1 Ikawa
siku moja, alipokuwa akiwafundisha watu hekaluni, na kuihubiri habari njema,
wakuu wa makuhani na waandishi pamoja na wazee walimtokea ghafula;
2 wakamwambia,
wakisema, Tuambie, unatenda mambo hayo kwa mamlaka gani? Tena, ni nani
aliyekupa mamlaka hii?
3 Akajibu
akawaambia, Nami nitawauliza ninyi neno moja; niambieni,
4 Ubatizo
wa Yohana, je! Ulitoka mbinguni au kwa wanadamu?
5 Wakahojiana
wao kwa wao, wakisema, Kama tukisema ulitoka mbinguni, atasema, Basi, mbona
hamkumwamini?
6 Na
tukisema ulitoka kwa wanadamu, watu wote watatupiga kwa mawe, kwa kuwa
wamemkubali Yohana kuwa ni nabii.
7 Wakajibu,
kwamba, Hatujui ulikotoka.
8 Yesu
akawaambia, Wala mimi siwaambii ninyi ni kwa mamlaka gani ninatenda mambo haya.
9 Akaanza
kuwaambia watu mfano huu; Mtu mmoja alipanda shamba la mizabibu; akapangisha
wakulima, akaenda akakaa katika nchi nyingine muda mrefu.
10 Na
wakati wa mavuno alituma mtumwa kwa wale wakulima ili wampe baadhi ya matunda
ya mizabibu; wakulima wakampiga wakamfukuza mikono mitupu.
11 Akatuma
na mtumwa mwingine. Wakampiga huyu naye, wakamwaibisha wakamfukuza mikono mitupu.
12 Akamtuma
na wa tatu; huyu naye wakamtia jeraha, wakamtupa nje.
13 Basi,
bwana wa shamba la mizabibu alisema, Nifanyeje? Nitamtuma mwanangu, mpendwa
wangu; yamkini watamheshimu yeye.
14 Lakini,
wale wakulima walipomwona, walishauriana wao kwa wao, wakisema, Huyu ndiye
mrithi; haya, na tumwue, ili urithi uwe wetu.
15 Wakamtupa
nje ya shamba la mizabibu, wakamwua. Basi, bwana wa shamba la mizabibu
atawatendeje?
16 Atakuja
na kuwaangamiza wakulima wale, na lile shamba la mizabibu atawapa wengine. Waliposikia
hayo walisema, Hasha! Yasitukie haya!
17 Akawakazia
macho akasema, Maana yake nini basi neno hili lililoandikwa, Jiwe walilolikataa
waashi, Hilo limekuwa jiwe kuu la pembeni?
18 Kila
mtu aangukaye juu ya jiwe hilo atavunjika-vunjika; na ye yote ambaye
litamwangukia litamsaga kabisa.
19 Nao
waandishi na wakuu wa makuhani walitafuta kumkamata saa iyo hiyo, wakawaogopa
watu, maana walitambua ya kwamba mfano huu amewanenea wao.
20 Wakamvizia-vizia,
wakatuma wapelelezi waliojifanya kuwa watu wa haki, ili wamnase katika maneno
yake, wapate kumtia katika enzi na mamlaka ya liwali.
21 Wakamwuliza,
wakisema, Mwalimu, twajua ya kwamba wasema na kufundisha yaliyo ya haki, wala
hujali cheo cha mtu, bali unafundisha njia ya Mungu kwa kweli.
22 Je!
Ni halali tumpe Kaisari kodi, au sivyo?
23 Lakini
yeye alitambua hila yao, akawaambia,
24 Nionyesheni
dinari. Ina sura na anwani ya nani? Wakamjibu, Ya Kaisari.
25 Akawaambia,
Basi, vya Kaisari mpeni Kaisari, na vya Mungu mpeni Mungu.
26 Wala
hawakuweza kumshitaki kwa maneno yake mbele ya watu; wakastaajabia majibu yake,
wakanyamaa.
27 Kisha
baadhi ya Masadukayo wakamwendea, wale wasemao ya kwamba hakuna ufufuo,
wakamwuliza,
28 wakisema,
Mwalimu, Musa alituandikia ya kuwa, mtu akifiwa na ndugu yake mwenye mke,
lakini hana mtoto na amtwae huyu mke, ampatie ndugu yake mzao.
29 Basi,
kulikuwa na ndugu saba. Wa kwanza alioa mke, akafa hana mtoto;
30 na
wa pili [akamtwaa yule mke, akafa hana mtoto;]
31 hata
wa tatu akamwoa, na kadhalika wote saba, wakafa, wasiache watoto.
32 Mwisho
akafa yule mke naye.
33 Basi,
katika ufufuo atakuwa mke wa yupi? Maana aliolewa na wote saba.
34 Yesu
akawaambia, Wana wa ulimwengu huu huoa na kuolewa;
35 lakini,
wale wahesabiwao kuwa wamestahili kuupata ulimwengu ule, na kule kufufuka
katika wafu, hawaoi wala hawaolewi;
36 wala
hawawezi kufa tena; kwa sababu huwa sawasawa na malaika, nao ni wana wa Mungu,
kwa vile walivyo wana wa ufufuo.
37 Lakini,
ya kuwa wafu hufufuliwa, hata na Musa alionyesha katika sura ya Kijiti, hapo alipomtaja
Bwana kuwa ni Mungu wa Ibrahimu, na Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo.
38 Naye
si Mungu wa wafu, bali wa walio hai; kwa kuwa wote huishi kwake.
39 Waandishi
wengine wakajibu wakamwambia, Mwalimu, umesema vema;
40 wala
hawakuthubutu kumwuliza neno baada ya hayo.
41 Akawaambia,
Wasemaje watu kwamba Kristo ni Mwana wa Daudi?
42 Maana,
Daudi mwenyewe asema katika chuo cha Zaburi, Bwana alimwambia Bwana wangu,
Uketi mkono wangu wa kuume,
43 Hata
niwaweke adui zako Kuwa kiti cha kuwekea miguu yako.
44 Basi
Daudi amwita Bwana; amekuwaje mwana wake?
45 Na
watu wote walipokuwa wakimsikiliza, aliwaambia wanafunzi wake,
46 Jilindeni
na waandishi, wapendao kutembea wamevaa mavazi marefu, na kusalimiwa masokoni,
na kuketi mbele katika masinagogi, na viti vya mbele karamuni.
47 Wanakula
nyumba za wajane, na kwa unafiki husali sala ndefu. Hao watapata hukumu iliyo
kuu.