1 Naye
alipoingia Yeriko alipita katikati yake.
2 Na
tazama, palikuwa na mtu, jina lake Zakayo, mkubwa mmoja katika watoza ushuru,
naye ni tajiri.
3 Huyu
alikuwa akitafuta kumwona Yesu ni mtu wa namna gani, asiweze kwa sababu ya
umati wa watu, maana ni mfupi wa kimo.
4 Akatangulia
mbio, akapanda juu ya mkuyu apate kumwona, kwa kuwa atakuja kuipitia njia ile.
5 Na
Yesu, alipofika mahali pale, alitazama juu, akamwambia, Zakayo, shuka upesi,
kwa kuwa leo imenipasa kushinda nyumbani mwako.
6 Akafanya
haraka, akashuka, akamkaribisha kwa furaha.
7 Hata
watu walipoona, walinung'unika wote, wakisema, Ameingia kukaa kwa mtu mwenye
dhambi.
8 Zakayo
akasimama, akamwambia Bwana, Tazama, Bwana, nusu ya mali yangu nawapa maskini,
na ikiwa nimenyang'anya mtu kitu kwa hila namrudishia mara nne.
9 Yesu
akamwambia, Leo wokovu umefika nyumbani humu, kwa sababu huyu naye ni mwana wa
Ibrahimu.
10 Kwa
kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea.
11 Waliposikia
hayo, aliongeza kusema mfano, kwa sababu alikuwa karibu na Yerusalemu, na wao
walidhani ya kuwa ufalme wa Mungu utaonekana mara.
12 Basi
akasema, Mtu mmoja, kabaila, alisafiri kwenda nchi ya mbali, ili ajipatie
ufalme na kurudi.
13 Akaita
watu kumi katika watumwa wake, akawapa mafungu kumi ya fedha, akawaambia,
Fanyeni biashara hata nitakapokuja.
14 Lakini
watu wa mji wake walimchukia, wakatuma wajumbe kumfuata na kusema, Hatumtaki
huyu atutawale.
15 Ikawa
aliporudi, ameupata ufalme wake, aliamuru waitwe wale watumwa aliowapa fedha,
ili ajue faida aliyopata kila mtu kwa biashara yake.
16 Akaja
wa kwanza, akasema, Bwana, fungu lako limeleta faida ya mafungu kumi zaidi.
17 Akamwambia,
Vema, mtumwa mwema; kwa vile ulivyokuwa mwaminifu katika neno lililo dogo, uwe
na mamlaka juu ya miji kumi.
18 Akaja
wa pili, akasema, Bwana, fungu lako limeleta mafungu matano faida.
19 Akamwambia
huyu naye, Wewe uwe juu ya miji mitano.
20 Akaja
mwingine akasema, Bwana, hili ndilo fungu lako, ambalo nililiweka akiba katika
leso.
21 Kwa
maana nilikuogopa kwa kuwa u mtu mgumu; waondoa usichoweka, wavuna usichopanda.
22 Akamwambia,
Nitakuhukumu kwa kinywa chako, mtumwa mwovu wewe. Ulinijua kuwa ni mtu mgumu,
niondoaye nisichoweka, na kuvuna nisichopanda;
23 basi,
mbona hukuiweka fedha yangu kwa watoao riba, ili nijapo niipate pamoja na faida
yake?
24 Akawaambia
waliosimama karibu, Mnyang'anyeni hilo fungu, mkampe yule mwenye mafungu kumi.
25 Wakamwambia,
Bwana, anayo mafungu kumi.
26 Nawaambia,
Kila aliye na kitu atapewa, bali yule asiye na kitu atanyang'anywa hata alicho
nacho.
27 Tena,
wale adui zangu, wasiotaka niwatawale, waleteni hapa mwachinje mbele yangu.
28 Na
alipokwisha kusema hayo, alitangulia mbele akipanda kwenda Yerusalemu.
29 Ikawa
alipokaribia Bethfage na Bethania, kwenye mlima uitwao wa Mizeituni, alituma
wawili katika wale wanafunzi,
30 akisema,
Nendeni mpaka kijiji kile kinachowakabili, na mtakapoingia ndani mtaona
mwana-punda, amefungwa, ambaye hajapandwa na mtu ye yote bado, mfungueni
mkamlete hapa.
31 Na
kama mtu akiwauliza, Mbona mnamfungua? Semeni hivi, Bwana anamhitaji.
32 Na
wale waliotumwa wakaenda wakaona kama alivyowaambia.
33 Na
walipokuwa wakimfungua mwana-punda, wenyewe waliwaambia, Mbona mnamfungua
mwana-punda?
34 Wakasema,
Bwana ana haja naye.
35 Wakampeleka
kwa Yesu, wakatandika nguo zao juu ya mwana-punda, wakampandisha Yesu.
36 Na
alipokuwa akienda walitandaza nguo zao njiani.
37 Hata
alipokuwa amekaribia matelemko ya mlima wa Mizeituni, kundi zima la wanafunzi
wake walianza kufurahi na kumsifu Mungu kwa sauti kuu, kwa ajili ya matendo
yote ya uwezo waliyoyaona,
38 wakasema,
Ndiye mbarikiwa Mfalme ajaye kwa jina la Bwana; amani mbinguni, na utukufu huko
juu.
39 Baadhi
ya Mafarisayo waliokuwa katika mkutano wakamwambia, Mwalimu, uwakanye wanafunzi
wako.
40 Akajibu,
akasema, Nawaambia ninyi, wakinyamaza hawa, mawe yatapiga kelele.
41 Alipofika
karibu aliuona mji, akaulilia,
42 akisema,
Laiti ungalijua, hata wewe katika siku hii, yapasayo amani! Lakini sasa
yamefichwa machoni pako.
43 Kwa
kuwa siku zitakuja, adui zako watakapokujengea boma, likuzunguke; watakuzingira
na kukuhusuru pande zote;
44 watakuangusha
chini wewe na watoto wako ndani yako, wasikuachie jiwe juu ya jiwe, kwa sababu
hukutambua majira ya kujiliwa kwako.
45 Akaingia
hekaluni, akaanza kuwatoa wale waliokuwa wakifanya biashara,
46 akiwaambia,
Imeandikwa, Nyumba yangu itakuwa nyumba ya sala; lakini ninyi mmeifanya kuwa
pango la wanyang'anyi.
47 Naye
akawa akifundisha kila siku hekaluni. Lakini wakuu wa makuhani, na waandishi, na
wakuu wa watu walikuwa wakitafuta njia ya kumwangamiza;
48 wasione
la kutenda, kwa kuwa watu wote walikuwa wakiandamana naye, wakimsikiliza.