1 Mwaka
wa kumi na tano wa kutawala kwake Kaisari Tiberio, Pontio Pilato alipokuwa
liwali wa Uyahudi, na Herode mfalme wa Galilaya, na Filipo, ndugu yake, mfalme
wa Iturea na nchi ya Trakoniti, na Lisania mfalme wa Abilene,
2 wakati
wa ukuhani mkuu wa Anasi na Kayafa, neno la Mungu lilimfikia Yohana, mwana wa
Zakaria, jangwani.
3 Akafika
nchi yote iliyo karibu na Yordani, akihubiri ubatizo wa toba liletalo ondoleo
la dhambi,
4 kama
ilivyoandikwa katika chuo cha maneno ya nabii Isaya; Sauti ya mtu aliaye
nyikani, Itengenezeni njia ya Bwana, Yanyosheni mapito yake.
5 Kila
bonde litajazwa, Na kila mlima na kilima kitashushwa; Palipopotoka patakuwa
pamenyoka, Na palipoparuza patalainishwa;
6 Na
wote wenye mwili watauona wokovu wa Mungu.
7 Basi,
aliwaambia makutano ya wale waliomwendea ili awabatize, Enyi wazao wa nyoka, ni
nani aliyewaonya ninyi kuikimbia hasira itakayokuja?
8 Basi,
toeni matunda yapatanayo na toba; wala msianze kusema mioyoni mwenu, Tunaye
baba, ndiye Ibrahimu; kwa maana nawaambia ya kwamba katika mawe haya Mungu
aweza kumwinulia Ibrahimu watoto.
9 Na
sasa hivi shoka limekwisha kuwekwa penye mashina ya miti; basi kila mti usiozaa
matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni.
10 Makutano
wakamwuliza, Tufanye nini basi?
11 Akawajibu
akiwaambia, Mwenye kanzu mbili na ampe asiye na kanzu; na mwenye vyakula na
afanye vivyo hivyo.
12 Watoza
ushuru nao wakaja kubatizwa, wakamwuliza, Mwalimu, tufanye nini sisi?
13 Akawaambia,
Msitoze kitu zaidi kuliko mlivyoamriwa.
14 Askari
nao wakamwuliza, wakisema, Sisi nasi tufanye nini? Akawaambia, Msidhulumu mtu,
wala msishitaki kwa uongo; tena mtoshewe na mshahara wenu.
15 Basi,
watu walipokuwa wakingoja yatakayotokea, wote wakiwaza-waza mioyoni mwao habari
za Yohana, kama labda yeye ndiye Kristo,
16 Yohana
alijibu akawaambia wote, Kweli mimi nawabatiza kwa maji; lakini yuaja mtu
mwenye nguvu kuliko mimi, ambaye mimi sistahili kuilegeza gidamu ya viatu
vyake; yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto;
17 ambaye
pepeo lake li mkononi mwake, naye atausafisha sana uwanda wake, na kuikusanya
ngano ghalani mwake, bali makapi atayateketeza kwa moto usiozimika.
18 Basi,
kwa maonyo mengine mengi aliwahubiri watu.
19 Lakini
mfalme Herode alipokaripiwa na yeye kwa ajili ya Herodia, mke wa nduguye, na
maovu yote aliyoyafanya Herode,
20 aliongeza
na hili juu ya yote, alimfunga Yohana gerezani.
21 Ikawa,
watu wote walipokwisha kubatizwa, na Yesu naye amebatizwa, naye anaomba, mbingu
zilifunuka;
22 Roho
Mtakatifu akashuka juu yake kwa mfano wa kiwiliwili, kama hua; sauti ikatoka
mbinguni, Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe.
23 Na
Yesu mwenyewe, alipoanza kufundisha, alikuwa amepata umri wake kama miaka
thelathini, akidhaniwa kuwa ni mwana wa Yusufu, wa Eli,
24 wa
Mathati, wa Lawi, wa Melki, wa Yana, wa Yusufu,
25 wa
Matathia, wa Amosi, wa Nahumu, wa Esli, wa Nagai,
26 wa
Maathi, wa Matathia, wa Semei, wa Yusufu, wa Yuda,
27 wa
Yoana, wa Resa, wa Zerubabeli, wa Shealtieli, wa Neri,
28 wa
Melki, wa Adi, wa Kosamu, wa Elmadamu, wa Eri,
29 wa
Yoshua, wa Eliezeri, wa Yorimu, wa Mathati, wa Lawi,
30 wa
Simeoni, wa Yuda, wa Yusufu, wa Yonamu, wa Eliakimu,
31 wa
Melea, wa Mena, wa Matatha, wa Nathani, wa Daudi,
32 wa
Yese, wa Obedi, wa Boazi, wa Salmoni, wa Nashoni,
33 wa
Aminadabu, wa Aramu, wa Hesroni, wa Peresi, wa Yuda,
34 wa
Yakobo, wa Isaka, wa Ibrahimu, wa Tera, wa Nahori,
35 wa
Serugi, wa Ragau, wa Pelegi, wa Eberi, wa Sala,
36 wa
Kenani, wa Arfaksadi, wa Shemu, wa Nuhu, wa Lameki,
37 wa
Methusela, wa Henoko, wa Yaredi, wa Mahalaleli, wa Kenani,
38 wa
Enoshi, wa Sethi, wa Adamu, wa Mungu.