1 Basi,
siku sita kabla ya Pasaka, Yesu alifika Bethania, alipokuwapo Lazaro, yeye
ambaye Yesu alimfufua katika wafu.
2 Basi
wakamwandalia karamu huko; naye Martha akatumikia; na Lazaro alikuwa mmojawapo
wa wale walioketi chakulani pamoja naye.
3 Basi
Mariamu akatwaa ratli ya marhamu ya nardo safi yenye thamani nyingi, akampaka
Yesu miguu, akamfuta miguu kwa nywele zake. Nayo nyumba pia ikajaa harufu ya
marhamu.
4 Basi
Yuda Iskariote, mmojawapo wa wanafunzi wake, ambaye ndiye atakaye kumsaliti,
akasema,
5 Mbona
marhamu hii haikuuzwa kwa dinari mia tatu, wakapewa maskini?
6 Naye
aliyasema hayo, si kwa kuwahurumia maskini; bali kwa kuwa ni mwivi, naye ndiye
aliyeshika mfuko, akavichukua vilivyotiwa humo.
7 Basi
Yesu alisema, Mwache aiweke kwa siku ya maziko yangu.
8 Kwa
maana maskini mnao sikuzote pamoja nanyi; bali mimi hamnami sikuzote.
9 Basi
watu wengi katika Wayahudi walipata kujua ya kuwa yeye yuko huko, nao wakaja,
si kwa ajili yake Yesu tu, ila wamwone na Lazaro, ambaye Yesu alimfufua katika
wafu.
10 Nao
wakuu wa makuhani wakafanya shauri la kumwua Lazaro naye;
11 maana
kwa ajili yake wengi katika Wayahudi walijitenga, wakamwamini Yesu.
12 Nayo
siku ya pili yake watu wengi walioijia sikukuu walisikia ya kwamba Yesu anakuja
Yerusalemu;
13 wakatwaa
matawi ya mitende, wakatoka nje kwenda kumlaki, wakapiga makelele, Hosana!
Ndiye mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana, Mfalme wa Israeli!
14 Naye
Yesu alikuwa amepata mwana-punda, akampanda, kama vile iliyoandikwa,
15 Usiogope,
binti Sayuni; tazama, Mfalme wako anakuja, amepanda mwana-punda.
16 Mambo
hayo wanafunzi wake hawakuyafahamu hapo kwanza; lakini Yesu alipotukuzwa, ndipo
walipokumbuka ya kwamba ameandikiwa hayo, na ya kwamba walimtendea hayo.
17 Basi
wakamshuhudia wale mkutano waliokuwapo pamoja naye alipomwita Lazaro kutoka
kaburini, akamfufua.
18 Na
kwa sababu hiyo mkutano walikwenda kumlaki, kwa kuwa wamesikia ya kwamba
ameifanya ishara hiyo.
19 Basi
Mafarisayo wakasemezana wao kwa wao, Mwaona kwamba hamfai neno lo lote;
tazameni, ulimwengu umekwenda nyuma yake.
20 Palikuwa
na Wayunani kadha wa kadha miongoni mwa watu waliokwea kwenda kuabudu kwenye
sikukuu.
21 Basi
hao walimwendea Filipo, mtu wa Bethsaida ya Galilaya, wakamwomba, wakisema,
Bwana, sisi tunataka kumwona Yesu.
22 Filipo
akaenda, akamwambia Andrea; kisha Andrea na Filipo wakamwambia Yesu.
23 Naye
Yesu akawajibu, akasema, Saa imefika atukuzwe Mwana wa Adamu.
24 Amin,
amin, nawaambia, Chembe ya ngano isipoanguka katika nchi, ikafa, hukaa hali iyo
hiyo peke yake; bali ikifa, hutoa mazao mengi.
25 Yeye
aipendaye nafsi yake ataiangamiza; naye aichukiaye nafsi yake katika ulimwengu
huu ataisalimisha hata uzima wa milele.
26 Mtu
akinitumikia, na anifuate; nami nilipo, ndipo na mtumishi wangu atakapokuwapo.
Tena mtu akinitumikia, Baba atamheshimu.
27 Sasa
roho yangu imefadhaika; nami nisemeje? Baba, uniokoe katika saa hii? Lakini ni
kwa ajili ya hayo nilivyoifikia saa hii.
28 Baba,
ulitukuze jina lako. Basi ikaja sauti kutoka mbinguni, Nimelitukuza, nami
nitalitukuza tena.
29 Basi
mkutano uliosimama karibu wakasikia, walisema ya kwamba kumekuwa ngurumo;
wengine walisema, Malaika amesema naye.
30 Yesu
akajibu, akasema, Sauti hiyo haikuwako kwa ajili yangu, bali kwa ajili yenu.
31 Sasa
hukumu ya ulimwengu huu ipo; sasa mkuu wa ulimwengu huu atatupwa nje.
32 Nami
nikiinuliwa juu ya nchi, nitawavuta wote kwangu.
33 Aliyanena
hayo akionyesha ni mauti gani atakayokufa.
34 Basi
mkutano wakamjibu, Sisi tumesikia katika torati ya kwamba Kristo adumu hata
milele; nawe wasemaje ya kwamba imempasa Mwana wa Adamu kuinuliwa? Huyu Mwana
wa Adamu ni nani?
35 Basi
Yesu akawaambia, Nuru ingaliko pamoja nanyi muda kidogo. Enendeni maadamu mnayo
nuru hiyo, giza lisije likawaweza; maana aendaye gizani hajui aendako.
36 Maadamu
mnayo nuru, iaminini nuru hiyo, ili mpate kuwa wana wa nuru. Hayo aliyasema
Yesu, akaenda zake, akajificha wasimwone.
37 Walakini
ajapokuwa amefanya ishara nyingi namna hiyo mbele yao, hawakumwamini;
38 ili
litimie lile neno la nabii Isaya alilolisema, Bwana, ni nani aliyezisadiki
habari zetu; Na mkono wa Bwana amefunuliwa nani?
39 Ndiyo
sababu wao hawakuweza kusadiki; kwa maana Isaya alisema tena,
40 Amewapofusha
macho, Ameifanya mizito mioyo yao; Wasije wakaona kwa macho yao, Wakafahamu kwa
mioyo yao, Wakaongoka, nikawaponya.
41 Maneno
hayo aliyasema Isaya, kwa kuwa aliuona utukufu wake, akataja habari zake.
42 Walakini
hata katika wakuu walikuwamo wengi waliomwamini; lakini kwa sababu ya Mafarisayo
hawakumkiri, wasije wakatengwa na sinagogi.
43 Kwa
maana walipenda utukufu wa wanadamu kuliko utukufu wa Mungu.
44 Naye
Yesu akapaza sauti, akasema, Yeye aniaminiye mimi, haniamini mimi bali yeye
aliyenipeleka.
45 Naye
anitazamaye mimi amtazama yeye aliyenipeleka.
46 Mimi
nimekuja ili niwe nuru ya ulimwengu, ili kila mtu aniaminiye mimi asikae
gizani.
47 Na
mtu akiyasikia maneno yangu, asiyashike, mimi simhukumu; maana sikuja ili
niuhukumu ulimwengu, ila niuokoe ulimwengu.
48 Yeye
anikataaye mimi, asiyeyakubali maneno yangu, anaye amhukumuye; neno hilo
nililolinena ndilo litakalomhukumu siku ya mwisho.
49 Kwa
sababu mimi sikunena kwa nafsi yangu tu; bali Baba aliyenipeleka, yeye mwenyewe
ameniagiza nitakayonena na nitakayosema.
50 Nami
najua ya kuwa agizo lake ni uzima wa milele; basi hayo ninenayo mimi, kama Baba
alivyoniambia, ndivyo ninenavyo.