ZABURI - SURA YA 141

1 Ee Bwana, nimekuita, unijie hima, Uisikie sauti yangu nikuitapo. 
2 Sala yangu ipae mbele zako kama uvumba, Kuinuliwa mikono yangu kama dhabihu ya jioni. 
3 Ee Bwana, uweke mlinzi kinywani pangu, Mngojezi mlangoni pa midomo yangu. 
4 Usiuelekeze moyo wangu kunako jambo baya, Nisiyazoelee matendo yasiyofaa, Pamoja na watu watendao maovu; Wala nisile vyakula vyao vya anasa. 
5 Mwenye haki na anipige, itakuwa fadhili; Anikemee, itakuwa kama mafuta kichwani; Kichwa changu kisikatae, Maana siachi kusali kati ya mabaya yao. 
6 Makadhi wao wakiangushwa kando ya genge, Watayasikia maneno yangu, maana ni matamu. 
7 Kama kupasua kuni na kuzichanja juu ya nchi, Ndivyo ilivyo mifupa yetu mdomoni pa kuzimu. 
8 Macho yangu yanakuelekea Wewe, MUNGU Bwana, Nimekukimbilia Wewe, usiniache nafsi yangu. 
9 Unilinde na mtego walionitegea, Na matanzi yao watendao maovu. 
10 Wabaya na waanguke katika nyavu zao wenyewe, Pindi mimi ninapopita salama.

TUMA KWA RAFIKI :

Twitter FacebookMore

 
Kuhusu Huduma Hii | Masharti Ya Utumiaji Wa Tovuti Hii | Wasiliana Nasi | Tangaza Kupitia Tovuti Hii