ZABURI - SURA YA 86

1 Ee Bwana, utege sikio lako unijibu, Maana mimi ni maskini na mhitaji 
2 Unihifadhi nafsi yangu, Maana mimi ni mcha Mungu. Wewe uliye Mungu wangu, Umwokoe mtumishi wako anayekutumaini. 
3 Wewe, Bwana, unifadhili, Maana nakulilia Wewe mchana kutwa. 
4 Uifurahishe nafsi ya mtumishi wako, Maana nafsi yangu nakuinulia Wewe, Bwana. 
5 Kwa maana Wewe, Bwana, U mwema, Umekuwa tayari kusamehe, Na mwingi wa fadhili, Kwa watu wote wakuitao. 
6 Ee Bwana, uyasikie maombi yangu; Uisikilize sauti ya dua zangu. 
7 Siku ya mateso yangu nitakuita, Kwa maana utaniitikia. 
8 Katikati ya miungu hakuna kama Wewe, Bwana, Wala matendo mfano wa matendo yako. 
9 Mataifa yote uliowafanya watakuja; Watakusujudia Wewe, Bwana, Watalitukuza jina lako; 
10 Kwa kuwa ndiwe uliye mkuu, Wewe ndiwe mfanya miujiza, Ndiwe Mungu peke yako. 
11 Ee Bwana, unifundishe njia yako; Nitakwenda katika kweli yako; Moyo wangu na ufurahi kulicha jina lako; 
12 Nitakusifu Wewe, Bwana, Mungu wangu, Kwa moyo wangu wote, Nitalitukuza jina lako milele. 
13 Maana fadhili zako kwangu ni nyingi sana; Umeiopoa nafsi yangu na kuzimu. 
14 Ee Mungu, wenye kiburi wamenishambulia; Mkutano wa wakatili wamenitafuta roho. Wala hawakukuweka Wewe Mbele ya macho yao. 
15 Lakini Wewe, Bwana, U Mungu wa rehema na neema, Mvumilivu, mwingi wa fadhili na kweli. 
16 Unielekee na kunifadhili mimi; Mpe mtumishi wako nguvu zako, Umwokoe mwana wa mjakazi wako. 
17 Unifanyie ishara ya wema, Wanichukiao waione na kuaibishwa. Kwa kuwa Wewe, Bwana, Umenisaidia na kunifariji.

TUMA KWA RAFIKI :

Twitter FacebookMore

 
Kuhusu Huduma Hii | Masharti Ya Utumiaji Wa Tovuti Hii | Wasiliana Nasi | Tangaza Kupitia Tovuti Hii