1 Lakini
Sauli, akizidi kutisha na kuwaza kuwaua wanafunzi wa Bwana, akamwendea Kuhani
Mkuu,
2 akataka
ampe barua za kuenda Dameski zilizoandikwa kwa masinagogi, ili akiona watu wa
Njia hii, waume kwa wake, awafunge na kuwaleta Yerusalemu.
3 Hata
alipokuwa akisafiri, ikawa anakaribia Dameski; ghafula ikamwangaza kote kote
nuru kutoka mbinguni.
4 Akaanguka
chini, akasikia sauti ikimwambia, Sauli, Sauli, mbona waniudhi?
5 Akasema,
U nani wewe, Bwana? Naye akasema, Mimi ndimi Yesu unayeniudhi wewe.
6 Lakini
simama, uingie mjini, nawe utaambiwa yakupasayo kutenda.
7 Na
wale watu waliosafiri pamoja naye wakasimama kimya, wakiisikia sauti, wasione
mtu.
8 Sauli
akainuka katika nchi, na macho yake yalipofumbuka, hakuona kitu; wakamshika
mkono wakamleta mpaka Dameski.
9 Akawa
siku tatu haoni; hali, wala hanywi.
10 Basi
palikuwapo Dameski mwanafunzi jina lake Anania. Bwana akamwambia katika maono,
Anania. Akasema, Mimi hapa, Bwana.
11 Bwana
akamwambia, Simama, enenda zako katika njia iitwayo Nyofu, ukaulize katika
nyumba ya Yuda mtu aitwaye Sauli, wa Tarso; maana, angalia, anaomba;
12 naye
amemwona mtu, jina lake Anania, akiingia, na kumwekea mikono juu yake, apate
kuona tena.
13 Lakini
Anania akajibu, Bwana, nimesikia habari za mtu huyu kwa watu wengi, mabaya
mengi aliyowatenda watakatifu wako Yerusalemu;
14 hata
hapa ana amri itokayo kwa wakuu wa makuhani awafunge wote wakuitiao Jina lako.
15 Lakini
Bwana akamwambia, Nenda tu; kwa maana huyu ni chombo kiteule kwangu, alichukue
Jina langu mbele ya Mataifa, na wafalme, na wana wa Israeli.
16 Maana
nitamwonyesha yalivyo mengi yatakayompasa kuteswa kwa ajili ya Jina langu.
17 Anania
akaenda zake, akaingia mle nyumbani; akamwekea mikono akisema, Ndugu Sauli,
Bwana amenituma, Yesu, yeye aliyekutokea katika njia uliyoijia, upate kuona
tena, ukajazwe Roho Mtakatifu.
18 Mara
vikaanguka machoni pake vitu kama magamba, akapata kuona, akasimama,
akabatizwa;
19 akala
chakula, na kupata nguvu. Akawa huko siku kadha wa kadha pamoja na wanafunzi
walioko Dameski.
20 Mara
akamhubiri Yesu katika masinagogi, kwamba yeye ni Mwana wa Mungu.
21 Na
wote waliosikia wakashangaa, wakasema, Siye huyu aliyewaharibu walioliitia Jina
hili huko Yerusalemu? Na hapa alikuwa amekuja kwa kusudi hilo, awafunge na
kuwapeleka kwa wakuu wa makuhani?
22 Sauli
akazidi kuwa hodari, akawatia fadhaa Wayahudi waliokaa Dameski, akithibitisha
ya kuwa huyu ndiye Kristo.
23 Hata
siku nyingi zilipopita, Wayahudi wakafanya shauri ili wamwue;
24 lakini
hila yao ikajulikana na Sauli. Wakamvizia malangoni mchana na usiku wapate
kumwua.
25 Wanafunzi
wake wakamtwaa usiku wakamshusha ukutani, wakimtelemsha katika kapu.
26 Na
Sauli alipofika Yerusalemu, alijaribu kujiunga na wanafunzi, nao walikuwa
wakimwogopa wote, wasisadiki ya kuwa yeye ni mwanafunzi.
27 Lakini
Barnaba akamtwaa, akampeleka kwa mitume, akawaeleza jinsi alivyomwona Bwana
njiani, na ya kwamba alisema naye, na jinsi alivyohubiri kwa ushujaa katika
Dameski kwa jina la Yesu.
28 Naye
akawa pamoja nao katika Yerusalemu akiingia na kutoka.
29 Akahubiri
kwa jina la Bwana kwa ushujaa, akinena na kuhojiana na Wayahudi wa Kiyunani.
Nao wakajaribu kumwua.
30 Lakini
ndugu walipopata habari wakamchukua mpaka Kaisaria, wakampeleka aende Tarso.
31 Basi
kanisa likapata raha katika Uyahudi wote na Galilaya na Samaria, likajengwa,
likiendelea na kuongezeka katika kicho cha Bwana, na faraja ya Roho Mtakatifu.
32 Hata
Petro alipokuwa akizunguka-zunguka pande zote akawatelemkia na watakatifu
waliokaa Lida.
33 Akamwona
mtu mmoja huko, jina lake Ainea, mtu huyo amelala kitandani miaka minane; maana
alikuwa amepooza.
34 Petro
akamwambia, Ainea, Yesu Kristo akuponya; ondoka, ujitandikie. Mara akaondoka.
35 Na
watu wote waliokaa Lida na Sharoni wakamwona, wakamgeukia Bwana.
36 Na
mwanafunzi mmoja alikuwako Yafa, jina lake Tabitha, tafsiri yake ni Dorkasi
(yaani paa); mwanamke huyu alikuwa amejaa matendo mema na sadaka alizozitoa.
37 Ikawa
siku zile akaugua, akafa; hata walipokwisha kumwosha, wakamweka orofani.
38 Na
kwa kuwa mji wa Lida ulikuwa karibu na Yafa, nao wanafunzi wamesikia ya kwamba
Petro yuko huko, wakatuma watu wawili kwake, kumsihi na kusema, Usikawie kuja
kwetu.
39 Petro
akaondoka akafuatana nao. Alipofika, wakampeleka juu orofani wajane wote
wakasimama karibu naye, wakilia na kumwonyesha zile kanzu na nguo alizozishona
Dorkasi wakati ule alipokuwa pamoja nao.
40 Petro
akawatoa nje wote, akapiga magoti, akaomba, kisha akaelekea yule maiti,
akanena, Tabitha, ondoka. Naye akafumbua macho yake, na alipomwona Petro
akajiinua, akaketi.
41 Akampa
mkono, akamwinua; hata akiisha kuwaita wale watakatifu na wajane akamweka mbele
yao, hali yu hai.
42 Ikajulikana
katika mji mzima wa Yafa; watu wengi wakamwamini Bwana.
43 Basi
Petro akakaa siku kadha wa kadha huko Yafa, nyumbani mwa mtu mmoja, jina lake
Simoni, mtengenezaji wa ngozi.