1 Akawaambia
mfano, ya kwamba imewapasa kumwomba Mungu sikuzote, wala wasikate tamaa.
2 Akasema,
Palikuwa na kadhi katika mji fulani, hamchi Mungu, wala hajali watu.
3 Na
katika mji huo palikuwa na mwanamke mjane, aliyekuwa akimwendea-endea, akisema,
Nipatie haki na adui wangu.
4 Naye
kwa muda alikataa; halafu akasema moyoni mwake, Ijapokuwa simchi Mungu wala
sijali watu,
5 lakini,
kwa kuwa mjane huyu ananiudhi, nitampatia haki yake, asije akanichosha kwa
kunijia daima.
6 Bwana
akasema, Sikilizeni asemavyo yule kadhi dhalimu.
7 Na
Mungu, je! Hatawapatia haki wateule wake wanaomlilia mchana na usiku, naye ni
mvumilivu kwao?
8 Nawaambia,
atawapatia haki upesi; walakini, atakapokuja Mwana wa Adamu, je! Ataiona imani
duniani?
9 Akawaambia
mfano huu watu waliojikinai ya kuwa wao ni wenye haki, wakiwadharau wengine
wote.
10 Watu
wawili walipanda kwenda hekaluni kusali, mmoja Farisayo, wa pili mtoza ushuru.
11 Yule
Farisayo akasimama akiomba hivi moyoni mwake; Ee Mungu, nakushukuru kwa kuwa
mimi si kama watu wengine, wanyang'anyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu
mtoza ushuru.
12 Mimi
nafunga mara mbili kwa juma; hutoa zaka katika mapato yangu yote.
13 Lakini
yule mtoza ushuru alisimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua macho yake
mbinguni, bali alijipiga-piga kifua akisema, Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye
dhambi.
14 Nawaambia,
huyu alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko yule; kwa maana
kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa.
15 Wakamletea
na watoto wachanga ili awaguse; lakini wanafunzi walipoona waliwakemea.
16 Bali
Yesu akawaita waje kwake, akasema, Waacheni watoto wadogo waje kwangu, wala
msiwazuie, kwa kuwa watu kama hao ufalme wa Mungu ni wao.
17 Amin,
nawaambia, Mtu ye yote asiyeupokea ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo hauingii
kamwe.
18 Tena,
mtu mkubwa mmoja alimwuliza, akisema, Mwalimu mwema, nifanye nini ili nipate
kuurithi uzima wa milele?
19 Yesu
akamwambia, Mbona unaniita mwema? Hakuna aliye mwema ila mmoja, naye ndiye
Mungu.
20 Wazijua
amri; Usizini, Usiue, Usiibe, Usishuhudie uongo, Waheshimu baba yako na mama
yako.
21 Akasema,
Hayo yote nimeyashika tangu utoto wangu.
22 Yesu
aliposikia hayo alimwambia, Umepungukiwa na neno moja bado; viuze ulivyo navyo
vyote, ukawagawanyie maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha, njoo
unifuate.
23 Lakini
aliposikia hayo alihuzunika sana, maana alikuwa na mali nyingi.
24 Yesu
alipoona vile alisema, Kwa shida gani wenye mali watauingia ufalme wa Mungu!
25 Kwa
maana ni vyepesi ngamia kupita katika tundu la sindano kuliko tajiri kuingia
katika ufalme wa Mungu.
26 Nao
waliosikia walisema, Ni nani basi awezaye kuokoka?
27 Akasema,
Yasiyowezekana kwa wanadamu yawezekana kwa Mungu.
28 Petro
akasema, Tazama, sisi tumeviacha vitu vyetu vyote na kukufuata.
29 Akawaambia,
Hakika nawaambia, hakuna mtu aliyeacha nyumba, au mke, au ndugu, au wazazi, au
wana, kwa ajili ya ufalme wa Mungu,
30 asiyepokea
zaidi mara nyingi katika zamani hizi, na katika ulimwengu ujao uzima wa milele.
31 Akawachukua
wale Thenashara, akawaambia, Tazameni, tunapanda kwenda Yerusalemu, na mambo
yote yatatimizwa, Mwana wa Adamu aliyoandikiwa na manabii.
32 Kwa
kuwa atatiwa mikononi mwa Mataifa, atafanyiwa dhihaka; atatendwa jeuri, na
kutemewa mate;
33 nao
watampiga mijeledi, kisha watamwua; na siku ya tatu atafufuka.
34 Walakini
hawakuelewa maneno hayo hata kidogo, na jambo hilo lilikuwa limefichwa kwao,
wala hawakufahamu yaliyonenwa.
35 Ikawa
alipokaribia Yeriko, mtu mmoja kipofu alikuwa ameketi kando ya njia, akiomba
sadaka;
36 na
alipowasikia makutano wakipita, aliuliza, Kuna nini?
37 Wakamwambia,
Yesu wa Nazareti anapita.
38 Akapiga
kelele, akisema, Yesu, Mwana wa Daudi, unirehemu.
39 Basi
wale waliotangulia wakamkemea ili anyamaze; lakini yeye alizidi sana kupaza
sauti, Ee Mwana wa Daudi, unirehemu.
40 Yesu
akasimama, akaamuru aletwe kwake; na alipomkaribia, alimwuliza,
41 Wataka
nikufanyie nini? Akasema, Bwana, nipate kuona.
42 Yesu
akamwambia, Upewe kuona; imani yako imekuponya.
43 Mara
hiyo akapata kuona, akamfuata, huku akimtukuza Mungu. Na watu wote walipoona
hayo walimsifu Mungu.