka
na kuinuka wengi walio katika Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa.
35 Nawe
mwenyewe, upanga utaingia moyoni mwako, ili yafunuliwe mawazo ya mioyo mingi.
36 Palikuwa
na nabii mke, jina lake Ana, binti Fanueli, wa kabila ya Asheri, na umri wake
ulikuwa miaka mingi, alikuwa amekaa na mume miaka saba baada ya uanawali wake.
37 Naye
ni mjane wa miaka themanini na minne; haondoki katika hekalu, ila huabudu usiku
na mchana kwa kufunga na kuomba.
38 Huyu
alitokea saa ile ile akamshukuru Mungu, na wote waliokuwa wakiutarajia ukombozi
katika Yerusalemu akawatolea habari zake.
39 Basi,
walipokwisha kuyatimiza yote kama yalivyoagizwa katika sheria ya Bwana,
walirejea Galilaya mpaka mjini kwao, Nazareti.
40 Yule
mtoto akakua, akaongezeka nguvu, amejaa hekima, na neema ya Mungu ilikuwa juu
yake.
41 Basi,
wazee wake huenda Yerusalemu kila mwaka, wakati wa sikukuu ya Pasaka.
42 Na
alipopata umri wake miaka kumi na miwili, walipanda kama ilivyokuwa desturi ya
sikukuu;
43 na
walipokwisha kuzitimiza siku, wakati wa kurudi kwao, yule mtoto Yesu alibaki
nyuma huko Yerusalemu, na wazee wake walikuwa hawana habari.
44 Nao
wakadhani ya kuwa yumo katika msafara; wakaenenda mwendo wa kutwa, wakawa
wakimtafuta katika jamaa zao na wenzao;
45 na
walipomkosa, wakarejea Yerusalemu, huku wakimtafuta.
46 Ikawa
baada ya siku tatu wakamwona hekaluni, ameketi katikati ya waalimu,
akiwasikiliza na kuwauliza maswali.
47 Nao
wote waliomsikia walistaajabia fahamu zake na majibu yake.
48 Na
walipomwona walishangaa, na mama yake akamwambia, Mwanangu, mbona umetutenda
hivi? Tazama, baba yako na mimi tulikuwa tukikutafuta kwa huzuni.
49 Akawaambia,
Kwani kunitafuta? Hamkujua ya kuwa imenipasa kuwamo katika nyumba ya Baba
yangu?
50 Nao
hawakuelewa na neno hilo alilowaambia.
51 Akashuka
pamoja nao mpaka Nazareti, naye alikuwa akiwatii; na mamaye aliyaweka hayo yote
moyoni mwake.
52 Naye
Yesu akazidi kuendelea katika hekima na kimo, akimpendeza Mungu na wanadamu.