1 Ikakaribia
sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu, iitwayo Sikukuu ya Pasaka.
2 Na
wakuu wa makuhani na waandishi walikuwa wakitafuta njia ya kumwua; maana
walikuwa wakiwaogopa watu.
3 Shetani
akamwingia Yuda, aitwaye Iskariote, naye ni mmoja wa wale Thenashara.
4 Akaondoka,
akaenda akasema na wakuu wa makuhani na majemadari, jinsi atakavyoweza kumtia
mikononi mwao.
5 Wakafurahi,
wakapatana naye kumpa fedha.
6 Akakubali,
akatafuta nafasi ya kumsaliti kwao pasipokuwapo mkutano.
7 Ikafika
siku ya mikate isiyotiwa chachu, ambayo ilipasa kuchinja pasaka.
8 Akawatuma
Petro na Yohana, akisema, Nendeni, mkatuandalie pasaka tupate kuila.
9 Wakamwambia,
Wataka tuandae wapi?
10 Akawaambia,
Tazama, mtakapoingia mjini mtakutana na mwanamume akichukua mtungi wa maji;
mfuateni mkaingie katika nyumba atakayoingia yeye.
11 Na
mtamwambia mwenye nyumba, Mwalimu akuambia, Ki wapi chumba cha wageni, nipate
kula pasaka humo pamoja na wanafunzi wangu?
12 Naye
atawaonyesha chumba kikubwa orofani, kimekwisha andikwa; andaeni humo.
13 Wakaenda,
wakaona kama alivyowaambia, wakaiandaa pasaka.
14 Hata
saa ilipofika aliketi chakulani, yeye na wale mitume pamoja naye.
15 Akawaambia,
Nimetamani sana kuila pasaka hii pamoja nanyi kabla ya kuteswa kwangu;
16 kwa
maana nawaambia ya kwamba siili tena hata itakapotimizwa katika ufalme wa
Mungu.
17 Akapokea
kikombe, akashukuru, akasema, Twaeni hiki, mgawanye ninyi kwa ninyi;
18 Maana
nawaambia ya kwamba tangu sasa sinywi mazao ya mzabibu hata ufalme wa Mungu
utakapokuja.
19 Akatwaa
mkate, akashukuru, akaumega, akawapa, akisema, [Huu ndio mwili wangu unaotolewa
kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu.
20 Kikombe
nacho vivyo hivyo baada ya kula; akisema, Kikombe hiki ni agano jipya katika
damu yangu, inayomwagika kwa ajili yenu.]
21 Walakini,
tazama, mkono wake yeye anayenisaliti upo hapa pamoja nami mezani,
22 Kwa
kuwa Mwana wa Adamu aenda zake kama ilivyokusudiwa; lakini, ole wake mtu yule
amsalitiye!
23 Wakaanza
kuulizana wao kwa wao, ni yupi miongoni mwao atakayelitenda jambo hilo.
24 Yakatokea
mashindano kati yao, kwamba ni nani anayehesabiwa kuwa mkubwa.
25 Akawaambia,
Wafalme wa Mataifa huwatawala, na wenye mamlaka juu yao huitwa Wenye fadhili;
26 lakini
kwenu ninyi sivyo; bali aliye mkubwa kwenu na awe kama aliye mdogo; na mwenye
kuongoza kama yule atumikaye.
27 Maana
aliye mkubwa ni yupi? Yeye aketiye chakulani, au yule atumikaye? Siye yule
aketiye chakulani? Lakini mimi kati yenu ni kama atumikaye.
28 Nanyi
ndinyi mliodumu pamoja nami katika majaribu yangu.
29 Nami
nawawekea ninyi ufalme, kama vile Baba yangu alivyoniwekea mimi;
30 mpate
kula na kunywa mezani pangu katika ufalme wangu; na kuketi katika viti vya
enzi, huku mkiwahukumu kabila kumi na mbili za Israeli.
31 Akasema,
Simoni, Simoni, tazama, Shetani amewataka ninyi apate kuwapepeta kama vile
ngano;
32 lakini
nimekuombea wewe ili imani yako isitindike; nawe utakapoongoka waimarishe ndugu
zako.
33 Akamwambia,
Bwana, niwapo pamoja nawe, mimi ni tayari kwenda gerezani au hata kifoni.
34 Akasema,
Nakuambia, Petro, jogoo hatawika leo, kabla wewe hujanikana mara tatu ya kuwa
hunijui.
35 Akawauliza,
Je! Hapo nilipowatuma hamna mfuko, wala mkoba, wala viatu, mlipungukiwa na
kitu? Wakasema, La!
36 Akawaambia,
Lakini sasa mwenye mfuko na auchukue, na mkoba vivyo hivyo; naye asiye na
upanga, na auze joho yake akanunue.
37 Kwa
kuwa nawaambia, hayo yaliyoandikwa hayana budi kutimizwa kwangu; ya kuwa,
Alihesabiwa pamoja na wahalifu. Kwa sababu yanipasayo yanao mwisho wake.
38 Wakasema,
Bwana, tazama, hapa pana panga mbili. Akawaambia, Basi.
39 Akatoka
akaenda mpaka mlima wa Mizeituni kama ilivyokuwa desturi yake; wanafunzi wake
nao wakafuatana naye.
40 Alipofika
mahali pale aliwaambia, Ombeni kwamba msiingie majaribuni.
41 Mwenyewe
akajitenga nao kama kiasi cha kutupa jiwe, akapiga magoti akaomba,
42 akisema,
Ee Baba, ikiwa ni mapenzi yako, uniondolee kikombe hiki; walakini si mapenzi
yangu, bali yako yatendeke.
43 Malaika
kutoka mbinguni akamtokea akamtia nguvu.
44 Naye
kwa vile alivyokuwa katika dhiki, akazidi sana kuomba; hari yake ikawa kama
matone ya damu yakidondoka nchini.]
45 Alipoondoka
katika kuomba kwake, akawajia wanafunzi wake, akawakuta wamelala usingizi kwa
huzuni.
46 Akawaambia,
Mbona mmelala usingizi? Ondokeni, mkaombe, msije mkaingia majaribuni.
47 Basi
alipokuwa katika kusema, tazama, mkutano wa watu, na yule aitwaye Yuda, ambaye
ni mmoja wa wale Thenashara, amewatangulia. Akamkaribia Yesu ili kumbusu.
48 Yesu
akamwambia, Yuda, wamsaliti Mwana wa Adamu kwa kumbusu?
49 Na
wale waliokuwa karibu naye walipoona yatakayotukia, walisema, Bwana, tuwapige
kwa upanga?
50 Mmoja
wao akampiga mtumwa wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio la kuume.
51 Yesu
akajibu akasema, Mwe radhi kwa hili. Akamgusa sikio, akamponya.
52 Yesu
akawaambia wakuu wa makuhani, na maakida wa hekalu, na wazee, waliokuja juu
yake, Je! Mmekuja wenye panga na marungu kama kukamata mnyang'anyi?
53 Kila
siku nilipokuwa pamoja nanyi hekaluni hamkuninyoshea mikono, lakini hii ndiyo
saa yenu, na mamlaka ya giza.
54 Wakamkamata,
wakamchukua, wakaenda naye nyumbani kwa Kuhani Mkuu. Na Petro alimfuata kwa
mbali.
55 Na
walipokwisha washa moto katikati ya kiwanja, waliketi pamoja, naye Petro
akaketi kati yao.
56 Ndipo
mjakazi mmoja akamwona ameketi mwangani, akamkazia macho akasema, Na huyu
alikuwa pamoja naye.
57 Akakana,
akisema, Ee mwanamke, simjui.
58 Baadaye
kitambo mtu mwingine alimwona akasema, Wewe nawe u mmoja wao. Petro akasema, Ee
mtu, si mimi.
59 Halafu,
yapata saa moja, mtu mwingine alikaza kusema, Hakika na huyu alikuwa pamoja
naye, kwa kuwa yeye pia ni Mgalilaya.
60 Petro
akasema, Ee mtu, sijui usemalo. Na papo hapo alipokuwa katika kusema, jogoo
aliwika.
61 Bwana
akageuka akamtazama Petro. Petro akalikumbuka lile neno la Bwana jinsi alivyomwambia,
Leo kabla hajawika jogoo utanikana mara tatu.
62 Akatoka
nje akalia kwa majonzi.
63 Na
wale watu waliokuwa wakimshika Yesu walimfanyia dhihaka, wakampiga.
64 Wakamfunika
macho, kisha wakamwuliza-uliza wakisema, Tabiri, ni nani aliyekupiga?
65 Wakamtolea
na maneno mengine mengi ya kumtukana.
66 Hata
kulipokucha, walikutanika jamii ya wazee, na wakuu wa makuhani, na waandishi,
wakamleta katika baraza yao, wakisema,
67 Kama
wewe ndiwe Kristo, tuambie. Akawaambia, Nijapowaambia, hamtasadiki kabisa.
68 Tena,
nikiwauliza, hamtajibu.
69 Lakini
tangu sasa Mwana wa Adamu atakuwa ameketi upande wa kuume wa Mungu Mwenyezi.
70 Wakasema
wote, Basi, wewe ndiwe Mwana wa Mungu? Akawaambia, Ninyi mwasema kwamba mimi
ndiye.
71 Wakasema,
Basi, tuna haja gani tena ya ushuhuda? Maana, sisi wenyewe tumesikia maneno ya
kinywa chake.