MITHALI - SURA YA 12

1 Kila apendaye mafundisho hupenda maarifa; Bali yeye achukiaye kulaumiwa ni kama mnyama. 
2 Mtu mwema atapata upendeleo kwa Bwana; Bali mtu wa hila atahukumiwa naye. 
3 Mtu hatathibitika kwa njia ya uovu; Shina la mwenye haki halitaondolewa kamwe. 
4 Mwanamke mwema ni taji ya mumewe; Bali aaibishaye ni kama kuoza mifupani mwake. 
5 Mawazo ya mwenye haki ni adili; Bali mashauri ya mtu mwovu ni hadaa. 
6 Maneno ya waovu huotea damu; Bali kinywa cha wanyofu kitawaokoa. 
7 Waovu huangamia, hata hawako tena; Bali nyumba ya mwenye haki itasimama. 
8 Mtu atasifiwa kwa kadiri ya akili zake; Bali mwenye moyo wa ukaidi atadharauliwa. 
9 Afadhali mtu anayedharauliwa, ikiwa ana mtumwa, Kuliko ajisifuye, ikiwa anahitaji chakula. 
10 Mwenye haki huufikiri uhai wa mnyama wake; Bali huruma za mtu mwovu ni ukatili. 
11 Alimaye shamba lake atakuwa na chakula tele; Bali afuataye mambo ya upuzi hana ufahamu. 
12 Asiye haki hutamani nyavu za wabaya; Bali shina lao wenye haki huleta matunda. 
13 Katika kosa la midomo kuna mtego kwa mbaya; Bali mwenye haki atatoka katika taabu. 
14 Mtu atashiba mema kwa matunda ya kinywa chake; Na atarudishiwa matendo ya mikono yake. 
15 Njia ya mpumbavu imenyoka machoni pake mwenyewe; Bali yeye aliye na hekima husikiliza shauri. 
16 Ghadhabu ya mpumbavu hujulika mara; Bali mtu mwerevu husitiri aibu. 
17 Atamkaye maneno ya kweli hufunua haki; Bali shahidi wa uongo hutamka hila. 
18 Kuna anenaye bila kufikiri, kama kuchoma kwa upanga; Bali ulimi wa mwenye haki ni afya. 
19 Mdomo wa kweli utathibitishwa milele; Bali ulimi wa uongo ni wa kitambo tu. 
20 Hila imo mioyoni mwao wafikirio uovu; Bali wafanyao mashauri ya amani, kwao kuna furaha. 
21 Mwenye haki hatapatikana na msiba wo wote; Bali wasio haki watajazwa mabaya. 
22 Midomo ya uongo ni chukizo kwa Bwana; Bali watendao uaminifu ndio furaha yake. 
23 Mwanadamu mwenye busara husitiri maarifa; Bali moyo wa wapumbavu hutangaza upumbavu. 
24 Mkono wa mwenye bidii utatawala; Bali mvivu atalipishwa kodi. 
25 Uzito katika moyo wa mtu huuinamisha; Bali neno jema huufurahisha. 
26 Mwenye haki ni kiongozi cha mwenzake; Bali njia ya wasio haki huwakosesha. 
27 Mtu mvivu hapiki mawindo yake; Bali mwenye bidii anazo mali za thamani. 
28 Katika njia ya haki kuna uhai; Wala hakuna mauti katika mapito yake.

TUMA KWA RAFIKI :

Twitter FacebookMore

 
Kuhusu Huduma Hii | Masharti Ya Utumiaji Wa Tovuti Hii | Wasiliana Nasi | Tangaza Kupitia Tovuti Hii