1 Msifadhaike
mioyoni mwenu; mnamwamini Mungu, niaminini na mimi.
2 Nyumbani
mwa Baba yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia; maana naenda
kuwaandalia mahali.
3 Basi
mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili
nilipo mimi, nanyi mwepo.
4 Nami
niendako mwaijua njia.
5 Tomaso
akamwambia, Bwana, sisi hatujui uendako; nasi twaijuaje njia?
6 Yesu
akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa
njia ya mimi.
7 Kama
mngalinijua mimi, mngalimjua na Baba; tangu sasa mnamjua, tena mmemwona.
8 Filipo
akamwambia, Bwana, utuonyeshe Baba, yatutosha.
9 Yesu
akamwambia, Mimi nimekuwapo pamoja nanyi siku hizi zote, wewe usinijue, Filipo?
Aliyeniona mimi amemwona Baba; basi wewe wasemaje, Utuonyeshe Baba?
10 Husadiki
ya kwamba mimi ni ndani ya Baba, na Baba yu ndani yangu? Hayo maneno
niwaambiayo mimi siyasemi kwa shauri langu; lakini Baba akaaye ndani yangu
huzifanya kazi zake.
11 Mnisadiki
ya kwamba mimi ni ndani ya Baba, na Baba yu ndani yangu; la! Hamsadiki hivyo,
sadikini kwa sababu ya kazi zenyewe.
12 Amin,
amin, nawaambieni, Yeye aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo mimi, yeye naye
atazifanya; naam, na kubwa kuliko hizo atafanya, kwa kuwa mimi naenda kwa Baba.
13 Nanyi
mkiomba lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya
Mwana.
14 Mkiniomba
neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya.
15 Mkinipenda,
mtazishika amri zangu.
16 Nami
nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele;
17 ndiye
Roho wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala
haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu.
18 Sitawaacha
ninyi yatima; naja kwenu.
19 Bado
kitambo kidogo na ulimwengu haunioni tena; bali ninyi mnaniona. Na kwa sababu
mimi ni hai, ninyi nanyi mtakuwa hai.
20 Siku
ile ninyi mtatambua ya kuwa mimi ni ndani ya Baba yangu, nanyi ndani yangu,
nami ndani yenu.
21 Yeye
aliye na amri zangu, na kuzishika, yeye ndiye anipendaye; naye anipendaye
atapendwa na Baba yangu; nami nitampenda na kujidhihirisha kwake.
22 Yuda
(siye Iskariote), akamwambia, Bwana, imekuwaje ya kwamba wataka kujidhihirisha
kwetu, wala si kwa ulimwengu?
23 Yesu
akajibu, akamwambia, Mtu akinipenda, atalishika neno langu; na Baba yangu
atampenda; nasi tutakuja kwake, na kufanya makao kwake.
24 Mtu
asiyenipenda, yeye hayashiki maneno yangu; nalo neno mnalolisikia silo langu,
ila ni lake Baba aliyenipeleka.
25 Hayo
ndiyo niliyowaambia wakati nilipokuwa nikikaa kwenu.
26 Lakini
huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu,
atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia.
27 Amani
nawaachieni; amani yangu nawapa; niwapavyo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo.
Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiwe na woga.
28 Mlisikia
ya kwamba mimi naliwaambia, Naenda zangu, tena naja kwenu. Kama mngalinipenda,
mngalifurahi kwa sababu naenda kwa Baba, kwa maana Baba ni mkuu kuliko mimi.
29 Na
sasa nimewaambia kabla halijatokea, kusudi litakapotokea mpate kuamini.
30 Mimi
sitasema nanyi maneno mengi tena, kwa maana yuaja mkuu wa ulimwengu huu, wala
hana kitu kwangu.
31 Lakini
ulimwengu ujue ya kuwa nampenda Baba; na kama vile Baba alivyoniamuru; ndivyo
nifanyavyo. Ondokeni, twendeni zetu.