1 Palikuwa
na mtu Kaisaria, jina lake Kornelio, akida wa kikosi kilichoitwa Kiitalia,
2 mtu
mtauwa, mchaji wa Mungu, yeye na nyumba yake yote, naye alikuwa akiwapa watu
sadaka nyingi, na kumwomba Mungu daima.
3 Akaona
katika maono waziwazi, kama saa tisa ya mchana, malaika wa Mungu, akimjia na
kumwambia, Kornelio!
4 Akamtazama
sana, akaogopa akasema, Kuna nini, Bwana? Akamwambia, Sala zako na sadaka zako
zimefika juu na kuwa ukumbusho mbele za Mungu.
5 Sasa
basi, peleka watu Yafa, ukamwite Simoni, aitwaye Petro.
6 Yeye
ni mgeni wa mtu mmoja, jina lake Simoni, mtengenezaji wa ngozi, ambaye nyumba
yake iko pwani, atakuambia yakupasayo kutenda.
7 Na
yule malaika aliyesema naye akiisha kuondoka, Kornelio akawaita wawili katika
watumishi wake wa nyumbani, na askari mmoja, mtu mtauwa katika wale
waliomhudumia daima;
8 na
alipokwisha kuwaeleza mambo yote akawatuma kwenda Yafa.
9 Hata
siku ya pili, walipokuwa wakisafiri na kuukaribia mji, Petro alipanda juu
darini, kwenda kuomba, yapata saa sita ya mchana;
10 akaumwa
na njaa sana, akataka kula; lakini walipokuwa wakiandaa, roho yake ikazimia,
11 akaona
mbingu zimefunuka, na chombo kikishuka kama nguo kubwa, inatelemshwa kwa pembe
zake nne hata nchi;
12 ambayo
ndani yake walikuwamo aina zote za wanyama wenye miguu minne, na hao watambaao,
na ndege wa angani.
13 Kisha
sauti ikamjia, kusema, Ondoka, Petro, uchinje ule.
14 Lakini
Petro akasema, Hasha, Bwana, kwa maana sijakula kamwe kitu kilicho kichafu au
najisi.
15 Sauti
ikamjia mara ya pili, ikimwambia, Vilivyotakaswa na Mungu, usiviite wewe
najisi.
16 Jambo
hili likatendeka mara tatu; kisha kile chombo kikapokewa tena mbinguni.
17 Hata
Petro alipokuwa akiona shaka ndani ya nafsi yake, maana yake ni nini maono hayo
aliyoyaona, wale watu waliotumwa na Kornelio, wakiisha kuiulizia nyumba ya
Simoni, wakasimama mbele ya mlango,
18 wakaita;
wakauliza kwamba Simoni aitwaye Petro anakaa humo.
19 Na
Petro alikuwa akiyafikiri yale maono. Roho akamwambia, Wako watu watatu
wanakutafuta.
20 Basi
ondoka ushuke ufuatane nao, usione tashwishi, kwa maana ni mimi niliyewatuma.
21 Petro
akawashukia wale watu, akanena, Mimi ndiye mnayemtafuta. Mmekuja kwa sababu
gani?
22 Wakasema,
Kornelio akida, mtu mwenye haki, mchaji wa Mungu, aliye na sifa njema kwa taifa
lote la Wayahudi, alionywa na malaika mtakatifu kutuma watu kwako, uende
nyumbani kwake, apate kusikiliza maneno kwako.
23 Akawakaribisha
wawe wageni wake. Hata siku ya pili, Petro akaondoka akatoka pamoja nao, na baadhi
ya ndugu waliokaa Yafa wakafuatana naye.
24 Siku
ya pili yake wakaingia Kaisaria. Na Kornelio alikuwa akiwangojea, hali
amekusanya jamaa zake na rafiki zake.
25 Petro
alipokuwa akiingia Kornelio akatoka amlaki akamwangukia miguu, akamsujudia.
26 Lakini
Petro akamwinua, akasema, Simama, mimi nami ni mwanadamu.
27 Na
katika kusema naye akaingia ndani, akaona watu wengi wamekusanyika.
28 Akawaambia,
Ninyi mnajua ya kuwa si halali mtu aliye Myahudi ashikamane na mtu aliye wa
taifa lingine wala kumwendea, lakini Mungu amenionya, nisimwite mtu awaye yote
mchafu wala najisi.
29 Kwa
sababu hiyo nalikuja nilipoitwa, nisikatae; basi nawauliza, ni neno gani
mliloniitia?
30 Kornelio
akasema, Siku tatu zilizopita, katika saa ii hii, yaani saa tisa, nilikuwa nikisali
nyumbani mwangu; nikamwona mtu amesimama mbele yangu, mwenye nguo zing'arazo,
31 akasema,
Kornelio, kuomba kwako kumesikiwa, na sadaka zako zinakumbukwa mbele za Mungu.
32 Basi,
tuma watu kwenda Yafa, ukamwite Simoni aitwaye Petro, anakaa katika nyumba ya
Simoni, mtengenezaji wa ngozi, karibu na pwani; naye akija atasema nawe.
33 Mara
nikatuma watu kwako, nawe umefanya vyema kuja. Basi sasa sisi sote tupo hapa
mbele za Mungu, tupate kuyasikiliza maneno yote uliyoamriwa na Bwana.
34 Petro
akafumbua kinywa chake, akasema, Hakika natambua ya kuwa Mungu hana upendeleo;
35 bali
katika kila taifa mtu amchaye na kutenda haki hukubaliwa na yeye.
36 Neno
lile alilowapelekea wana wa Israeli akihubiri habari njema ya amani kwa Yesu
Kristo (ndiye Bwana wa wote),
37 jambo
lile ninyi mmelijua, lililoenea katika Uyahudi wote likianzia Galilaya, baada
ya ubatizo aliouhubiri Yohana;
38 habari
za Yesu wa Nazareti, jinsi Mungu alivyomtia mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu
naye akazunguka huko na huko, akitenda kazi njema na kuponya wote walioonewa na
Ibilisi; kwa maana Mungu alikuwa pamoja naye.
39 Nasi
tu mashahidi wa mambo yote aliyoyatenda katika nchi ya Wayahudi na katika
Yerusalemu; ambaye walimwua wakamtundika mtini.
40 Huyo
Mungu alimfufua siku ya tatu, akamjalia kudhihirika,
41 si
kwa watu wote, bali kwa mashahidi waliokuwa wamekwisha kuchaguliwa na Mungu,
ndio sisi, tuliokula na kunywa pamoja naye baada ya kufufuka kwake kutoka kwa
wafu.
42 Akatuagiza
tuwahubiri watu na kushuhudia ya kuwa huyu ndiye aliyeamriwa na Mungu awe
Mhukumu wa walio hai na wafu.
43 Huyo
manabii wote humshuhudia, ya kwamba kwa jina lake kila amwaminiye atapata
ondoleo la dhambi.
44 Petro
alipokuwa akisema maneno hayo Roho Mtakatifu akawashukia wote waliolisikia lile
neno.
45 Na
wale waliotahiriwa, walioamini, wakashangaa, watu wote waliokuja pamoja na
Petro, kwa sababu Mataifa nao wamemwagiwa kipawa cha Roho Mtakatifu.
46 Kwa
maana waliwasikia wakisema kwa lugha, na kumwadhimisha Mungu. Ndipo Petro
akajibu,
47 Ni
nani awezaye kuzuia maji, hawa wasibatizwe, watu waliopokea Roho Mtakatifu vile
vile kama sisi?
48 Akaamuru
wabatizwe kwa Jina lake Yesu Kristo. Ndipo wakamsihi azidi kukaa siku kadha wa
kadha.