1 Wakasimama
mkutano wote, wakampeleka kwa Pilato.
2 Wakaanza
kumshitaki, wakisema, Tumemwona huyu akipotosha taifa letu, na kuwazuia watu
wasimpe Kaisari kodi, akisema kwamba yeye mwenyewe ni Kristo, mfalme.
3 Pilato
akamwuliza, akisema, Wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi? Akajibu akamwambia, Wewe
wasema.
4 Pilato
akawaambia wakuu wa makuhani na makutano, Sioni neno lililo ovu katika mtu
huyu.
5 Nao
walikaza sana, wakisema, Huwataharakisha watu, akifundisha katika Uyahudi yote,
tokea Galilaya mpaka huku.
6 Pilato
aliposikia hayo aliuliza kama huyu ni mtu wa Galilaya.
7 Na
alipopata habari ya kuwa yu chini ya mamlaka ya Herode, alimpeleka kwa Herode,
kwa kuwa yeye naye alikuwapo Yerusalemu siku zile.
8 Na
Herode alipomwona Yesu alifurahi sana, kwa sababu alikuwa akitaka sana kumwona
tangu siku nyingi, maana amesikia habari zake, akataraji kuona ishara
iliyofanywa na yeye.
9 Akamwuliza
maneno mengi, yeye asimjibu lo lote.
10 Wakuu
wa makuhani na waandishi wakasimama wakamshitaki kwa nguvu sana.
11 Basi
Herode akamfanya duni, pamoja na askari zake, akamdhihaki, na kumvika mavazi
mazuri; kisha akamrudisha kwa Pilato.
12 Basi
siku ile ile Herode na Pilato walipatana kwa urafiki kwa maana hapo kwanza
walikuwa na uadui wao kwa wao.
13 Na
Pilato akawakutanisha wakuu wa makuhani, na wakubwa, na watu,
14 akawaambia,
Mtu huyu mmemleta kwangu kana kwamba anapotosha watu; nami, tazama, nimeamua
mambo yake mbele yenu, ila sikuona kwake kosa lo lote katika mambo hayo
mliyomshitaki;
15 wala
hata Herode, kwa maana amemrudisha kwetu; basi tazama, hakuna neno lo lote
alilolitenda lipasalo kufa.
16 Kwa
hiyo nitamrudi, kisha nitamfungua. [
17 Maana
ilimlazimu kuwafungulia mfungwa mmoja wakati wa sikukuu.]
18 Wakapiga
kelele wote pamoja, wakisema, Mwondoe huyu, utufungulie Baraba.
19 Naye
ni mtu aliyetupwa gerezani kwa ajili ya fitina iliyotokea mjini, na kwa uuaji
20 Basi
Pilato alisema nao mara ya pili, kwa vile alivyotaka kumfungua Yesu.
21 Lakini
wakapiga kelele, wakisema, Msulibishe. Msulibishe.
22 Akawaambia
mara ya tatu, Kwa sababu gani? Huyu ametenda uovu gani? Sikuona kwake hata neno
lipasalo kufa. Basi nikiisha kumrudi nitamfungua.
23 Lakini
wakatoa sauti zao kwa nguvu sana, wakitaka asulibiwe. Sauti zao zikashinda.
24 Pilato
akahukumu kwamba haja yao ifanyike.
25 Akamfungua
yule aliyetupwa gerezani kwa ajili ya fitina na uuaji, yule waliyemtaka,
akamtoa Yesu wamfanyie watakavyo.
26 Na
walipokuwa wakimwondoa walimkamata mtu mmoja, Simoni Mkirene, aliyekuwa ametoka
shamba, wakamtwika msalaba, auchukue nyuma yake Yesu.
27 Mkutano
mkubwa wa watu wakamfuata, na wanawake waliokuwa wakijipiga vifua na
kumwombolezea.
28 Yesu
akawageukia, akasema, Enyi binti za Yerusalemu, msinililie mimi, bali jililieni
nafsi zenu na watoto wenu.
29 Kwa
maana tazama, siku zitakuja watakaposema, Heri walio tasa, na matumbo
yasiyozaa, na maziwa yasiyonyonyesha.
30 Ndipo
watakapoanza kuiambia milima, Tuangukieni, na vilima, Tufunikeni.
31 Kwa
kuwa kama wakitenda mambo haya katika mti mbichi, itakuwaje katika mkavu?
32 Wakapelekwa
na wawili wengine, wahalifu, wauawe pamoja naye.
33 Na
walipofika mahali paitwapo Fuvu la Kichwa, ndipo walipomsulibisha yeye, na wale
wahalifu, mmoja upande wa kuume, na mmoja upande wa kushoto.
34 Yesu
akasema, Baba, uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo. Wakagawa mavazi yake,
wakipiga kura.
35 Watu
wakasimama wakitazama. Wale wakuu nao walikuwa wakimfanyia mzaha, wakisema,
Aliokoa wengine; na ajiokoe mwenyewe, kama ndiye Kristo wa Mungu, mteule wake.
36 Wale
askari nao wakamfanyia dhihaka, wakimwendea na kumletea siki,
37 huku
wakisema, Kama wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi, ujiokoe mwenyewe.
38 Na
juu yake palikuwa na anwani; HUYU NDIYE MFALME WA WAYAHUDI.
39 Na
mmoja wa wale wahalifu waliotungikwa alimtukana, akisema, Je! Wewe si Kristo?
Jiokoe nafsi yako na sisi.
40 Lakini
yule wa pili akamjibu akamkemea, akisema, Wewe humwogopi hata Mungu, nawe u
katika hukumu iyo hiyo?
41 Nayo
ni haki kwetu sisi, kwa kuwa tunapokea malipo tuliyostahili kwa matendo yetu;
bali huyu hakutenda lo lote lisilofaa.
42 Kisha
akasema, Ee Yesu, nikumbuke utakapoingia katika ufalme wako.
43 Yesu
akamwambia, Amin, nakuambia, leo hivi utakuwa pamoja nami peponi.
44 Hapo
ilikuwa yapata saa sita, kukawa giza juu ya nchi yote hata saa kenda,
45 jua
limepungua nuru yake; pazia la hekalu likapasuka katikati.
46 Yesu
akalia kwa sauti kuu, akasema, Ee Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu.
47 Alipokwisha
kusema hayo alikata roho. Yule akida alipoona yaliyotukia, alimtukuza Mungu,
akisema, Hakika yake, mtu huyu alikuwa mwenye haki.
48 Na
makutano yote ya watu waliokuwa wamekutanika kutazama mambo hayo, walipoona
yaliyotendeka, wakaenda zao kwao, wakijipiga-piga vifua.
49 Na
wote waliojuana naye, na wale wanawake walioandamana naye toka Galilaya,
wakasimama kwa mbali, wakitazama mambo hayo.
50 Na
tazama, akatoka mtu mmoja, jina lake Yusufu, ambaye ni mtu wa baraza, mtu
mwema, mwenye haki;
51 (wala
hakulikubali shauri na tendo lao), naye ni mtu wa Arimathaya, mji mmoja wa
Wayahudi, tena anautazamia ufalme wa Mungu;
52 mtu
huyo alikwenda kwa Pilato, akataka kupewa mwili wa Yesu.
53 Akaushusha,
akauzinga sanda ya kitani, akauweka katika kaburi lililochongwa mwambani,
ambalo hajalazwa mtu bado ndani yake.
54 Na
siku ile ilikuwa siku ya Maandalio, na sabato ikaanza kuingia.
55 Na
wale wanawake waliokuja naye toka Galilaya walifuata, wakaliona kaburi, na
jinsi mwili wake ulivyowekwa.
56 Wakarudi,
wakafanya tayari manukato na marhamu. Na siku ya sabato walistarehe kama
ilivyoamriwa.