1 Kuhani
Mkuu akasema, Je! Mambo hayo ndivyo yalivyo?
2 Naye
akasema, Ndugu zangu na baba zangu, sikilizeni: Mungu wa utukufu alimtokea baba
yetu Ibrahimu, alipokuwa katika Mesopotamia, kabla hajakaa Harani,
3 akamwambia,
Toka katika nchi yako na katika jamaa zako, ukaende hata nchi
nitakayokuonyesha.
4 Ndipo
alipotoka katika nchi ya Wakaldayo, akakaa Harani, akatoka huko baada ya kufa
babaye, Mungu akamhamisha mpaka nchi hii mnayokaa ninyi sasa.
5 Wala
hakumpa urithi humu hata kiasi cha kuweka mguu; akaahidi kwamba atampa, iwe
milki yake, na ya uzao wake baadaye alipokuwa hana mtoto.
6 Mungu
akanena hivi, ya kwamba wazao wake watakuwa wageni katika nchi ya watu wengine,
nao watawafanya kuwa watumwa wao, na kuwatenda mabaya kwa muda wa miaka mia
nne.
7 Na
lile taifa watakaowafanya watumwa nitawahukumu mimi, alisema Mungu; na baada ya
hayo watatoka, nao wataniabudu mahali hapa.
8 Akampa
agano la tohara; basi Ibrahimu akamzaa Isaka, akamtahiri siku ya nane. Isaka
akamzaa Yakobo. Yakobo akawazaa wale kumi na wawili, wazee wetu.
9 Wale
wazee wetu wakimwonea wivu Yusufu, wakamwuza aende Misri. Mungu akawa pamoja
naye,
10 akamtoa
katika dhiki zake zote, akampa fadhili na hekima mbele ya Farao, mfalme wa
Misri; naye akamfanya awe mtawala juu ya Misri na nyumba yake yote.
11 Basi
kukawa njaa katika nchi yote ya Misri na Kanaani, na dhiki nyingi, wala baba
zetu hawakupata chakula cha kuwatosha.
12 Hata
Yakobo aliposikia ya kwamba huko Misri kuna nafaka, akawatuma baba zetu mara ya
kwanza.
13 Hata
safari ya pili Yusufu akajitambulisha kwa ndugu zake, jamaa ya Yusufu ikawa
dhahiri kwa Farao.
14 Yusufu
akatuma watu akamwita Yakobo babaye na jamaa zake wote pia, watu sabini na
watano.
15 Basi
Yakobo akashuka mpaka Misri; akafa yeye na baba zetu;
16 wakachukuliwa
mpaka Shekemu wakazikwa katika kaburi lile, ambalo Ibrahimu alilinunua kwa kima
cha fedha kwa wana wa Hamori, huko Shekemu.
17 Basi
wakati wa ile ahadi ambayo Mungu alimpa Ibrahimu ulipokuwa unakaribia, wale
watu wakazidi na kuongezeka sana huko Misri,
18 hata
mfalme mwingine akainuka juu ya Misri, asiyemfahamu Yusufu.
19 Huyo
akawafanyia hila kabila yetu, na kuwatenda mabaya baba zetu, akiwaamuru
wawatupe watoto wao wachanga, ili wasiishi.
20 Wakati
huo akazaliwa Musa, naye alikuwa mzuri sana, akalelewa muda wa miezi mitatu
katika nyumba ya babaye.
21 Hata
alipotupwa, binti Farao akamtwaa, akamlea awe kama mwanawe.
22 Musa
akafundishwa hekima yote ya Wamisri, akawa hodari wa maneno na matendo.
23 Umri
wake ulipopata kama miaka arobaini akaazimu moyoni mwake kwenda kuwatazama
ndugu zake Waisraeli.
24 Akamwona
mmoja akidhulumiwa, akamtetea, akamlipia kisasi yule aliyekuwa akionewa,
akampiga huyo Mmisri.
25 Alidhani
kwamba ndugu zake watafahamu ya kuwa Mungu anawapa wokovu kwa mkono wake,
lakini hawakufahamu.
26 Siku
ya pili yake akawatokea walipokuwa wakishindana, akataka kuwapatanisha,
akisema, Enyi bwana zangu, ninyi ni ndugu. Mbona mnadhulumiana?
27 Lakini
yeye aliyemdhulumu mwenziwe akamsukumia mbali, akisema, Ni nani aliyekuweka
wewe kuwa mkuu na mwamuzi juu yetu?
28 Je!
Wataka kuniua mimi kama ulivyomwua yule Mmisri jana?
29 Musa
akakimbia kwa neno hilo, akakaa hali ya ugeni katika nchi ya Midiani, akazaa
wana wawili huko.
30 Hata
miaka arobaini ilipotimia, malaika wa Bwana akamtokea katika jangwa la mlima wa
Sinai katika mwali wa moto, kijitini.
31 Musa
alipouona, akastaajabia maono yale, na alipokaribia ili atazame, sauti ya Bwana
ikamjia,
32 Mimi
ni Mungu wa baba zako, Mungu wa Ibrahimu, na Mungu wa Isaka, na Mungu wa
Yakobo. Musa akatetemeka, asithubutu kutazama.
33 Bwana
akamwambia, Vua viatu miguuni mwako, kwa maana mahali hapa unaposimama ni nchi
takatifu.
34 Yakini
nimeona mateso ya watu wangu waliomo Misri, nimesikia kuugua kwao, nami
nimeshuka niwatoe. Basi sasa, nitakutuma mpaka Misri.
35 Musa
huyo waliyemkataa, wakisema, Ni nani aliyekuweka kuwa mkuu na mwamuzi? Ndiye
aliyetumwa na Mungu kuwa mkuu na mkombozi, kwa mkono wa yule malaika
aliyemtokea katika kile kijiti.
36 Huyo
ndiye aliyewatoa, akifanya ajabu na ishara katika nchi ya Misri, na katika
bahari ya Shamu, na katika jangwa muda wa miaka arobaini.
37 Musa
huyo ndiye aliyewaambia Waisraeli, Bwana Mungu wenu atawainulieni nabii, katika
ndugu zenu, kama mimi; msikieni yeye.
38 Yeye
ndiye aliyekuwa katika kanisa jangwani pamoja na yule malaika aliyesema naye
katika mlima wa Sinai, tena pamoja na baba zetu; ndiye aliyepokea maneno ya
uzima atupe sisi.
39 Mtu
huyo baba zetu hawakutaka kumtii, bali wakamsukumia mbali, na kwa mioyo yao
wakarejea Misri,
40 wakamwambia
Haruni, Tufanyie miungu, watakaotutangulia; maana huyo Musa, aliyetutoa katika
nchi ya Misri, hatujui lililompata.
41 Wakafanya
ndama siku zile, wakaleta dhabihu kwa sanamu ile, wakafurahia kazi za mikono
yao.
42 Basi
Mungu akaghairi, akawaacha ili waliabudu jeshi la mbinguni, kama ilivyoandikwa
katika chuo cha manabii, Je! Mlinitolea mimi dhabihu na sadaka Miaka arobaini
katika jangwa, enyi nyumba ya Israeli?
43 Nanyi
mlichukua hema ya Moleki, Na nyota za mungu wenu Refani, Sanamu mlizozifanya
ili kuziabudu; Nami nitawafahamisha mwende mbali kupita Babeli.
44 Ile
hema ya ushahidi ilikuwa pamoja na baba zetu jangwani, kama alivyoagiza yeye
aliyesema na Musa, ya kwamba aifanye sawasawa na mfano ule aliouona;
45 ambayo
baba zetu, kwa kupokezana, wakaiingiza pamoja na Yoshua katika milki ya Mataifa
wale, ambao Mungu aliwafukuza mbele ya baba zetu, mpaka siku za Daudi;
46 aliyepata
fadhili mbele za Mungu, naye aliomba ampatie Mungu wa Yakobo maskani.
47 Lakini
Sulemani alimjengea nyumba.
48 Ila
Yeye aliye juu hakai katika nyumba zilizofanywa kwa mikono, kama vile asemavyo
nabii,
49 Mbingu
ni kiti changu cha enzi, Na nchi ni pa kuwekea miguu yangu; Ni nyumba gani
mtakayonijengea? Asema Bwana,
50 Au
ni mahali gani nitakapostarehe? Si mkono wangu uliofanya haya yote?
51 Enyi
wenye shingo gumu, msiotahiriwa mioyo wala masikio, siku zote mnampinga Roho
Mtakatifu; kama baba zenu walivyofanya, na ninyi ni vivyo hivyo.
52 Ni
yupi katika manabii ambaye baba zenu hawakumwudhi? Nao waliwaua wale
waliotabiri habari za kuja kwake yule Mwenye Haki; ambaye ninyi sasa mmekuwa
wasaliti wake, mkamwua;
53 ninyi
mlioipokea torati kwa agizo la malaika msiishike.
54 Basi
waliposikia maneno haya, wakachomwa mioyo, wakamsagia meno.
55 Lakini
yeye akijaa Roho Mtakatifu, akakaza macho yake, akitazama mbinguni, akauona
utukufu wa Mungu, na Yesu akisimama upande wa mkono wa kuume wa Mungu.
56 Akasema,
Tazama! Naona mbingu zimefunguka, na Mwana wa Adamu amesimama mkono wa kuume wa
Mungu.
57 Wakapiga
kelele kwa sauti kuu, wakaziba masikio yao, wakamrukia kwa nia moja,
58 wakamtoa
nje ya mji, wakampiga kwa mawe. Nao mashahidi wakaweka nguo zao miguuni pa
kijana mmoja aliyeitwa Sauli.
59 Wakampiga
kwa mawe Stefano, naye akiomba, akisema, Bwana Yesu, pokea roho yangu.
60 Akapiga
magoti, akalia kwa sauti kuu, Bwana, usiwahesabie dhambi hii. Akiisha kusema
haya akalala. Na Sauli alikuwa akiona vema kwa kuuawa kwake.