1 Siku
ile kukatukia adha kuu ya kanisa lililokuwa katika Yerusalemu; wote
wakatawanyika katika nchi ya Uyahudi na Samaria, isipokuwa hao mitume.
2 Watu
watauwa wakamzika Stefano, wakamfanyia maombolezo makuu.
3 Sauli
akaliharibu kanisa, akiingia kila nyumba, na kuwaburuta wanaume na wanawake na
kuwatupa gerezani.
4 Lakini
wale waliotawanyika wakaenda huko na huko wakilihubiri neno.
5 Filipo
akatelemka akaingia mji wa Samaria, akawahubiri Kristo.
6 Na
makutano kwa nia moja wakasikiliza maneno yale yaliyosemwa na Filipo
walipoyasikia na kuziona ishara alizokuwa akizifanya.
7 Kwa
maana pepo wachafu wakawatoka wengi waliopagawa nao, wakilia kwa sauti kuu; na
watu wengi waliopooza, na viwete, wakaponywa.
8 Ikawa
furaha kubwa katika mji ule.
9 Na
mtu mmoja, jina lake Simoni, hapo kwanza alikuwa akifanya uchawi katika mji
ule, akiwashangaza watu wa taifa la Wasamaria, akisema ya kuwa yeye ni mtu
mkubwa.
10 Wote
wakamsikiliza tangu mdogo hata mkubwa, wakisema, Mtu huyu ni uweza wa Mungu,
ule Mkuu.
11 Wakamsikiliza,
kwa maana amewashangaza muda mwingi kwa uchawi wake.
12 Lakini
walipomwamini Filipo, akizihubiri habari njema za ufalme wa Mungu, na jina lake
Yesu Kristo, wakabatizwa, wanaume na wanawake.
13 Na
yeye Simoni mwenyewe aliamini akabatizwa, akashikamana na Filipo; akashangaa
alipoziona ishara na miujiza mikubwa inayotendeka.
14 Na
mitume waliokuwako Yerusalemu, waliposikia ya kwamba Samaria imelikubali neno
la Mungu, wakawapelekea Petro na Yohana;
15 ambao
waliposhuka, wakawaombea wampokee Roho Mtakatifu;
16 kwa
maana bado hajawashukia hata mmoja wao, ila wamebatizwa tu kwa jina lake Bwana
Yesu.
17 Ndipo
wakaweka mikono yao juu yao, nao wakampokea Roho Mtakatifu.
18 Hata
Simoni alipoona ya kuwa watu wanapewa Roho Mtakatifu kwa kuwekewa mikono ya
mitume, akataka kuwapa fedha akisema,
19 Nipeni
na mimi uwezo huu, ili kila mtu nitakayemweka mikono yangu, apokee Roho
Mtakatifu.
20 Lakini
Petro akamwambia, Fedha yako na ipotelee mbali pamoja nawe, kwa kuwa umedhania
ya kuwa karama ya Mungu yapatikana kwa mali.
21 Huna
fungu wala huna sehemu katika jambo hili, kwa kuwa moyo wako si mnyofu mbele za
Mungu.
22 Basi,
tubia uovu wako huu, ukamwombe Bwana, ili kama yamkini, usamehewe fikira hii ya
moyo wako.
23 Kwa
maana nakuona u katika uchungu kama nyongo, na tena u katika kifungo cha uovu.
24 Simoni
akajibu, akasema, Niombeeni ninyi kwa Bwana, yasinifikilie mambo haya mliyosema
hata moja.
25 Nao
walipokwisha kushuhudia na kulihubiri neno la Bwana wakarudi Yerusalemu,
wakaihubiri Injili katika vijiji vingi vya Wasamaria.
26 Malaika
wa Bwana akasema na Filipo, akamwambia, Ondoka ukaende upande wa kusini hata njia
ile itelemkayo kutoka Yerusalemu kwenda Gaza; nayo ni jangwa.
27 Naye
akaondoka, akaenda; mara akamwona mtu wa Kushi, towashi, mwenye mamlaka chini
ya Kandake malkia wa Kushi, aliyewekwa juu ya hazina yake yote; naye alikuwa
amekwenda Yerusalemu kuabudu,
28 akawa
akirejea, ameketi garini mwake akisoma chuo cha nabii Isaya.
29 Roho
akamwambia Filipo, Sogea karibu na gari hili, ukashikamane nalo.
30 Basi
Filipo akaenda mbio, akamsikia anasoma chuo cha nabii Isaya; akanena, Je!
Yamekuelea haya unayosoma?
31 Akasema,
Nitawezaje kuelewa, mtu asiponiongoza? Akamsihi Filipo apande na kuketi pamoja
naye.
32 Na
fungu la Maandiko alilokuwa akilisoma ni hili, Aliongozwa kwenda machinjoni
kama kondoo, Na kama vile mwana-kondoo alivyo kimya mbele yake amkataye
manyoya, Vivyo hivyo yeye naye hafunui kinywa chake.
33 Katika
kujidhili kwake hukumu yake iliondolewa. Ni nani atakayeeleza kizazi chake? Kwa
maana uzima wake umeondolewa katika nchi.
34 Yule
towashi akamjibu Filipo, akasema, Nakuomba, nabii huyu; asema maneno haya kwa
habari ya nani; ni habari zake mwenyewe au za mtu mwingine?
35 Filipo
akafunua kinywa chake, naye, akianza kwa andiko lilo hilo, akamhubiri habari
njema za Yesu.
36 Wakawa
wakiendelea njiani, wakafika mahali penye maji; yule towashi akasema, Tazama,
maji haya; ni nini kinachonizuia nisibatizwe?
37 Filipo
akasema, Ukiamini kwa moyo wako wote, inawezekana. Akajibu, akanena, Naamini ya
kwamba Yesu Kristo ndiye Mwana wa Mungu.]
38 Akaamuru
lile gari lisimame; wakatelemka wote wawili majini, Filipo na yule towashi;
naye akambatiza.
39 Kisha,
walipopanda kutoka majini, Roho wa Bwana akamnyakua Filipo, yule towashi
asimwone tena; basi alikwenda zake akifurahi.
40 Lakini
Filipo akaonekana katika Azoto, na alipokuwa akipita akahubiri Injili katika
miji yote, hata akafika Kaisaria.