MITHALI - SURA YA 11

1 Mizani ya hadaa ni chukizo kwa Bwana; Bali vipimo vilivyo sawasawa humpendeza. 
2 Kijapo kiburi ndipo ijapo aibu; Bali hekima hukaa na wanyenyekevu. 
3 Ukamilifu wao wenye haki utawaongoza Bali ukaidi wao wenye fitina utawaangamiza. 
4 Mali hazifaidii kitu siku ya ghadhabu; Bali haki huokoa na mauti. 
5 Haki yake mtu mkamilifu itamwongoza njia yake; Bali mtu mwovu ataanguka kwa uovu wake. 
6 Haki yao wenye haki itawaokoa; Bali wafanyao fitina watanaswa kwa hila yao wenyewe. 
7 Mtu mwovu atakapokufa, taraja lake lapotea; Na matumaini ya uovu huangamia. 
8 Mwenye haki huokolewa katika dhiki, Na mtu mwovu ataiingia badala yake. 
9 Asiyemcha Mungu humpoteza jirani yake kwa kinywa chake; Bali wenye haki watapona kwa maarifa. 
10 Wenye haki wasitawipo, mji hufurahi; Waovu waangamiapo, watu hupiga kelele. 
11 Mji hutukuzwa kwa mbaraka wa mwenye haki; Bali mji hupinduliwa kwa kinywa cha mwovu. 
12 Asiye na akili humdharau mwenziwe; Bali mtu aliye na ufahamu hunyamaza. 
13 Mwenye kitango akisingizia hufunua siri; Bali mwenye roho ya uaminifu husitiri mambo. 
14 Pasipo mashauri taifa huanguka; Bali kwa wingi wa washauri huja wokovu. 
15 Amdhaminiye mgeni hakosi ataumia; Achukiaye mambo ya dhamana yu salama. 
16 Mwanamke wa adabu huheshimiwa daima; Na watu wakali hushika mali siku zote. 
17 Mwenye rehema huitendea mema nafsi yake; Aliye mkali hujisumbua mwili wake. 
18 Mtu mwovu hupata mshahara wa udanganyifu; Apandaye haki ana thawabu ya hakika. 
19 Haki huelekea uzima; Afuataye maovu hufuata mauti yake mwenyewe. 
20 Wenye kuhalifu moyoni ni chukizo kwa Bwana; Walio wakamilifu katika njia zao humpendeza. 
21 Hakika, mtu mwovu hatakosa adhabu; Bali wazao wa wenye haki wataokoka. 
22 Kama pete ya dhahabu katika pua ya nguruwe, Kadhalika mwanamke mzuri asiye na akili. 
23 Haja ya mwenye haki ni mema tu; Bali kutaraji kwake mtu mwovu ni ghadhabu. 
24 Kuna atawanyaye, lakini huongezewa zaidi; Kuna azuiaye isivyo haki, lakini huelekea uhitaji. 
25 Nafsi ya mtu mkarimu itawandishwa; Anyweshaye atanyweshwa mwenyewe. 
26 Awanyimaye watu nafaka, watu watamlaani; Auzaye nafaka, baraka itakuwa kichwani pake. 
27 Atafutaye mema kwa bidii hutafuta fadhili; Atafutaye madhara, hayo yatamjia. 
28 Azitegemeaye mali zake ataanguka; Mwenye haki atasitawi kama jani. 
29 Ataabishaye nyumba yake mwenyewe ataurithi upepo; Mpumbavu atakuwa mtumwa wa mtu mwenye moyo wa akili. 
30 Mazao ya mwenye haki ni mti wa uzima; Na mwenye hekima huvuta roho za watu. 
31 Tazama, mwenye haki atalipwa duniani; Basi mwovu na mkosaji si mara nyingi zaidi?

TUMA KWA RAFIKI :

Twitter FacebookMore

 
Kuhusu Huduma Hii | Masharti Ya Utumiaji Wa Tovuti Hii | Wasiliana Nasi | Tangaza Kupitia Tovuti Hii